Pages

Friday, 25 July 2014

MKUU WA SHULE ILIYOONGOZA KITAIFA MATOKEO KIDATO CHA 6 AHAMA NYUMBA ILI WANAFUNZI WAPATE PA KULALA

SHULE ya Igowole, iliyoshika nafasi ya kwanza kitaifa katika matokeo ya Kidato cha Sita mwaka huu, inakabiliwa na matatizo mengi, ikiwemo ukosefu wa mabweni, kiasi cha Mkuu wa Shule kulazimika kuhama nyuma kuachia wanafunzi wapate pa kulala.


Mbali na ukosefu wa mabweni ya kuhimili idadi ya wanafunzi, matatizo mengine ya shule hiyo ni ukosefu wa maji, maktaba, vifaa vya kufundishia na kusomea, gari la shule na walimu hasa wa masomo ya Sayansi na Hisabati.

Mkuu wa shule hiyo ya serikali iliyoko katika Kijiji cha Igowole wilayani Mufindi, Andrew Kauta, ameachia nyumba kwa ajili ya sehemu ya wanafunzi wa kike 237 wanaojiunga na kidato cha tano shuleni hapo.

Hata hivyo, shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1988 na kidato cha tano na sita kuanza mwaka 2008, pamoja na matatizo hayo, imeongoza kitaifa katika matokeo ya kidato cha sita ya mwaka huu, yaliyotangazwa hivi karibuni.

Kati ya wanafunzi 30 waliohitimu Kidato cha Sita mwaka jana, 19 walipata daraja la kwanza, 10 daraja la pili na mmoja ndiye mwenye daraja la tatu.

Kitendo cha kuibuka na matokeo mazuri, licha ya kuwepo changamoto hizo, kimekuna wadau wengi akiwemo Mbunge wa Mufindi Kusini, Mendrad Kigola ambaye amesema mafanikio ya shule hiyo yanaonesha jinsi walimu na wanafunzi wake wasivyokatishwa tamaa.

Alisisitiza upo umuhimu mkubwa wa kupewa misaada wanayohitaji ili wafanye vizuri zaidi. Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkuu wa Shule alisema tangu kuanzishwa kwa shule hiyo, haijawahi kupokea wanafunzi wengi wa Kidato cha Tano kama ilivyotokea mwaka huu.

“Tangu elimu ya kidato cha tano na sita ianze kutolewa shuleni hapa mwaka 2008, tumekuwa tukipokea wastani wa wanafunzi 30 wa kidato cha tano kila mwaka,” alisema Mkuu huyo.

Alisema mwaka huu, shule hiyo imeletewa wanafunzi wa kike 237 wa Kidato cha Tano, watakaoungana na 30 walioingia kidato cha sita. Shule hiyo ina wanafunzi zaidi ya 900 kidato cha kwanza hadi cha sita.

Hata hivyo, mkuu huyo alisema shule ina bweni moja pekee lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi wasiozidi 86. Alisema bweni hilo lililojengwa tangu shule ilipoanzishwa, miaka 26 iliyopita, haliko katika hali nzuri.

Alisema wanafunzi takribani 30 wa Kidato cha Tano, watajibana katika nyumba hiyo huku wengine 36 wakipelekwa katika bweni hilo pekee. Wanaobaki watahifadhiwa katika madarasa matatu, yanayotumiwa na wanafunzi wa vidato vya chini.

Mwalimu wa Taaluma, Isiaka Chodota alisema kutokana na sehemu ya madarasa kutumika kama mabweni, shule inabakiwa na vyumba 19 vya madarasa.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu na Mbunge wa Mufindi Kusini, Mendrad Kigola waliahidi kuongeza kasi ya kushughulikia matatizo ya shule hiyo, waliyoieleza kwamba mafanikio yake yameutoa kimasomaso mkoa wa Iringa.

Akizungumzia siri ya mafanikio ya shule hiyo katika matokeo ya Kidato cha Sita, Mkuu wa Shule alisema mwaka 2010 walijiwekea mpango mahususi wa miaka mitano wa kuboresha elimu katika shule hiyo, ikiwa ni pamoja na kusisitiza matumizi ya Kiingereza.

Siri nyingine ya mafanikio ya shule hiyo ni kuipa kipaumbele nidhamu. Kwa mujibu wa mkuu wa shule, kila Ijumaa huhakikisha wanafunzi na walimu wanakumbushwa sheria, kanuni na miiko ya shule.
Chanzo: Habarileo

No comments:

Post a Comment