KWA sasa kilio kilichotanda nchini ni cha ukosefu wa ajira. Vijana wengi, hasa wanaomaliza elimu ya juu katika vyuo mbalimbali, wanalia na wanachokiita ukosefu wa ajira.
Wao wanataka wakimaliza masomo wakute ajira tele zikiwasubiri, hakuna anayejiuliza hizo ajira zinatoka wapi au nani mwenye jukumu la kuzitengeneza.
Kabla sijaenda mbali nihitimishe kwanza kwa kusema kwamba ajira ziko tele ila kinachokosekana ni uwezo ulio kwenye utashi wa kuzitambua hizo ajira, walio wengi wamezama kwenye mapokeo ya kwamba kila anayemaliza masomo anapaswa akute ajira inamsubiri kana kwamba ajira zinatengenezwa na Mungu.
Tatizo ninaloliona mimi ni la mfumo tulionao wa ufundishaji na uelimishaji katika nchi yetu, mfumo ambao ni wa kimapokeo usioenda na wakati.
Mfumo uliotumika kwa zaidi ya miaka 50 iliyopita ambapo nchi ingeweza kuzalisha vijana kama 100 au chini yake wenye shahada ya kwanza kwa mwaka, ukiendelezwa hadi leo ambapo nchi inaweza kuzalisha vijana kama 10,000 kwa mwaka wenye shahada ya kwanza.
Tatizo hilo la mfumo wa kimapokeo liko hivi; kijana anaandaliwa akashinde mtihani ili akapate cheti kitakachomwezesha kupata ajira.
Kwahiyo anacholazimika kukiwaza ni ajira anayoamini iko tayari. Matokeo yake anaweka bidii katika kukariri mambo atakayoulizwa kwenye mtihani, hahangaiki na uelewa wa mambo mengine nje ya hapo. Huo ni mfumo wa kimapokeo, kujaza fikira bila tafakuri.
Mfumo huo uliopitwa na wakati haumpi kijana nafasi ya kuwaza kwamba nchi iliyopata uhuru wake zaidi ya miaka 50 iliyopita haijaongezeka hata sentimeta moja zaidi ya kuongezeka tu idadi ya watu wake. Hakuna mwenye wazo la kwamba tulipata uhuru tukiwa watu karibu milioni 8 na sasa tunakaribia watu milioni 50.
Vijana wanataka yaliyotokea wakati watu wakiwa milioni 8 ndiyo yaendelee kutokea hata leo wakati tuko milioni 50!
Kinachowazwa ni mtu kumaliza masomo na kupata ajira iliyo tayari “ready made”. Ndani ya fikira bila tafakuri za aina hiyo nani asiyeona kuwa humo kuna tatizo?
Ni tatizo sababu vijana wanajifunza kukariri bila kuona ulazima wa kuelewa. Aliyeelewa hawezi kutaja ukosefu wa ajira kana kwamba ajira inapatikana kama mvua inayonyesha bila kujali idadi ya watu waliopo ardhini.
Katika uelewa ingebidi vijana wanaomaliza masomo, hususan wale wa elimu ya juu, waelewe ni ajira kiasi gani na za aina gani zinazoweza kupatikana kila mwaka nchini mwetu na idadi ya wahitimu ambao nchi inawazalisha kila mwaka kabla ya kulilalamikia suala hilo.
Pia ieleweke kwamba nafasi za ajira zinazoweza kupatikana kila mwaka haziwezi zikajirudia zilezile kwa mwaka unaofuatia kwa vile wanaozipata kwa mwaka uliotangulia ndio kwanza wanakuwa wameanza kuzizoea, hivyo haiwezekani kwamba watakuwa wamehitaji kustaafu kwa maana ya kuziacha wazi ili kuwapisha wengine.
Tukichukulia kwamba mtu anaweza akaajiriwa kwenye nafasi fulani kwa zaidi ya miaka 20, ni wangapi wenye fani kama ya kwake watakaolazimika kusubiri katika kipindi hicho?
