Loliondo. Polisi wawili, PC Isaack na PC Mabrouk wamejeruhiwa baada ya kupigwa na vijana wanaodaiwa kuwa ni Wamasai (morani) katika Kijiji cha Ololosokwani, Tarafa ya Loliondo wilayani Ngorongoro.
Tukio hilo pia limesababisha watu 25 kutiwa nguvuni, akiwamo mbunge wa zamani wa Jimbo la Ngorongoro, Merthew ole Timan na madiwani wawili.
Inadaiwa tukio hilo limetokana na kuchochewa na uhasama kati ya wananchi na polisi kutokana na migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo, limesababisha PC Isaack kuvunjwa mkono na jana alihamishiwa Hospitali ya Seliani Arusha Medical Center kwa matibabu zaidi baada ya hali yake kuwa mbaya.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Hashimu Mgandilwa alisema watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
“Ni kweli polisi wawili wamepigwa na jeshi liliendesha msako wa kuwatafuta watuhumiwa na kufanikiwa kuwakamata watu 25 kwa tuhuma za kushambulia polisi, uchochezi, kufanya mikusanyiko isiyo halali na kupanga mbinu za uhalifu,” alisema Mgandilwa.
Alisema chanzo cha kupigwa polisi ni operesheni ya kuchunguza wahamiaji haramu ambayo inapingwa na wananchi na viongozi wa eneo hilo.
Hata hivyo, viongozi waliokamatwa kuhusu tukio hilo, jana walipata dhamana.
Diwani wa Kata ya Ololosokwani, Iyanick Ndoinyo na Diwani wa Oldonyosambu Daniel Ngoitiko, walisema wanapinga tukio la kupigwa polisi hao, lakini chanzo ni polisi kukamata pikipiki za wananchi na kudai faini kubwa.
Iyanick alisema ingawa ni kweli kuna uhasama wa polisi na wananchi, lakini taarifa alizopata ni kwamba polisi wadai faini kubwa na kisha kumpiga kijana mmoja wa Kimasai.
“Sisi kama viongozi tunapinga kupigwa polisi, pia kukamatwa kwetu ni kudhalilishwa,” alisema.
Alisema, “Hatupingi hatua ya Serikali kuwaondoa wahamiaji haramu kutoka nchi jirani.”
Naye Ngoitiko alisema wao kama viongozi wanalaani tukio hilo na wanataka Serikali kufanya uchunguzi kujua chanzo badala ya kukamata watu bila kuwa na ushahidi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ololosokwani, Kerry Dukunyi ambaye ni mmoja ya waliokamatwa, alisema amedhalilishwa kwa kutembezwa kwa miguu kilomita nane kutoka Halmashauri ya Ngorongoro hadi Mji wa Loliondo.
“Tunapinga kupigwa polisi, lakini pia hatujafurahishwa jinsi polisi walivyotudhalilisha mbele ya wananchi wetu,” alisema Ndoinyo.
Mkuu wa wilaya hiyo, Mgandilwa alisema wanasiasa hao wamekamatwa kutokana na kubainika walikuwa wakienda maeneo ya Posimori, Kenya na kuitisha mikutano na wakazi wa huko, jambo ambalo kinyume na sheria.
“Tatizo hapa kuna koo zinaingiliana maeneo ya mipakani hasa jamii ya Wamasai wa Purko. Unaweza kukuta familia moja inaishi Kenya na nyingine Tanzania. Hili ni tatizo,” alisema Mgandilwa.
Hata hivyo, Diwani Ndoinyo alisema vikao walivyofanya ni kwa ajili ya kudumisha amani katika eneo lao.
Kwa zaidi ya miaka zaidi ya 20 sasa wilaya hiyo ina migogoro ya ardhi baina ya jamii za Wamasai na Wasonjo, wananchi na wawekezaji.
No comments:
Post a Comment