Friday 20 March 2015

IMF yatoa ripoti bajeti ya 2014/15



SHIRIKA la Fedha la Kimataifa (IMF), limesema utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2014/2015 unakabiliwa na changamoto kubwa hivyo ni vigumu kutekelezeka. 


IMF imesema hali hiyo inatokana na ukusanyaji wa mapato yatokanayo na kodi na yasiyo ya kodi kuwa chini ya lengo kwa kiwango kikubwa, pamoja na ucheleweshwaji wa fedha za misaada na mikopo kutoka nje. Taarifa iliyotolewa na ujumbe wa IMF ambao ulikuwa nchini kwa ajili ya kufanya tathmini ya Mpango wa Ushauri wa Sera za Uchumi ilibainisha kuwa juhudi za haraka zinahitajika kuwianisha matumizi ya Serikali na mapato na kuimarisha udhibiti wa matumizi ili kuepuka malimbikizo ya madeni.

 “Malimbikizo ya madeni katika sekta ya umma yanahitaji kutafutiwa ufumbuzi haraka. Tatizo hili limekuwepo kwa muda na ulimbikizaji huu umekuwa mkubwa na unazidi kuongezeka hasa kwa watoa huduma wa ndani na mifuko ya hifadhi ya jamii. 

“Tatizo hili lipo pia kwenye Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa watoa huduma wake. Kwa sasa ni muhimu kwa Serikali kutekeleza hatua za kulipa malimbikizo ya madeni na kuzuia kujitokeza madeni mapya kwa vyanzo vya malimbikizo haya. “Ili sera ya mapato na matumizi ya Serikali iendelee kuaminika ni muhimu bajeti ya 2015/16 ikatengenezwa kwa kuzingatia makisio halisi ya mapato ya ndani, misaada na mikopo ya kibajeti. “Bajeti yenye uhalisia pamoja na nakisi ya wastani ni kigezo muhimu katika kuepuka malimbikizo mapya ya madeni na marekebisho makubwa ya matumizi wakati wa mapitio ya nusu mwaka, na pia kulinda uhimilivu wa deni la taifa,” ilisema taarifa hiyo ambayo nakala yake ilipatikana jijini Dar es Salaam jana. Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa majadiliano yataendelea wiki chache zijazo ili kufikia maelewano ya mwisho kuhusu mfumo wa sera za kiuchumi ambazo zitasaidia kukamilika kwa mapitio ya pili ya mpango wa PSI ambao unatarajiwa kujadiliwa katikati ya mwaka huu.

 Pia, taarifa hiyo imebainisha kuwa ujumbe huo umetambua juhudi za Serikali katika kushughulikia suala la IPTL jambo ambalo litawafanya wafadhili waendelee kutoa misaada na kuepusha uharibifu wa mazingira ya kufanyia biashara. Taarifa hiyo ilisema kuwa maendeleo ya ukuaji wa uchumi yameendelea kuwa mazuri huku ukuaji wa pato la taifa kwa mwaka 2014 ukiongezeka kwa zaidi ya asilimia 7 wakati mfumuko wa bei ukishuka chini ya lengo la asilimia 5. “Kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia hivi karibuni kutachochea ukuaji wa uchumi mwaka 2015 na kusaidia kuthibiti mfumuko wa bei.

 “Takwimu za pato la taifa zilizorekebishwa kwa kuzingatia takwimu zilizotokana na tafiti mpya za hivi karibuni zinaonesha kwamba uchumi wa Tanzania ni mkubwa zaidi kwa asilimia 30 kuliko ulivyodhaniwa hapo awali. “Thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani imeshuka kutokana na kuimarika kwa dola ya Marekani dhidi ya sarafu nyingine. Jambo hili linachangia kuongezeka kwa ushindani wa mauzo ya nje ya Tanzania na hivyo kuleta faida kwa wakulima na wauzaji wengine. “Wakati huohuo kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia hivi karibuni kumepunguza makali ya kushuka kwa thamani ya shilingi kwenye gharama za uagizaji bidhaa nje,” ilieleza taarifa. ''

Ufisadi Wakati huo huo, Serikali imepoteza sh. bilioni 250 katika kipindi cha miaka tisa kutokana na kashfa nne za ufisadi ambazo zimetikisa taifa. Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu mwenendo na hatua za kisheria kwa viongozi wa umma wanaokiuka maadili. “Katika kipindi kisichozidi miaka tisa kumeripotiwa kashfa kubwa nne ambazo kwa ujumla wake zimeisababishia taifa hasara ya zaidi ya sh. bilioni 250 ambapo kwa wastani inapoteza takriban asilimia 20 ya bajeti yake ya mwaka,” alisema Sungusia. 



Sungusia alizitaja kashfa hizo kuwa ni ununuzi wa rada iliyotumika kutoka Kampuni ya Bae Systems ya Uingereza, wizi wa mabilioni Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (Epa) kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mkataba usio na tija wa Kmpuni ya Richmond na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow. Alisema licha ya kuwepo vyombo vya kusimamia maadili ya viongozi wa umma hali inaendelea kuwa mbaya siku hadi siku kwani rushwa inaendelea kushamiri na matumizi mabaya ya rasilimali za umma. Sungusia alisema bado kauli za kejeli na dharau zimeendelea kutolewa na viongozi wanaotuhumiwa na mapendekezo yaliyowekwa katika rasimu ya pili ya katiba na Tume ya Kukusanya Maoni kuhusu maadili ya viongozi yametolewa.

 “Mwenendo wa kuweka pingamizi Mahakama Kuu kuzuia Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kufanya kazi yake kikatiba limeonesha mwanya na udhaifu wa sheria na vyombo vya kusimamia maadili ya viongozi,” alisema. Alisema Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inaundwa kikatiba ina kazi, nguvu na mipaka yake, hivyo haitakiwa kuingiliwa inapofanya kazi zake. Aliongeza kuwa kwa mapingamizi yaliyotolewa na kusababisha baraza lisiendee na kazi yake kama ilivyopangwa inaonesha wazi namna vyombo vya kusimamia maadili ya viongozi vinavyopuuzwa.

CHANZO:JAMBO LEO.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!