Kwangu mimi siwezi kusema wanaolazimika kusubiri wanafanya hivyo kwa kutokana na ukosefu wa ajira, hapana, ila naulaumu mfumo kwa kuwanyima uwezo wa kutafakari na kubuni, ubunifu.
Utoaji wa elimu haupaswi kuishia kwenye karatasi ya mtu kusahihishwa akapata alama na baadaye kutunukiwa karatasi nyingine inayoitwa cheti, halafu akaanza mchakamchaka akikimbizana nacho eti anatafuta ajira.
Utoaji wa elimu unatakiwa uende sambamba na uwezeshaji wa mtu kuitafakari halihalisi na kubuni njia mbalimbali za kukabiriana nayo. Bila hivyo elimu itakuwa inakaririsha tu bila kuelewesha, kitu kinacholeta tatizo badala ya kuliondoa.
Sababu elimu ya juu inapaswa izalishe ajira badala ya kuitafuta au kuiomba. Lakini katika hali ya kuelimisha kwa njia ya kukaririsha bila kuelewesha, uwezekano wa mtu mwenye elimu ya juu kupata fikira za kumwajiri mtu mwingine utatoka wapi?
Ila wapo wasomi, japo ni mmoja mmoja, walioelimika katika maana halisi. Bwana Kashenshero Kamushoina ni mtu wa kutolea mfano.
Baada ya yeye kupata shahada ya uchumi kutoka chuo kikuu, alihangaika kwa muda akitafuta ajira ambayo kipato chake kisingefikia hata sh milioni moja kwa mwezi.
Akaamua kuachana nayo na kubuni njia ya kujiajiri mwenyewe. Wasomi wenzake wakaendelea kusaka vibarua wakimuona yeye kama mtu aliyepotea njia.
Kwa sasa anasema mbali na kipato chake, ambacho kwa utaalamu wake wa uchumi, kajipangia mshahara wa shilingi milioni 10 kwa mwezi, pia ameajiri watu 10 anaowalipa kila mmoja mshahara usiopungua shilingi laki 5 kwa mwezi.
Anasema kama utaalamu wake huo angeuuza mahali popote nchini, kwa maana ya kuajiriwa, hakuna mahali ambako angeweza kupata kipato hicho. Yeye kabuni na kutengeneza ajira badala ya kulialia kwamba hakuna ajira.
Kwa maneno ya utani anasema, “akatembya amaizi aibanga”, kwa maana ya kuyapandisha maji mlimani, tofauti na ilivyozoeleka ambapo maji hutoka mlimani na kutiririkia bondeni.
Fikiria tungekuwa na watu walau 5,000 hapa nchini walioelimika na kuwa wabunifu kama alivyo Kashenshero Kamushoina nani angekuwa anataja neno ukosefu wa ajira?
Lawama zangu kwa mamlaka husika ni kutobadili mfumo wa uelimishaji, mfumo unaoendelezwa ni wa kuwafundisha vijana kukariri badala ya kuelewa.
Vijana wanakariri kuanzia mambo ya darasani mpaka maisha ya uraiani. Utaratibu huo hauwezi kumpa mtu upenyo wa kuitafakari halihalisi.
Ni kwamba kila kijana anapokuwa chuoni akiwaangalia waliomtangulia kumaliza na kubahatika kupata ajira, naye anawaza kumaliza chuo ili baadaye apate ajira nzuri zaidi, ajenge nyumba kubwa na nzuri katika maeneo kama ya Mbezi Beach, Masaki na mengine kama hayo yaliyopo jijini Dar es Salaam, pamoja na kumiliki magari ya kifahari.
Hayo yote yanatokana na mawazo ya kukariri, yasiyo na aina yoyote ya ubunifu ndani yake. Hayo yasipofanikiwa kelele zinaanza kwamba hakuna ajira.
