Friday, 6 June 2014

HIKI NDIO CHAMA CHA URITHI KWA WANAWAKE WAJANE KENYA

Wanachama waliosalia katika chama cha kuwarithi wajane Kenya
Kuna vyama vya kisiasa na vya mambo mengine katika nchi mbalimbali, lakini Je umewahi kusikia chama cha wanaume kuwarithi wajane?
Basi hilo linapatikana katika kijiji cha Kakmasia huko Migori Magharibi mwa Kenya.
Paul Nabiswa alimtembelea mwenyekiti wa chama hicho mzee Peter Ogema Nyajwaya Oria ambaye ana miaka 71.
Mzee Peter Ogema Nyajwaya ni mmoja wa wazee wakakamavu katika umri wake, wala hajutii kuwarithi wanawake akisema kuwa alichukua mwelekeo huo kwa sababu alizaliwa katika familia ambayo ilikuwa inapenda suala la kurithi wanawake waume zao wanapofariki.
Na ili kuonyesha kuwa pengine anahalalisha mipango ya kurithi wajane, waliungana wanaume watano na kubuni chama kitakachojulikana kwa kurithi wanawake. Yeye anasema alichaguliwa kuwa mwenyekiti kwa sababu wenzake walimtambua kuwa mtu mwenye uwezo.
Wanachama hao walipokuwa watano walikuwa wakitembela katika mazishi na kucheza na mkuki na ngao wakipanga namna ya kuwarithi wajane waume zao wakifariki.
Mzee Peter Ogema Nyajwaya
Hata hivyo wamesalia wawili tu katika kundi hilo kwani wenzake watatu wamefariki na Ogema anadai kuwa walikufa vifo vya kawaida.
Japokuwa watu katika maeneo hayo ya magharibi mwa Kenya wamekashifu maazimio ya chama hicho Ogema anasema kuwa amefaulu kuwarithi zaidi ya wanawake kumi.
'Je anawatosheleza?'
''Wanawake niliorithi wamefika karibu kumi naweza kuwatosheleza wote kwa mapenzi, hufanyi mapenzi na wote kila siku unagawanya siku zako,'' alisema mzee Ogema.
Baadhi ya kanuni za chama hicho kulingana na Ogema ni kuwa wanawake wanaorithiwa wanasalia katika maboma yao na wanaume wanawatembelea huko.
Vivyo hivyo ikiwa amemrithi mwanamke na amesafiri mbali, wanaenda kupimwa virusi vya ukimwi kabla ya kuingiliana kimwili. Mbali na hayo anapigia debe matumizi ya mipira ya Condom akisema kuwa wazee kama yeye hawajaachwa nyuma kuitumia wanapolazimika kufanya hivyo.
'Zamani sana'
Ogema ambaye ana wanawake wawili kando na wale kumi aliorithi kwa sasa hakumbuki miaka aliorithi wanawake hao.
''Siwezi kukumbuka ni lini nilirithi hao wanawake kwa sababu kifo hutokea kwa wakati tofauti, mtu mmoja anaweza kufa leo mwingine baada ya mika mitatu na kadhalika.''
Mzee Ogema na wake zake pamoja na wanawe
Mke wake Mary Aluoch ambaaye amedumu naye katika ndoa kwa karibu miaka 50, anasema kuwa hana tatizo na mume kuwarithi wanawake wengine kwa sababu ni mila na hata yeye anaweza kurithiwa ikiwa mumewe atafariki sasa.
Jambo linalojitokeza katika mpango huu ni kuwa Ogema amemeathirika kwa sababu anawahudumia pia watoto zaidi ya kumi aliowazaa na wanawake aliowarithi.
''mimi nimezaa watoto wanne, na bibi mmoja watoto wanne na bibi mwingine, watoto wawili kwa mwingine mmoja kwa mwingine, na mmoja kwa mwingine. Mimi huwa nawafanyia kila kitu wakihitaji.''
Eneo la Migori na maeneo jirani ni kati ya sehemu zilizoathirika na kusambaa kwa ugonjwa wa ukimwi na ndoa za urithi huenda zikachangia hali kuwa mbaya ikiwa tahadhari hazitachukuliwa.
 BBC SWAHILI

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!