MAAFA zaidi yaliyosababishwa na mvua iliyonyesha kwa zaidi ya saa 48 mfululizo jijini Dar es Salaam, yameendelea kutokea ambapo mbali na vifo vya watu watano, mamia ya nyumba zimefunikwa na maji.
Taarifa ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam iliyotolewa jana, mbali na kutaja majina ya waliofikwa na mauti, pia imeeleza kuwa wakazi ambao nyumba zao zimefunikwa na maji, wamepatiwa hifadhi katika kambi za dharura zilizopo katika shule mbalimbali za Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova, zaidi ya wakazi 300 wa Kata ya Jangwani wamekimbia makazi yao baada ya nyumba zinazokadiriwa kuwa kati ya 90 hadi 100, kufunikwa na maji.
Hali hiyo imejitokeza pia katika Kata ya Mchikichini, ambako nyumba zinazokadiriwa kuwa kati ya 60 hadi 70, zimefunikwa na maji na wakazi wake tayari wamehama kutekeleza agizo la Serikali, lililowataka wahame maeneo hayo.
Hata hivyo, ingawa walioharibiwa makazi yao ni zaidi ya 300, ni wakazi kati ya 25 hadi 30 tu, waliokwenda katika kambi ya dharura, iliyoandaliwa katika Shule ya Sekondari Mchikichini.
Waliokufa Kwa mujibu wa Kamanda Kova, watu watano wamekufa katika mafuriko hayo, akiwemo Shaban Idd (73), mkazi wa Manzese aliyesombwa na maji wakati akijaribu kuvuka Mto Ng’ombe.
Alisema Shaban alisombwa na maji Jumatano ya Mei 6, mwaka huu, katika maeneo ya Magomeni wilayani Kinondoni na mwili wake ulipatikana kesho yake Mei 7, mwaka huu na kupelekwa katika Hospitali ya Mwananyamala kuhifadhiwa.
Kifo kingine ni cha mkazi wa Mwananyamala Mbuyuni, Masumbuko Douglass mwenye miaka kati ya 50-55, ambaye alianguka na kufa ghafla wakati akitoa maji yaliyoingia nyumbani kwake.
‘’Uchunguzi wa awali umebaini kuwa Douglass alikuwa na ugonjwa wa kifafa, hivyo wakati akihangaika kutoa maji, ugonjwa huo ulimpata na kuanguka kwenye maji na kufa baada ya kukosa msaada,’’ alisema Kova. Alisema mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi zaidi.
Katika tukio la tatu, Jumatano ya Mei 6, mwaka huu, Rashid Hassan (36), mkazi wa maeneo ya Mvuruhani Pemba Mnazikigambo, alizama katika mkondo wa maji yanayokwenda baharini.
Kamanda Kova alisema kuwa mwili wa Hassan ulipatikana Mei 7, mwaka huu, ukiwa unaelea umbali wa meta 500 kutoka eneo alilozama.
Aidha, mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi sita, aliyekuwa akiishi na wazazi wake Yombo Makangarawe, Gloria Mrema, alipotea baada ya watoto wenzake wawili kumuacha wakati wakicheza pamoja.
Alisema juhudi za kumtafuta mtoto huyo zilifanyika bila ya mafanikio hadi mwili wake ulipopatikana ukiwa unaelea katika Mto Mzinga ambako uliopolewa na kupelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya Temeke.
Mkazi wa maeneo ya Kinondoni Mkwajuni mwanamume ambaye jina lake halikufahamika mwenye umri wa miaka 40-45 alikutwa amekufa. Mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa uchunguzi,’’ alifafanua Kova.
Majeruhi Mbali na maafa hayo, mkulima Mabula Mosses (65) mkazi wa Vingunguti, Buguruni wilayani Ilala, alivunjika mguu wa kulia sehemu ya chini ya goti, baada ya kuangukiwa na ukuta wa ghala la Fidas Hussein lililopakana na nyumba yake.
Kova alisema ukuta huo pia ulisababisha uharibifu wa vitu mbalimbali na majeruhi amepelekwa katika Hospitali ya Amana kwa matibabu.
Maeneo yaliyoathirika Akielezea zaidi kuhusu maafa hayo, Kova alisema maeneo yaliyoathirika zaidi na mvua zinazoendelea kunyesha ni Keko, Chang’ombe Maduka Mawili, Yombo Vituka, Vingunguti na Afrikana.
Pia alisema maeneo mengine ni Msasani Bonde la Mpunga, Jangwani, Kigogo, Mburahati, Boko Basihaya pamoja na maeneo mengine ambayo taarifa zake hazijapokelewa.
Vilevile alisema kuwa barabara zinazounganisha katikati na pembezoni ya Jiji, zimeharibika kiasi cha kulazimu Jeshi la Polisi kutoa maelekezo ili barabara hizo zifungwe kupunguza madhara ambayo yangetokea.
Mbali na barabara, alisema pia kuna madaraja mbalimbali yameharibika na kukata mawasiliano kutoka upande mmoja kwenda mwingine. ‘’Kwa mfano daraja linalounganisha Mbagala na Kijichi maarufu kama Njia ya Ng’ombe, limeharibika kutokana na mafuriko hayo, ’’ alisema Kova.
Pia alisisitiza kuwa jeshi hilo kwa kushirikiana na Serikali, limejipanga kukabili foleni kwa kuhusisha askari wa vikosi mbalimbali, ili kukabiliana na tatizo hilo ambalo kwa kiasi kikubwa limesababisha uharibifu wa miundombinu.
Ubishi wamkera RC Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, amesisitiza wananchi waishio maeneo ya mabondeni kuhama ili kuepuka athari zinazotokana na mafuriko ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha jijini humo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Sadiki alisema anasikitishwa na wananchi ambao bado wamekaidi kuhama na kuendelea kuvumilia katika maeneo hatarishi bila kuhofia usalama wao. “Tulishawaambia wananchi wanaoishi mabondeni na maeneo hatarishi waondoke kwa hiari yao, lakini baadhi yao walikaidi na wengine wametupeleka mahakamani.
“Sasa nawaambia kwa mara nyingine tena wajisaidie wenyewe kwa kuhama ili kuokoa familia zao kwa kuwa wanapozidi kukaidi, wanawatesa watoto wao… nawapa pole sana waliofikwa na matatizo,” alisema.
Alisema tathmini ya uharibifu uliotokana na mvua hizo haijafanyika kwa kuwa bado mvua zinaendelea, hivyo zitakapokoma watafanya tathmini na kutoa taarifa.
Wanafunzi warudishwa Katika maeneo mengine, gazeti hili lilishuhudia baadhi ya shule zikiwa zimefungwa huku wanafunzi wakishindwa kufika shuleni na wengine wakiruhusiwa kuondoka mapema kwenda nyumbani kuhofia tabu ya usafiri.
HabariLeo ilishuhudia walimu katika Shule ya Mtendeni iliyopo katikati ya Jiji, wakiruhusu wanafunzi kuondoka mapema shuleni hapo kwa kuhofia shida ya usafiri kutokana na mvua.
Mwalimu mmoja wa kike ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake, alisema wanafunzi wengi shuleni hapo hawakufika kutokana na mvua kuharibu miundombinu ya barabara katika maeneo wanayotokea.
Pia mkazi wa Mbagala, Timothy Andrew, alisema katika maeneo ya Mtongani nyumba nyingi na barabara zimejaa maji na mitaro imefurika.
Imeandikwa na Francisca Emmanuel, Hellen Mlacky na Lucy Ngowi.
No comments:
Post a Comment