Kwa sasa hakuna kijana anayetafakari kwamba nchi inaweza ikawa na nafasi 30,000 za ajira zinazohitaji wasomi wenye shahada, lakini nchi ileile ikawa inazalisha wasomi wenye kiwango kilekile wasiopungua elfu 10 kwa mwaka na wakati huohuo nafasi zote zikiwa tayari zimejaa, ajira zitatoka wapi?
Sababu waliopaswa kutengeneza ajira zaidi ndio wanaotaka ajira zilizotengenezwa tayari! Kwa nini mfumo unaotumika kuwaelimisha vijana nchini unawaandaa kuwa vibarua, kwa maana ya kuajiriwa, badala ya kuwaandaa wawe wabunifu wa kutengeneza ajira? Uko ni kuwaandaa au kuwahadaa?
Hebu fikiria iwapo vijana wanaomaliza elimu ya juu kila mmoja angekuwa anapewa changamoto ya kubuni walau ajira 20 kwa kila mwaka tungekuwa na ajira kiasi gani hapa nchini? Si ajira zingekuwa zinawatafuta watu badala ya wao kuzitafuta? Je, huu wimbo wa taifa wa hakuna ajira ungekuwepo?
Lakini badala yake vijana wanaelekezwa kukariri maisha waliyoyakuta. Watu wenye elimu ya Chuo Kikuu wanapigana vikumbo na watu wenye elimu ya darasa la 7 kutafuta vibarua eti ni ajira! Sielewi ni nani wanamtegemea awe amewaandalia vibarua hivyo! Aliyetoka mbinguni?
Matokeo yake ukosefu wa elimu ya ubunifu unawafanya wahitimu wa shahada waishie kuajiriwa na watu waliomaliza darasa la saba.
Mtu mmoja aliyeniambia kaishia darasa la sita kwa sasa ni mkurugenzi wa kampuni iliyowaajiri watu wengi wenye elimu ya shahada! Yeye hakupata elimu ila akapata ubunifu, wao wakakosa ubunifu na kupata elimu. Kwahiyo waliopata elimu wakaishia kumuita “bosi” mtu aliyekosa elimu.
Kwahiyo tuseme kizuri ni kipi, elimu au ubunifu?
Mfano mwingine ni wa bilionea mkubwa duniani, Bill Gate. Mtu huyo angeng’ang’ania vibarua, akiwa anaulilia ukosefu wa ajira, mambo yote anayoyasimamia yaliyotokana na ubunifu wake na kuinufaisha sana dunia yangekuwepo?
La kuzingatia ni kwamba nchi zote zilizoendelea duniani zimeyafikia maendeleo hayo kwa kutegemea zaidi ubunifu. Sidhani kama kuna nchi yoyote iliyoendelea kwa kutegemea misaada kama tunayotamba nayo sisi Tanzania.
Maana yangu hapa ni kwamba misaada ni kama ajira, kutegemea kunufaika na vilivyo tayari. Kulilia ajira ni sawa na kulilia misaada.
Tuangalie hapa nchini, tunawaona watu kama Reginald Abraham Mengi, Mohammed Gulam Dewji, Rostam Abdulrasul Aziz, Said Salim Awadh Bakhresa na wengineo.
Mbali na watu hao kuwa na maisha yao binafsi yaliyo bora, pia wana mchango mkubwa katika pato la nchi, pamoja na kuzalisha ajira nyingi sana. Mtaji wao mkubwa katika mafanikio yao hayo ni ubunifu.
Je, watu hao wangetegemea elimu ili iwawezeshe kupata ajira hayo yote yanayotokana na ubunifu wao yangekuwepo? Ni mtu gani aliyefikia mafanikio kama waliyo nayo wao kwa kutegemea ajira tu? Kama kuna anayemjua anieleze.
Mwisho niseme, tuache kulilia ajira, tujikite kwenye ubunifu ndipo tutajikomboa sisi wenyewe pamoja na kuikomboa nchi yetu kiuchumi na kimaendeleo
VIA TZ-DAIMA
No comments:
Post a Comment