Sunday 8 June 2014

MADAKTARI WAZAWA JIFUNZENI UPASUAJI WA MATOBO"

‘Madaktari wazawa jifunzeni upasuaji wa matobo’
KUTOKANA na uhaba wa huduma za upasuaji kwa njia ya matobo nchini, madaktari wazawa 200 kutoka hospitali mbalimbali wameshauriwa kujifunza aina hiyo ya upasuaji inayopunguza gharama za wagonjwa wasio na kipato kwenda nje ya nchi kufuata huduma hiyo.

Hali hiyo inatokana na idadi kubwa ya wagonjwa kukimbizwa nje ya nchi kufuata upasuaji wa aina hiyo wakati wapo baadhi ya madaktari wenye uwezo wa kufanya huduma hizo, licha ya kukosekana kwa elimu ya kutosha kwa baadhi ya madaktari na wagonjwa juu ya njia hiyo ya upasuaji.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua semina ya upasuaji kwa njia ya matobo, uliofanyika kwa uwazi jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Kairuki, Dk. Muganyizi Kairuki, alisema anaamini zipo hospitali zitakazokubaliana na teknolojia hiyo na kuitumia.
Dk. Kairuki alitaja faida za upasuaji huo tofauti na ule wa kawaida ambao mtu hupasuliwa sehemu kubwa ya tumbo, ni mgonjwa kurudi nyumbani mara baada ya operesheni.
“Kutokana na umuhimu wa tiba hii kuhitajika nchini, tumeamua kushirikiana na baadhi ya madaktari kutoka India, China, Afrika Kusini, Namibia na Kenya ili kupeana uzoefu na mafunzo ya kufanya operesheni kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya matobo madogo.
“Badala ya kuchana eneo kubwa la mwili wa mgonjwa na kumlaza hospitalini, anafanyiwa upasuaji huu asubuhi, jioni anarudi nyumbani,” alisema Dk. Kairuki.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Donan Mmbando, katika hotuba yake iliyosomwa na kaimu wake, Dk. Edwin Mng’ong’o, alisema anaamini ujenzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba cha Muhimbili, utaongeza udahili kutoka wanafunzi 2,400 hadi 12,000 na kuchangia ongezeko la wataalamu wa upasuaji.

TZ-DAIMA

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!