INGAWA kuna baadhi ya wataalamu wa afya, hususan wale wa tiba mbadala, wanashauri wananchi waache ama kupunguza kula nyama nyekundu, lakini Bodi ya Nyama Tanzania inashauri Watanzania waongeze kula nyama.
Kwa mujibu wa bodi hiyo, takwimu zilizopo zinaonesha kwamba Mtanzania hula wastani wa kilo 12 tu za nyama kwa mwaka wakati kiwango kinachotakiwa kwa mujibu wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) ni wastani wa kilo 50. Kwa bara la Afrika nchi ya Botswana inatajwa kuwa na kiwango kizuri cha ulaji wa nyama kwa mtu kwa mwaka, kwani imefikia kilo 36.
Wale wanaokataza ulaji wa nyama, hususan nyama nyekundu, wanadai kwamba inasababisha magonjwa kama shinikizo la damu kutokana na lehemu (cholesterol) na kusababisha damu kuwa na kiwango kilichozidi kemikali iitwayo uric acid. Lakini Bodi ya Nyama wakati wa maonesho ya Nanenane mwaka jana ilikuwa inahimiza wananchi kula nyama kwa wingi ili kujenga miili yao inayohitaji protini ya kutosha ambayo inapatikana katika nyama.
Hapa nchini nyama huliwa kama kitoweo kwa kutumia vyakula mbalimbali ikiwemo ugali, chipsi na wali. Wengine nyama huichanganya katika baadhi ya vyakula kama vile ndizi. Nyama pia huchomwa kwa kutumia majiko ya kuni, mkaa au kwa yale yanayotumia umeme. Nyama pia huchemshwa na kuliwa kama supu.
Kama ilivyodokezwa hapo juu, nyama inahitajika kiafya katika mwili wa binadamu kwa sababu, mbali na protini, pia ina madini ya chuma ambayo ni muhimu kwa wanawake wanaotarajia kujifungua watoto. Wataalamu pia wanasema nyama ina vitamini B12 ambayo husaidia katika utengenezaji wa vinasaba (DNA) kwa ajili ya kujenga mishipa na seli za damu.
Nyama pia ina madini ya zinki ambayo huiwezesha kinga ya mwili kufanya kazi na kikubwa, kama ilivyokwishadokezwa hapo juu, ina protini ambayo ni muhimu kwa ajili ya ujenzi wa mifupa na misuli kwenye mwili wa binadamu. Wakati nyama nyekundu inazalishwa kutokana na wanyama kama ng’ombe, mbuzi, kondoo, nyati, pundamilia, swala na wengine wengi, nyama nyeupe ni ile tunayopata kutokana na wanyama jamii ya ndege kama kuku na bata au samaki.
Licha ya umuhimu wake kwa ujenzi wa mwili kutokana na wingi wa protini, na licha ya makatazo ya matabibu wa tiba mbadala, yapo baadhi ya makabila hayali nyama kutokana na imani zao za kimila na kiitikadi. Hata hivyo, madhara yanayofahamika kutokana na nyama ni kuila ikiwa haijachemshwa au kupikwa kama si kuchomwa kwa kiwango kinachotakiwa.
Nyama pia baada ya kuchinjwa inatakiwa ikaguliwe na maofisa wa afya ili kuona kama haina magonjwa ambayo yanaweza kuwaambukiza walaji na hasa kama haitachemshwa vya kutosha. Nyama choma ndizo zinazoaminika kutoiva kwa kiwango kinachotakiwa na hivyo wapenzi wa nyama hiyo kila mara wanakumbushwa kuwa makini.
Mbali na faida za kiafya, nyama pia ni muhimu kwa maendeleo ya nchi kutokana na mazao yake kuokoa fedha nyingi za kigeni ambazo zingetumika kuagiza mazao hayo kutoka nje ya nchi. Makala haya yanajielekeza katika kuangalia hali ya ulaji nyama, hasa katika kumbi za starehe, baa na katika migahawa na mwandishi amefanya uchunguzi wake zaidi katika jiji la Mwanza.
Wakati tatizo la kiafya linaweza kuanzia kwenye machinjio zetu ambazo nyingi hazikidhi vigezo vya kimataifa, mwandishi pia amegundua kwa chakula hicho, katika baadhi ya maeneo (mabaa na migahawa) huandaliwa katika mazingira ambayo yanatishia afya za walaji.
Uchomaji wa nyama Nyama imekuwa ikichomwa katika mazingira machafu katika baadhi ya baa na kumbi za starehe hususan za mitaani lakini hakuna anayejali.
Baadhi ya wachomaji wa nyama hawaogi na wanavaa mavazi ambayo sio nadhifu. Wakati wakiwa katika shughuli hiyo ya kuchoma nyama wanaweza kushika nyama na kisha kushika chochote kama vile kupokea fedha na kurudisha chenji kutoka kwa walaji na kisha kushika nyama bila kunawa kwanza.
