Watu saba wamefariki dunia na wengine 14 kujeruhiwa vibaya baada ya gari walilokuwa wamepanda kuacha njia na kupinduka katika Kitongoji cha Kwatondoro, Kijiji cha Magundi, Tarafa ya Mbungu wilaya ya Korogwe, Tanga.
Majeruhi wa ajali hiyo wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe ya Magunga kwa wanaendelea na matibabu.
Ajali hiyo iliyohusisha gari lenye namba za usajili T783 BLM aina ya Mitsubishi Canter lililokuwa likitokea Kijiji cha Ambangulu Kata ya Vugiri wilaya ya Korogwe kuelekea Korogwe mjini.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga Frasser Kashai, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa ilitokea juzi jioni katika Kijiji cha Magundi, wilayani Korogwe .
Kamanda Kashai aliwataja marehemu hao kuwa ni Ali Juma(47), Kihiyo Rutha, Merina Kiteleko, Asha Mussa, Stella Charles(32), Mama Kivula, na Jane Mbajo, wote wakazi wa wilayani Korogwe.
Waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni Ester Akili, Amlima Mohamed, Zaituni Bakari, Amina Rajab, Veronica Dabiel, Marik Peter, John charles, Mariam Sadiki, Zai Zalika, Ngosha Bakari, Monica Charles, Veronika Kiondo, Zaina Hamis na Richard Moses na wamelazwa katika katika hospitali ya wilaya Korogwe.
Alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo bado hakijafahamika mara moja na kwamba Polisi inawashikiliwa dereva Ramadhan Omar (32), mkazi wa Korogwe na mmiliki wa gari hilo, Haji Hamza a.k Haji Mambo (47).
“Chanzo cha ajali bado hakijafahamika mara moja, lakini tunamshikilia dereva pamoja na mmiliki wa gari hilo mpaka hapo Polisi itakapokamilisha uchunguzi wa ajali hiyo ili sheria iweze kuchukua mkondo wake,” alisema Kashai.
Alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Magunga wilayani Korogwe.
Kamanda huyo wa Polisi alitoa onyo kali kwa madereva wa vyombo vya moto kufuata kanuni na sheria za usalama barabarani ili kupunguza ongezeko la ajali nchini.
Alhamisi iliyopita, watu 13 walipoteza maisha na wengine 20 kujeruhiwa vibaya katika ajali iliyotokea eneo la Mkanyageni wilaya ya Muheza, mkoani Tanga.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment