Monday, 1 December 2014

MAALIM SEIF ASHANGAZWA NA UMASKINI MIKOA YA KUSINI



Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, amesema anashangazwa sana na jinsi mikoa ya kusini  inavyokabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi kwa zaidi ya miaka 52 wakati mikoa hiyo imejaaliwa rasilimali nyingi.



Maalim Seif alitolea mfano kwa rasilimalimali za asili zilizopo katika mikoa ya Lindi na Mtwara ikiwamo bahari ambayo alisema inaweza kutoa ajira kwa vijana wa Mikoa hiyo.

Alisema vilevile kuna mazao ya korosho na ufuta ambayo alisema yana umuhimu mkubwa kutokana na kuwa ya biashara.

 Akizungumza na umati wa wananchi na wanachama wa CUF wa Kata ya Mchoteka, Wilaya ya Tunduru, Ruvuma, Maalim Seif alisema kuwa korosho inalimwa eneo kubwa la mikoa ya kusini, lakini bado haina soko la uhakika na kwamba zao hilo kwa sasa linaonekana kama vile halina faida yoyote katika uchumi wa taifa na wakulima, kutokana na serikali kutolijali.

Kuhusu gesi asilia, Maalim Seif alisema kuwa rasilimali hiyo muhimu kwa taifa imegeuka kuwa janga kwa wakazi wa mikoa ya kusini badala ya kuwa neema itayopunguza ukali wa maisha.

”Aisema: Ndugu  zangu mna rasilimali za kutosha, mna madini ya kutosha kama vile rubi, almasi na shaba, lakini hali zenu za maisha ndiyo hii mnayoiona. Mimi nimesafiri kwa gari kutoka Masasi mpaka hapa Tunduru kilomita 252, nimetumia saa nne. Tatizo la nchi yetu viongozi ni wa Chama Cha Mapinduzi, wameshindwa kuwa na sera nzuri za kilimo, wakulima hawatazamwi na hawana thamani.”

“Hakuna mkakati wa kuwahudumia wakulima hao. Lakini pia katika suala la matumizi ya rasilimali yetu na mali ya asili ya nchi yetu, pia hakuna sera ya makusudi ya kuwanufaisha Watanzania katika matumizi ya rasilima zetu, na badala yake rasilimali zetu zinawanufaisha zaidi wageni kuliko wenyeji,’ aliongeza Maalim Seif.

Alisema kuwa ikiwa CUF kitapata nafasi ya kuongoza taifa  kitabadilisha sera ya uwekezaji na kuanzisha sera itayokuwa na manufaa ya moja kwa moja na Mtanzania.

“CUF itaanzisha utaratibu wa makusanyo ya pamoja ya mapato yatokanayo na rasilimalimali ya asili kama vile madini, dhahabu, gesi, almasi, Tanzanite, shaba, chuma, makaa ya mawe, uranium na madini mengine na kupanga matumizi ya mapato hayo katika makundi manne,” alieleza.

Alisema robo ya mapato hayo yataingia kwenye mgawo wa moja kwa moja kwa kila Mtanzania na robo tatu itayobaki itaingia kwenye matumizi ya kujenga nchi.

”CUF inaamini kwamba iwapo Mtanzania atakuwa anapata mgawo wa moja kwa moja utaotokana na mapato ya mali asili, yeye ndiye atakayekuwa mlinzi wa kwanza atakayelinda rasilimali zetu,” alisema.

“Kwa hiyo wananchi nawaomba mtuunge mkono CUF ili tulete sera zitazoongeza uwajibikaji kwa viongozi wa Serikali na kuleta manufaa kwa wananchi,” alisema.

 

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!