Monday 9 June 2014

SAA ZA MWISHO ZA MZEE SMALL, ALITAKA UPENDO KATIKA FAMILIA

 
Nguli wa michezo ya kuigiza na vichekesho, Saidi Wangamba ‘Mzee Small’ (59), amefariki dunia juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam akiwa ni msanii wanne kukutwa na mauti katika mwezi mmoja.
Kifo cha msanii huyo ambaye anatarajiwa kuzikwa katika Makaburi ya Segerea, Dar es Salaam leo kimetokana na ugonjwa wa kiharusi uliompata, mwaka 2012 alipoanguka bafuni na baadaye kupooza upande wa kushoto.
Mtoto wa marehemu, Muhidin Saidi alisema jana kwamba muda mfupi kabla ya kukutwa na mauti, baba yake alikuwa anakoroma huku akitapika damu mfululizo na ilipofika saa nne usiku alikata roho... “Sijawahi kumuona baba akiwa katika maumivu kama ilivyokuwa usiku kabla ya kifo.”
Hata hivyo, anasema wanafarijika kwani wiki moja kabla kifo chake, aliwaachia wasia akiwataka wanaosoma kushika elimu pia akisisitiza upendo miongoni mwao na matunzo kwa mke wake.
“Wanangu najua kuwa ninakufa, hilo halina mjadala na ninaomba mnizike jirani na ninapoishi ili marafiki zangu wasipate tabu kufika kwenye kaburi langu,” alisema Muhidini akimnukuu baba yake.
Alisema Mzee Small alikataa wazo la kuzikwa kwao Kilwa, Lindi au Kiparang’anda, Pwani ambako kuna shamba lake.
Saidi alisema baba yao aliwasisitizia wanaye ambao bado wanasoma waishike elimu kwa kuwa ndiyo ukombozi wao ingawa yeye hakupata elimu ya kutosha na kusisitiza mshikamano baina yao. Mzee Small ni msanii wa nne kufariki ndani ya mwezi mmoja, akiwa ametanguliwa na Rachel Haule, Adam Kuambiana na George Otieno ‘Tyson’.
Sababu za kifo
Msanii huyo alifariki dunia baada ya hali yake kubadilika ghafla juzi nyumbani kwake Tabata Kisiwani na kupelekwa hospitali.
Said alisema baba yake alilalamika kujisikia vibaya na kukohoa na kutapika damu na ndipo walipompeleka Muhimbili ambako alifanyiwa vipimo mbalimbali kikiwamo cha CT-Scan.
“Alikutwa na uvimbe katika maeneo matatu tofauti kichwani na ulionekana kama kuvia kwa damu katika ubongo na wakati akiendelea na matibabu saa mbili alikata kauli na alikuwa akiendelea kutapika damu,” alisema.
Alisema ingawa baba yao alikuwa amepooza upande wa kushoto kutokana na kiharusi, alikuwa anaendelea vizuri kabla ya kuzidiwa juzi
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!