Rais Jakaya Kikwete ameliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata wezi wa fedha za wakulima wa tumbaku mkoani Tabora kwa kuwafikisha mahakamani haraka iwezekanavyo.
Alitoa agizo hilo katika hotuba yake ya uzinduzi wa uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi kwenye Viwanja vya Chipukizi, Tabora mwishoni mwa wiki.
Baada ya kumaliza uzinduzi huo Rais Kikwete alisema haitakuwa vyema kama hatazungumzia mambo mengine yakiwamo maji, barabara na zao la tumbaku.
Alisema amewasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu na kumwagiza ndani ya siku mbili awe amepeleka Tabora kikosi cha uchunguzi kutoka makao makuu ya Polisi kupitia ripoti ya ukaguzi na uchunguzi kuhusiana na ubadhirifu wa fedha za wakulima wa tumbaku na kuchukua hatua.
Rais alisema Serikali imechoshwa na wezi wa fedha za wakulima wa tumbaku na kwamba safari hii hatakuwa na huruma kwa wale wote watakaobainika.
Mara kadhaa, Rais Kikwete amekuwa akilalamikia wizi wa fedha za umma. Julai mwaka jana, akizungumza na wananchi baada ya kufungua jengo la kitega uchumi la Chama cha Ushirika cha Mkoa wa Kagera (KCU), mjini Bukoba alisema baadhi ya vyama vya ushirika nchini vina mkusanyiko wa wezi wanaokula fedha za wananchi bila hata kunawa... “Hapa Kagera ni kitovu cha ushirika na KCU ni kitovu cha kuboresha na kuleta usasa katika shughuli za ushirika. Siyo kama vyama vingine ambavyo ni mkusanyiko wa wezi wanaokula waziwazi mchana bila hata aibu…. Wanakula bila kunawa.”
Akionekana kukerwa Rais Kikwete alisema anazo taarifa zote za wahusika kutamba wakijiita ‘wakubwa’ na hawataguswa na dola... “Mimi ndiye bosi wa nchi hii hakuna mwingine zaidi yangu… Hivyo ninaagiza wale wote watakaobainika na ubadhirifu na wizi wa fedha za wakulima wa tumbaku, wafikishwe mahakamani mara moja.”
Alisema hakuna mjadala na wezi kwani siku zote mwizi sehemu yake ni polisi ambao wakichunguza na kuthibitisha huchukua hatua kwa kuwafikisha mahakamani.
Alisema baada ya kuwasili mkoani Tabora, alifanya mazungumzo na viongozi wa mkoa na ameridhia wezi wote wafikishwe mahakamani haraka iwezekanavyo bila mjadala.
Mapema mwaka jana, Bodi ya Chama cha Kikuu cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (Wetcu) Ltd, ilijiuzulu kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa mabilioni ya shilingi za chama hicho.
Baada ya bodi hiyo kujiuzulu, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwassa aliteua bodi ya muda ambayo inayo inadaiwa kuwa haina maelewano na uongozi wa mkoa.
Msuguano baina ya uongozi wa mkoa na Wetcu unadaiwa pia kukolezwa wakati wa ujio wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana aliyefikia hatua ya kuangua kilio kutokana na dhuluma wanazofanyiwa wakulima na kushindwa kunufaika na kilimo cha tumbaku.
No comments:
Post a Comment