Thursday 2 April 2015

GESI ZAIDI YAGUNDULIKA MTWARA

Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana kuhusiana na kampuni ya Statoil kufanya ugunduzi wa nane wa gesi asilia katika bahari kuu ya Tanzania. Kulia ni Naibu Waziri wa Nishati, Charles Mwijage. (Picha na Mroki Mroki).

WIZARA ya Nishati na Madini iko kwenye mchakato wa kukamilisha uandaaji wa sheria tatu, zitakazowasilishwa bungeni wakati wowote, zenye lengo la kuweka uwazi katika maeneo yote yanayohusu mikataba ya uchimbaji wa madini na gesi.


Aidha, wizara hiyo imetangaza kugunduliwa kwa gesi asilia ya futi za ujazo trilioni 1.0 hadi 1.8 katika kisima cha Mdalasini 1 mkoani Mtwara. Ugunduzi huo unaongeza kiwango cha gesi asilia iliyopatikana kwenye kitalu namba mbili na kufikia futi za ujazo trilioni 22.
Unafanya gesi asilia iliyopatikana nchini hadi sasa kufikia futi za ujazo trilioni 55.08.
Akizungumza mjini hapa, Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alitaja sheria zinazofanyiwa kazi kwa sasa ni ya uchimbaji, usambazaji na utafutaji.
Sheria nyingine ni ya Uwazi na Uwajibikaji katika masuala ya madini na inayofanyiwa marekebisho ni Sheria ya Petroli ya mwaka 1984. Alisema sheria hizo zote zina lengo la kuhakikisha kila kitu kuhusu madini kuanzia uchimbaji, utafutaji wake na mikataba kinakuwa wazi, tofauti na ilivyo sasa ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Petroli mikataba yote ni ya siri.
“Najua watu wamekuwa wakipigia kelele uwazi wa mikataba, sasa hili tunataka tulifanyie marekebisho ya kisheria, kwa kuwa mimi kama waziri nimefungwa mikono siwezi kuweka hadharani kutokana na sheria kukataza hilo, nikiiweka wazi kampuni hizi zina uwezo wa kunishitaki na nitalipa mamilioni ya fedha,” alisema Simbachawene.
Alisema ili kuendana na wakati na kasi ya ugunduzi wa gesi asilia nchini na nchi nyingine za jirani, ikiwa ni pamoja na ushindani wa soko la gesi, wizara hiyo inataka kuomba Bunge lifanyie kazi haraka sheria hizo, ikiwezekana kabla ya Bunge la bajeti.
“Wenzetu Msumbiji wamegundua gesi nyingi kuliko sisi, sasa tukiendelea kusuasua na jambo hili la sheria kwa mwaka mmoja pekee, tutaachwa sana nyuma, tunataka suala hili liishe muda si mrefu,” alisisitiza.
Hata hivyo, Simbachawene alisema si kweli kwamba mikataba iliyopo ilikuwa na usiri mkubwa, kama ilivyodhaniwa kwani mingi, ilikuwa ikiwasilishwa kwenye Kamati za Bunge na kupitiwa na wabunge.
Ugunduzi mpya
Akizungumzia ugunduzi mpya wa gesi asilia, waziri huyo alisema kisima kilichogunduliwa gesi hiyo cha Mdalasini 1, kimechimbwa katika urefu wa meta za maji ya bahari 2,296 Kusini mwa Kitalu namba mbili chenye miamba yenye umri miaka 66 hadi 145.
Alisema ugunduzi huo wa gesi, ulithibitishwa na Rais wa kampuni ya Statoil, Nick Maden ambaye kampuni yake ndiyo inafanya uchimbaji huo na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Alisema kuanzia mwanzo wa uchimbaji Februari mwaka 2012, kampuni hiyo ilichimba visima 13 na kugundua gesi katika visima vine, ikiwamo Mdalasini 1.
Aidha, Simbachawene alisema pamoja na mafanikio hayo ya ugunduzi wa gesi, bado uwekezaji zaidi unahitajika katika mitambo ya kuchakata na kusafirishia gesi hiyo, ambayo itajengwa katika maeneo ya nchi kavu.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!