Friday, 20 March 2015

ZITTO KUUTEMA RASMI UBUNGE


MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto anatarajia kuaga wabunge wenzake na kubainisha mbele ya Bunge hilo, kuwa anaachia rasmi madaraka yake ya ubunge baada ya kuhitilafiana na Chama chake cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).



Akitoa maelezo yake binafsi kwa gazeti hili bungeni mjini Dodoma jana, mbunge huyo alisema kwa muda mrefu kumekuwa na msuguano wa kiuongozi kati yake na viongozi ndani ya Chadema, uliosababishwa na tofauti za kimtazamo juu ya tafsiri pana ya demokrasia ndani ya chama hicho.
Alisema hatimaye tofauti hizo, zilisababisha Novemba mwaka 2013 Kamati Kuu ya Chadema kumvua nafasi zake zote za uongozi.
“Sikuridhika na maamuzi hayo na hivyo nikaonyesha kusudio la kukata rufaa katika Baraza Kuu la chama chetu, kama taratibu za kikatiba za chama chetu zinavyotaka.Bahati mbaya ofisi ya Katibu Mkuu haikunipa fursa hiyo, na huo ndio ukawa msingi wa mimi kufungua kesi mahakamani kuweka pingamizi dhidi ya kamati hiyo,” alisema.
Aliongeza kuwa, yaliyotokea baada ya hapo ni historia, lakini hatimaye Mahakama Kuu ilitoa hukumu yake Machi mwaka huu na katika hukumu hiyo alishindwa, kutokana na sababu za kiufundi kwa maelezo kwamba pingamizi lake liliwasilishwa kimakosa.
Alisema katika hali ya kawaida, kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho, ilitarajiwa kwamba baada ya maamuzi ya Mahakama Kuu, Kamati Kuu ingekaa na kumpatia rasmi mbunge huyo mashitaka yake yanayohusu uanachama wake na kuitwa kujieleza na ndipo itoe uamuzi.
“Hata hivyo, mara baada ya hukumu ya Mahakama Kuu, dunia nzima ilitangaziwa na Mwanasheria wetu Mkuu, kwa niaba ya chama, kwamba mimi nimeshafukuzwa na sio mwanachama tena wa Chadema,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa; “Baada ya hapo viongozi wa chama changu pia walitoa matamko mbalimbali yote yakionesha kwamba sitakiwi tena katika chama hiki, pamoja na kwamba hadi ninapoongea hapa leo, sijawahi kukabidhiwa barua yoyote inayonitaarifu kufukuzwa kwangu katika chama,” alisema Zitto.
Alisema kutokana na hali hiyo, ni wazi kwamba uanachama wake wa kisiasa ndani ya Chadema, umeshaondolewa.
Alisema japokuwa ana uwezo wa kuendelea kupigania uanachama wake kisheria, lakini kwa kuwa ni mwanasiasa na hakushinda kesi mahakamani, ikiwa ni pamoja na ukweli kuwa alichaguliwa na wananchi wa Kigoma Kaskazini, anatambua kuwa hawezi kuwa mbunge bila udhamini wa chama cha siasa.
“Huu ndio utaratibu wa kisheria tuliojiwekea. Kwa mujibu wa viongozi wangu katika chama ni kwamba udhamini wa chama changu umekwishaondolewa,” alisema.
Alisema kutokana na hali ilivyo, hana mpango wa kupigania uanachama wake wa Chadema katika viunga vya Mahakama na hivyo alitangaza rasmi kuwa taratibu za kikatiba zitakapokamilika tu, ataachia rasmi uanachama wake ndani ya chama hicho.
“Chadema ni chama nilichokipenda sana kwa sababu ya kuendelea kukua kwa tofauti za kiitikadi, kimtazamo na hata kibinafsi kati yangu na viongozi katika chama changu, nimeona kuendelea kupigania uanachama kisheria ni kutatiza na kukwaza harakati za mabadiliko hapa nchini katika wakati ambapo mfumo wa kisiasa unatambua uwepo wa vyama vingi vya siasa,” alisema.
Alisema kwa kuwa taratibu hizo hajui zitakamilika lini, alitumia fursa hiyo kuwaaga rasmi wabunge wenzake, Watanzania na wananchi wa jimbo lake la Kigoma Kaskazini alilolitumikia kwa miaka kumi kuanzia mwaka 2005 akiwa kijana mdogo wa miaka 29 tu.
Alisema vyama vya siasa ni jukwaa muhimu katika ujenzi wa demokrasia, lakini havipaswi kamwe kuwa juu ya wananchi.
Alisema kutokana na ukweli huo, wakati umefika sasa kukomesha udola na ufalme wa vyama vya siasa nchini, mfumo aliodai kuwa unavipa vyama vya siasa mamlaka ya kisheria ya kukanyaga mamlaka ya wananchi, hivyo haupaswi kuendelea katika Karne ya 21 na katika nchi inayoendeshwa kwa misingi ya demokrasia ya kuheshimu wananchi.
“Mimi ninaondoka bungeni si kwa sababu wananchi wangu wa Kigoma Kaskazini walionichagua wametaka niondoke. Siondoki kwa sababu nimeshindwa kufanya kazi zangu za ubunge. Na kwa kweli siondoki kwa sababu wanachama wenzangu katika Chadema wametaka niondoke,” alisema.
Alisema anaondoka bungeni, kwa sababu mfumo uliopo wa kisheria, unavipa vyama vya siasa mamlaka juu ya wananchi na wapigakura.
Alisema anatarajia Bunge hilo, halitoruhusu mfumo huo kupora mamlaka ya wananchi uendelee, kwa kuwa lina uwezo wa kukomesha mfumo huo, unaotukuza nguvu ya chama, badala ya nguvu ya watu.
Aliwataka wananchi wanaomuunga mkono, wasisikitike kwa maamuzi yake hayo kwa kuwa bado anayo fursa ya kuwatumikia kupitia jukwaa lingine, atakaloamua katika siku chache zijazo, ambapo huenda akarejea tena bungeni.
Alisema katika kipindi cha miaka 10 alichotumikia bungeni, ana uhakika yote aliyoyafanya yalikuwa sahihi, ingawa yapo aliyoyakosea akiwa kama binadamu na hivyo aliwaomba radhi wote aliowakosea.
“Watanzania wote kwa yote ambayo sikuyafanya kwa usahihi. Mimi ni binadamu, kiumbe dhaifu, sijakamilika. Ni Mola peke yake aliyekamilika. Nawaomba radhi sana,” alisema.
Aliongeza kuwa, anajivunia kuwa sehemu ya Bunge la 10 chini ya Spika Anne Makinda kwani pamoja na kukuzwa kifikra, ameweza kuibua hoja mbalimbali zilizotikisa Bunge ikiwemo hoja ya Buzwagi na kusababisha nchi kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa uendeshaji wa sekta ya madini na hivyo kukuza mapato.
Alisema Bunge la 10 limejenga ‘Bunge lenye Nguvu’ katika mfumo wa Bajeti ya nchi na kupitia Bunge hilo imewekwa misingi ya kujenga mfumo madhubuti wa uwajibikaji nchini.
Zitto alitarajia kuwasilisha hoja hiyo bungeni jana, hata hivyo hakupewa nafasi ya kufanya hivyo na Spika wa Bunge, Anne Makinda. Alipohojiwa na gazeti hili baada ya bunge kuahirishwa jana usiku, alisema: “Spika amesema ratiba imebana leo (jana)”.

HABARI LEO

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!