Friday, 6 June 2014

MBUNGE ATAKA WABAKAJI WAHUKUMIWE KUNYONGWA


MBUNGE wa Bunge la Tanzania kupitia chama cha CUF, Moza Abeid Saidy ameiomba serikali kuweka adhabu ya kifo kwa wabakaji ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo.
Alisema hayo katika swali lake la nyongeza bungeni mjini hapa jana, baada ya kutoridhika na majibu aliyopewa kwenye swali lake la msingi.


“Kwa nini serikali isitoe adhabu ya kifo kwa wabakaji ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia hizo?. Pia, serikali ina mpango gani wa kuweka muda maalum kwa kesi za ubakaji?” alihoji
Akijibu swali hilo la nyongeza, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angella Kairuki alisema kuwa serikali haina mpango wa kuongeza adhabu kwa wabakaji, kwani adhabu ya sasa ya kifungo cha miaka 30 jela inatosha.
Alisisitiza kuwa anakubaliana na mbunge huyo, kuwa ubakaji unaendelea kukua kwa kasi, lakini adhabu za sasa zinatosha kutoa fundisho kwa wahusika.
Aliwahimiza wote wenye tabia hiyo chafu, waache mara moja. Katika swali lake la msingi, Moza aliuliza “Je, ni kwa sababu gani hukumu ya makosa ya ubakaji, hutolewa tofauti, ambapo wengine huhukumiwa kifungo cha maisha, wakati wengine hufungwa kifungo cha miaka 15-50?”.
Akijibu swali hilo la msingi, Kairuki alisema kubaka ni kosa la jinai, ambalo linatendeka katika mazingira yaliyoelezwa chini ya Kifungu cha 130 (1) na (2) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura ya 16. Naibu Waziri alisema Adhabu ya kosa la kubaka imetamkwa wazi na Sheria ya Kanuni za Adhabu chini ya Kifungu cha 131 (1).
Adhabu ya kosa hili chini ya sheria hii ni kifungo cha miaka 30 au kifungo cha maisha pamoja na kuchapwa viboko na kulipa faini.
Alisema pamoja na adhabu inayotolewa chini ya Kifungu cha 131(1), Kifungu cha 131(3) kinabainisha kwamba endapo muathirika wa ubakaji ni mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 10, adhabu ya mbakaji atakapopatikana na hatia ni kifungo cha maisha.
Kairuki alisema kwa upande wa mkosaji mwenye umri wa miaka 18 au pungufu, Kifungu cha 131(2) kinaeleza kwamba adhabu yake itakuwa ni kuchapwa viboko.
Endapo kosa alilolitenda ni kosa la kwanza, kifungo cha miezi 12 na kuchapwa viboko kama ni kosa la pili. Na endapo atarudia kosa hilo kwa mara ya tatu na kuonekana ni mzoefu, atafungwa kifungo cha maisha.
Kwa mantiki hiyo, hakuna hukumu ya kifungo cha miaka 15 jela kwa makosa ya ubakaji

CHANZO: HABARI LEO

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!