KAMA kawaida ya safu hii ni kukuletea habari za wanamama ambao habari zao hazisikiki wala kuandikwa.
Nimekuwa nikiwaletea habari za mama mmoja mmoja na tutaendelea kufanya hivi, lakini leo imekuwa tofauti kidogo, nakuletea kikundi cha kinamama Tushikamane kutoka Wilaya mpya ya Mbogwe, Mkoa wa Geita.
Kikundi hiki kilianzishwa na wanawake wanaoishi na virusi vya ukimwi (VVU), kwa lengo la kuelimisha jamii kuhusu maambukizi ya VVU, kuelimisha jamii juu ya unyanyapaa na kunyanyapaliwa, kuikumbusha jamii kwamba mtu mwenye VVU ana haki ya kuoa na kuolewa na kupata mtoto asiye na maambukizi.
Pia kuelimisha jamii juu ya kuzuia maambukizi mapya, na la msingi kwao ni kuelimisha juu ya kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kuhamasisha watu kupima afya zao; maana bila kupima ni vigumu kujua mgonjwa na mzima, na vigumu kuwaanzishia dawa.
Nimeamua niandike juu ya wanawake hawa kwa pamoja, maana wote wanafanya kitu kinachofanana. Wote hawa wana sifa ya mwanamama, ambaye tunamwandika kwenye safu hii.
Pamoja na mambo mazuri ya kutetea na kuulinda uhai, wanayoyafanya wanawake hawa, wana sifa moja kubwa ya kushinda vita kubwa ya kujinyanyapaa wao wenyewe. Hatua hii ni kubwa na ni muhimu sana katika kupambana na ukimwi.
Mtu akijinyanyapaa mwenyewe, anapoteza maisha haraka sana. Mtu akijinyanyapaa mwenyewe, anaufanya ugonjwa wa ukimwi kuwa wa siri na matokeo yake hawezi kupata msaada kwa wakati.
Wanawake hawa wa Masumbwe, wameshinda mtihani huu na kuna haja ya kuwapongeza na kuwatolea mfano, ili watu wengine wajifunze na kuiga mfano wao.
Septemba 26, 2013, wakati wa kufungua jengo la kliniki ya huduma na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU huko Masumbwe, wanawake hawa walisimama mbele ya umati mkubwa uliokuwa umekusanyika siku hiyo na kutangaza mafanikio yao; kwamba miongoni mwao zaidi ya wanawake sita, ambao wana VVU wamefanikiwa kujifungua watoto wasiokuwa na virusi.
No comments:
Post a Comment