Wednesday 6 May 2015

KI-MOON: DUNIA INA IMANI NA KIKWETE

Katibu Mkuu wa Umoja wa Maaifa, Ban Ki-moon akimkaribisha Rais Jakaya Kikwete katika ofisi yake jijini New York, Marekani ambapo Rais Kikwete aliongoza kikao cha kutafuta majawabu ya dunia kuhusu athari za magonjwa ya milipuko. (Picha na Freddy Maro).
KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon amesema dunia ina imani kubwa na Rais Jakaya Kikwete na wajumbe wengine wa Jopo la Watu Maarufu Duniani waliopewa jukumu la kutafuta jinsi dunia inavyoweza kukabiliana na magonjwa ya milipuko, kama vile ebola, katika siku zijazo.


Aidha, Ki-moon amewaambia wajumbe hao kuwa uteuzi wao uliofanywa na yeye mwenyewe mwezi uliopita umefanyika baada ya majina yao kuwa yamependekezwa na taasisi nyingine za kimataifa, mbali na Umoja wa Mataifa na ni matarajio yake kwamba jopo hilo litakuja na mapendekezo yanayolenga kuifanya dunia mahali bora zaidi pa kuishi.
Aliyasema hayo juzi wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa jopo hilo ofisini kwake katika Makao Makuu ya UN mjini New York, muda mfupi kabla ya wajumbe hao kufanya kikao chao cha kwanza chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete.
“Nawashukuru sana kwa kukubali uteuzi wangu. Dunia ina imani kubwa na uwezo wenu katika kutuwezesha sote kukabiliana kwa kujiamini zaidi na magonjwa ya milipuko katika siku zijazo,” Ki Moon aliwaambia wajumbe hao sita ambao wamepewa hadi Desemba mwaka huu kuwasilisha Ripoti kuhusu namna gani dunia inavyoweza kukabiliana vizuri zaidi na magonjwa ya milipuko.
Mbali na Rais Kikwete ,ambaye ni Mwenyekiti wa Jopo hilo, wajumbe wengine ni Celso Amorim wa Brazil, Micheline Calmy-Rey wa Uswisi, Marty Natalegwa wa Indonesia, Joy Phumaphi wa Botswana na Rajiv Shah wa Marekani.
Rais Kikwete amemshukuru Ki -moon kwa uteuzi wa jopo hilo akisisitiza kuwa uteuzi huo unaonyesha ni kiasi gani UN ina imani katika uwezo wa wajumbe wa Jopo kuifanya kazi hiyo vizuri.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!