Vatican, Italia. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amefungisha ndoa 20 katika Kanisa la Mtakatifu Petro mjini Vatican, lakini baadhi ya wakosoaji walipaza sauti kupinga kutokana na muundo wa ndoa hizo.
Pamoja na kwamba Vatican inaichukulia ngono nje ya ndoa kuwa ni dhambi, lakini miongoni mwa maharusi hao wapya walikuwamo wawili ambapo bibi harusi tayari alikuwa na mtoto, na bwana harusi alikuwa na ndoa iliyobatilishwa na kanisa.
Kama hiyo haitoshi wengine wawili waliofungishwa ndoa hiyo walikuwa wakiishi pamoja kabla ya kuoana, jambo ambalo pia ni kinyume na desturi ya kanisa hilo.
Baadhi ya wakosoaji walisema kuwa pamoja na kitendo hicho kwenda kinyume na misingi ya kanisa, baadhi ya maharusi walikuwa wamevalia mavazi mafupi ambayo walidai ‘yanawakwaza’ waumini.
“ Hili jambo siyo haki kabisa kwa kuzingatia historia ya kanisa kwa vile wengine tayari wameshazaa watoto wengine wamekuwa wakiishi pamoja kwa muda mrefu. Tunavyoona Papa hajatilia maanani kabisa suala la kukemea dhambi maana baadhi ya wanandoa walikuwa wamevalia nguo fupi,” alisema mmoja wa watu hao.
Malalamiko hayo, hata hivyo, yamepuuzwa na Vatican iliyosema kuwa wapendanao hao ni watu kama walivyo waumini wengine. “Hivyo hawa walioana Jumapili ni wapendanao kama walivyo kwa wengine. Baadhi yao wameishi pamoja kwa muda mrefu na wengine tayari wana watoto,” ilisema taarifa iliyotolewa na Vatican.
Taarifa zaidi zinasema kuwa maharusi hao wapya walichaguliwa kwa ajili ya sherehe hiyo ya nadra kama sampuli halisi ya wapendao wa kisasa wa Kikatoliki, wenye historia tofauti za kijamii.
Tukio hilo lilikuwa mwendelezo wa malengo ya Papa Francis, raia wa Argentina, ya kufanya mageuzi ndani ya kanisa hilo lenye waumini bilioni 1.3.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment