Thursday 19 March 2015

JAMBAZI SUGU KUTOKA BURUNDI LANASWA KIGOMA



MKAZI wa nchini Burundi anayetuhumiwa kuwa jambazi sugu amekamatwa katika Kijiji cha Kibuye wilayani Kibondo mkoani Kigoma alikotorokea baada ya kufanya uhalifu nchini Burundi.



Inadaiwa baada ya uhalifu huo nchini humo alifanikiwa kutoroka licha ya kupigwa risasi katika mguu wake wa kushoto.

Ofisa Mtendaji wa kata hiyo mpya ya Kagezi, Stephen Apolinar alimtaja mtu huyo kuwa ni Hakengimana Ndoyebili (33), mkazi wa Kijiji cha Mlugondo Mkoa wa Lutana nchini Burundi.

Apolinar alisema kuwa, tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 5 asubuhi baada ya wananchi wa Burundi kutoa taarifa kwa uongozi wa Kijiji cha Kibuye juu ya kuonekana jambazi hilo likivuka mpaka na ndipo ukaundwa mtego kwa kushirikiana na viongozi wa Kijiji cha Kibuye. Mtego uliofanikisha kukamatwa kwa jambazi hilo.

Alisema, jambazi huyo alikuwa akitafutwa nchini Burundi kufuatia tukio alilolitekeleza la kumuua askari polisi wa nchini Burundi wakati wa majibizano ya risasi na baada ya kukamatwa amekutwa akiwa na fedha kiasi cha sh.700,000 zikiwa mchanganyiko fedha za Tanzania pamoja na za Burundi.

Apolinary alisema kuwa, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kibuye, Laurence Vitus, Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Felix Sabas pamoja na wanamgambo ndio waliomkamata jambazi huyo kisha kumkabidhi kwa uongozi wa Burundi na baadae taarifa zikapelekwa kwa Jeshi la Polisi Wilaya ya Kibondo.

Nao baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Kibuye wilayani Kibondo wakizungumza na gazeti hili walisema, tukio hilo lilizua hofu kwa wakazi wa maeneo hayo katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za pasaka na kwamba hali ya usalama wao huenda ikapungua kufuatia kujitokeza kwa matukio ya namna hiyo.

Hata hivyo, Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Stephen Apolinary amewahakikishia usalama wakazi wa kata hiyo na kusema kuwa licha ya Kata ya Kagezi kuwa jirani na mpaka wa Burundi, lakini usalama utaimarishwa ili kuhakikisha kuwa hakuna tukio lolote la ujambazi linaloweza kutokea katika kata hiyo

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!