Ikumbukwe kwamba fedha nyingi huwa chafu zikiwa zimepitia kwenye mikono mbalimbali ya watu. Katika moja ya ukumbi wa starehe wa mtaani ambao mwandishi alitembelea, aliona mchoma nyama akienda kujisaidia kwenye choo kichafu cha ukumbi huo lakini aliporejea hakuhangaika hata kunawa mikono kwa sabuni, akaendelea na kushika nyama kwa ajili ya kuwahudumia wateja kama kawaida.
Bodi ya Nyama, wakati wa maonesho ya Nanenane mwaka jana ilikuwa inaelekeza kwamba, hata kwenye bucha (na kama ilivyo katika eneo la kuchomea nyama) inatakiwa wawepo watu wawili; mkata nyama ama mchomaji maalumu na yule anayepokea fedha na kurudisha chenji.
Kwa mantiki hiyo, ni kosa kwa mtu anayechoma nyama au kuuza nyama katika bucha, awe tena ndiye huyo huyo anayepokea fedha kutoka kwa wateja.
Akilazimika kufanya hivyo basi anatakiwa anawe mikono kwa maji ya moto ama hata kwa sabuni barabara na kuendelea kuhudumia wateja, jambo ambalo ni nadra kuliona. Katika uchunguzi wake, mwandishi pia aligundua kwamba baadhi ya meza au miti ambayo hutumiwa kukatia nyama mara nyingi huwa ni michafu na hazisafishwi vya kutosha.
Kwa mujibu wa Bodi ya Nyama, hata kwenye mabucha, miti ambayo ndio mabucha mengi mitaani huitumia kwa kukatia nyama haikubaliki, kwani licha ya baadhi yao kuwa na uwezekano wa kuzalisha sumu, inatunza rundo la bakteria kwa kuwa huachwa ikiwa michafu siku nenda siku rudi.
Katika baa moja jijini Mwanza, mwandishi alimuona mchoma nyama akikata nyama akiwa kifua wazi na huku akitokwa na jasho kwapani. Hata hivyo, mteja mmoja aliyekuwa akihudumiwa nyama hiyo, alionekana mwelewa kutokana na wajihi wake lakini hakuhoji wala kukereka na hali hiyo!
Mtaalamu mmoja wa afya jijini Mwanza anasema kuwa mtu anayependelea kula nyama lazima awe makini na aina ya nyama anayokula kwa kuzingatia uandaaji wake unakuwa mzuri, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa imeiva vizuri ili kuepuka uwezekano wa kupata magonjwa yatokanayo na ulaji wa nyama.
Uchemshaji wa supu Katika eneo la uchemshaji wa supu, hasa katika mabaa na migahawa ya mtaani ambako ndiko watu wengi huenda, mwandishi aliona kukiwa na afadhali kidogo kulinganisha na maeneo ya uchomaji nyama. Hata hivyo, bado uvaaji wa wapika supu na unadhifu wao hakuonekana kama ni wenye kuridhisha.
Kimsingi, maofisa wa afya sambamba na Bodi ya Nyama wanapaswa kuongeza elimu ya watendaji wa biashara ya nyama na kuwabana ipasavyo wale wanaokiuka taratibu. Lakini walaji wa nyama ni lazima pia tukatae kula nyama inayoandaliwa katika mazingira machafu. Mtu anaweza kusema hajui kinachotokea katika maneo ya machinjio lakini inakuwaje unashindwa hata kukemea na kukereka kwa mchoma nyuma anayekuhudumia kuwa mchafu?
Maandalizi yanavyotishia afya ya walaji nyama Na Danny Kadadi “MIMI napenda sana kula chapati. Niliona kero kwenda kununua ngano kwa wenzangu kila mara hivyo nikaamua nilime mwenyewe ngano ili nijipatie unga wa kutengeneza chapati,” anasema Anjela Marco alipokuwa anazungumza na mwandishi wa makala haya.
Anjela anasema awali alikuwa analima mazao ya mahindi, maharage, mbaazi kwa ajili ya chakula, yaani kilimo cha kujikimu lakini ulimaji wa ngano ndio ‘uliomtoa’ na ambao asili yake ni kutaka tu kupata unga wa chakula anachopenda, chapati. Anasema alianza rasmi kilimo hicho cha ngano mwaka 2010.
Anasema awali kilimo chake kilikuwa mazoea kwa maana ya kutofuata kanuni bora za kilimo cha mazao mbalimbali kama inavyoshauriwa na wataalamu wa kilimo na hivyo kipato chake kilikuwa ni kidogo.
Anjela Marco ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kambi ya Simba kilichopo kata ya Mbulumbulu, Tarafa ya Mbulumbulu wilaya ya Karatu anasema mwaka 2012, chini ya Mpango wa Kuongeza Tija ya Uzalishaji wa Mazao ya mpunga, ngano na muhogo (EAAPP) alichaguliwa kuhudhuria mafunzo ya kilimo bora cha zao la ngano katika Chuo cha Kilimo Uyole.
