Thursday 2 April 2015

MAUAJI DHIDI YA POLISI WETU YATAFUTIWE DAWA

Katika toleo letu la jana ukurasa wa mbele, kuna habari ya kusikitisha inayoelezea askari wawili kuuawa baada ya majambazi kuwavamia wakati wakiwa kazini kwenye eneo la Kipara Mpakani, kijiji kinachozigawa Wilaya za Temeke jijini Dar es Salaam na Mkuranga mkoani Pwani.


Katika habari hii, imeelezwa kuwa watu zaidi ya wawili wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, wakiwa na mapanga na bunduki, waliwavamia polisi watatu waliokuwa kwenye eneo hilo na kuwaua wawili, kumjeruhi mmoja kwa kumpiga risasi na kisha kupora bunduki kabla ya kukimbilia katika pori lililopo jirani na maeneo hayo.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, tukio hilo lilitokea majira ya saa 2:00 usiku na wahalifu hao bado wanasakwa. NIPASHE tunatoa pole kwa familia za askari hao. 
Hakika, tukio hili limeacha huzuni kubwa. Ni muendelezo wa aina ya matukio ambayo sasa yamekuwa yakijirudia mara kwa mara. Sasa ni wakati mwafaka wa kuangalia ni kwa namna gani matendo haya ya kinyama dhidi ya askari wetu yanakoma mara moja.
Inakumbukwa kuwa kabla ya tukio hili la kijiji cha mpakani mwa wilaya za Temeke na Mkuranga juzi, yapo pia matukio mengine kadhaa yenye kuhusisha uvamizi wa majambazi kwa polisi, kuwaua, kuwajeruhi na kuwapora silaha za aina mbalimbali. 
Kwa mfano, katika tukio lililotokea Juni 11 mwaka jana, watu wasiojulikana walivamia Kituo Kidogo cha Polisi Mkamba kilichoko katika Wilaya ya Mkuranga na kuua askari polisi mmoja na mgambo huku polisi mwingine akijeruhiwa vibaya. Katika tukio hilo, majambazi walifanikiwa kupora bunduki mbili aina ya SMG, tatu aina ya shotgun na magazini 30.
Septemba mwaka jana, majambazi yalivamia tena Kituo Kikuu cha Polisi kilichoko katika Wilaya ya Bukombe mkoani Geita na kuwaua askari wawili na kujeruhi wengine watatu. Walipora bunduki 10 aina ya SMG, risasi ambazo idadi yake haikutambulika na pia mabomu ya kutupa kwa mkono.
Januari 26 mwaka huu, majambazi yalitumia silaha za jadi kuwavamia polisi wawili waliokuwa doria katika mitaa ya jiji la Tanga na kuwapora bunduki mbili zilizokuwa na risasi kadhaa. Katika tukio hilo, askari mmojawapo alijeruhiwa vibaya na kulazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Bombo. 
Ni wazi kwamba hali hii inawapa hofu wananchi, hasa pale wanapoona kuwa wale waliokabidhiwa dhamana ya kuwalinda wao na mali zao wakivamiwa na kuuawa kinyama na  kuporwa silaha za moto ambazo bila shaka, ndizo hurudishwa tena uraiani na kutumika kwenye matukio mengine ya uhalifu. 
Mathalan, hadi sasa hakuna taarifa ya kupatikana kwa silaha zilizoporwa na wahalifu baada ya kuvamia Kituo cha Polisi Ikwiriri na kufanya mauaji. Sisi tunasema, kwamba ifike wakati polisi nao wadhamirie kwa dhati kabisa kuwa sasa ni mwisho kuvamiwa na kuporwa silaha walizokabidhiwa kwa kazi ya kujilinda wao wenyewe na kuwalinda raia na mali zao. Ni habari mbaya kuona majambazi yakitamba na kufanya yatakavyo dhidi ya polisi wetu. Ni dharau na jeuri kubwa dhidi ya jeshi letu ambayo kwa namna yoyote ile, kamwe haipaswi kuachwa iendelee  kujirudia. 
Matukio ya aina hii yanaweza kuibua maswali kuwa je, hatma ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao ikoje ikiwa sasa polisi wetu wanavamiwa na majambazi, kuuawa na kisha kuporwa silaha? Je, kama Polisi wanafanyiwa unyama huu, raia wasio na silaha wala mafunzo ya kukabiliana na wahalifu watakuwa katika hali gani?
Inatarajiwa kuwa majambazi yawaogope polisi na vituo vya polisi. Yatambue kwamba yakithubutu kuwakaribia polisi wetu kwa nia ya kufanya uhalifu, kamwe hayatatoka salama. Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi kujipanga vilivyo kwa zana za kisasa na mbinu mpya za kukabiliana na matukio ya aina hii. Wananchi wanapaswa pia kutoa ushirikiano wa kutosha kwa jeshi letu ili kufanikisha operesheni za kuwanasa wahalifu. Ikumbukwe kuwa mafanikio ya polisi katika kutekeleza majukumu yao ndiyo kushamiri kwa usalama wa raia na mali zao. 
Shime, tuseme yatosha kwa vitendo hivi vya uporaji wa silaha na mauaji dhidi ya polisi.    
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!