Anasema katika mafunzo hayo, alipata uelewa zaidi wa uzalishaji wa zao la ngano kama vile uandaaji mapema wa shamba la ngano kabla ya kupanda, matumizi ya mbegu bora kulingana na jiografia ya maeneo yake anayolima, matumizi sahihi ya viuatilifu vya kuua wadudu, kudhibiti magonjwa na magugu pamoja na matumizi sahihi ya mbolea kulingana na eneo analolima mtu.
Baada ya kupata mafunzo hayo msimu huo wa 2012 anasema alianza kulima ekari mbili za ngano kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo cha zao hilo na kipato cha uvunaji kikaongezeka kufikia gunia 10 kwa ekari wakati awali alikuwa akipata gunia sita kwa ekari hiyo hiyo.
Aidha kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo cha ngano kwa msimu wa 2014 ameweza kuzalisha ngano yenye ubora wa juu zaidi na kumpatia mauzo ya kihistoria ya bei ya Sh 1,000 kwa kilo akiuzia ngano yake hapo nyumbani kwake kijijini wakati wakulima wenzake huwalaziimu kupeleka ngano yao Arusha mjini umbali zaidi ya kilomita 150 na kuuza kwa bei ya Sh 725 kwa kilo.
Akizungumzia mafanikio aliyoyapata kutokana na kilimo hicho cha zao la ngano anasema ameweza kusomesha watoto wake kuanzia shule ya msingi hadi sekondari na kwenda ziara mbalimbali za mafunzo ya zao la ngano ambapo ameweza kujifunza utunzaji wa bustani wa miche mama ya matunda na migomba ambayo ameanza kuitekeleza hapo nyumbani kwake anapoishi.
Mafanikio mengine anasema ni kuendelea kujenga nyumba bora na ya kudumu, kununua mbuzi mmoja wa maziwa ambaye ameshazaa kitoto, pesa za mauzo ya ngano zimemsaidia matibabu mwanawe aliyepigwa baada ya kuvamiwa na majambazi na pia kumtibia mumewe aliyevunjika mbavu baada ya kudondoka.
Mafanikio mengine anasema ni kupata ufahamu wa matumizi mbalimbali ya ngano kama vile utengenezaji wa maandazi, keki, pilau, kande na matumizi ya dawa ya asili ya kutibu presha na kisukari. Mafanikio mengine anasema ni kusafiri safari za mafunzo ndani na nje ya nchi kama vile Mbeya na Ethiopia.
Kwa upande wa changamoto anazopambana nazo katika kilimo cha zao la ngano, Anjela anasema ni pamoja na usumbufu wa wanyama na ndege waharibifu na kwamba hii ni kutokana na mashamba yao kupakana na hifadhi ya Ngorongoro.
Pia anasena kuna changamoto ya viuatilifu kutokuwa na ufanisi mzuri wa kuangamiza wadudu waharibifu na kudhibiti magonjwa na ugumu wa upatikanaji wa mbegu bora za ngano zifaazo kulingana na jiografia yao na huwalazimu kuzifuata mbegu hizo Arusha mjini.
Changamoto nyingine ni uhaba wa mashine za kuvunia ngano (combine harvester) hivyo husababisha ngano nyingi kupotea shambani baada ya kuchelewa kuvunwa.
Pia anasma kuna tatizo la mabadiliko ya tabia nchi ambapo mvua hukosa mtawanyiko mzuri na hivyo huathiri mavuno yao, ukosefu wa soko la uhakika la zao la ngano, hali ambayo huwafanya wakati mwingine kujikuta wanauza kwa bei isiyowapatia mrejesho wa gharama zao za uzalishaji na ukosefu wa jembe kucha la kukatua tabaka gumu la ardhi ili kuruhusu mzunguko mzuri wa maji utakaosababisha ustawi mzuri wa zao la ngano.
Ughali wa pembejeo kama mbegu, mbolea na viuatilifu ambavyo kwa pamoja huongeza gharama za uzalishaji anasema ni changamoto nyingine katika kilimo hicho.
Mkulima hiyo anaiomba serikali iwaagize wakala wa mbegu wafungue matawi yao katika ngazi ya wilaya ili kuwapunguzia wakulima gharama za kufuatilia mbegu bora Arusha mjini. Pia anapendekeza zao la ngano lipewe kipaumbele kama yalivyo mazao mengine hapa nchini na pia elimu ya kina ya matumizi zaidi ya ngano itolewe kwa wakulima ili waeweze kujua manufaa yake.
“Ninachoweza kusema, kama isingekuwa upenzi wa chapati nisingejiingiza katika kilimo cha ngano ambacho kimenipa manufaa makubwa,” anasema Anjela Marco aliyezaliwa mwaka 1966 na ambaye ni mama wa familia ya mume, watoto wanne na mjukuu mmoja.
No comments:
Post a Comment