Monday, 30 June 2014

HERI MASIKINI JASIRI KULIKO TAJIRI MUOGA"

USWAHIBA walionao watendaji wa serikali na wafanyabiashara wakubwa (matajiri) hapa nchini kinaweza kuwa kigezo kikubwa cha kudumaza maendeleo ya nchi na kukosa uwiano wa mapato kati ya walionacho na wale wasiokuwa nacho.

Hali hiyo imechangia kuwasukuma wafanyabiashara wengi waamue kujipendekeza ndani ya mfumo wa utawala wakiamini kuwa shughuli zao haziwezi kuharibika kwa kuwa wamebebwa kwa mbeleko za watendaji wa umma, na huko ndiko kunakowafanya waishi bila kubughudhiwa.
Kwa muda mrefu tabia na mienendo ya wafanyabiashara haiwiani kabisa na tabia waliyonayo wananchi wa kawaida ambao jitihada zao kubwa wanazozililia kila kukicha ni kutaka kujikomboa, lakini wanakandamizwa na hofu ya watawala wasiojali maslahi ya watu duni.
Wimbi la wafanyabiashara wengi kujikumbatia kwenye mbeleko za watawala kunatokana na hofu waliyonayo ili isije siku biashara zao zikaharibiwa na aina yoyote ile ya masuala ya kisiasa kwani kadiri upinzani unavyozidi kuwa mkubwa wao pia wanazidi kuongeza woga.
Kwa kutambua kuwa kuzaliwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa hakukuja kwa ajili ya kuwakandamiza watu masikini, hali hiyo inazidi kushamiri kwenye mifumo ya ukusanyaji mapato na ulipaji wa kodi unaofanywa na wafanyabiashara walioamua kujipendekeza kirahisi kwa watoza ushuru ili waonewe huruma.
Ikumbukwe kuwa kila Mtanzania ana haki yake ya kuishi, kufanya kazi zake halali bila kubughudhiwa na kujipatia kipato chake kwa muda na wakati anaoona kuwa unafaa.
Wapo wafanyabiashara wazalendo, wenye asili ya Kiafrika, Waasia, Waarabu, Wasomali na Wazungu ambao kwa wingi wao wameipenda Tanzania na wamekubali kwa hiari yao kuwekeza katika masuala ya uchumi.
Katika makundi hayo wapo walipa kodi wazuri na wapo wakwepa kodi wazuri, na hao wote wanafanya hivyo kwa kisingizio kuwa wapo wanaojitahidi kujipendekeza kwa viongozi wa serikali wakati sio waaminifu.
Kwa kuwa serikali na chama tawala wameanzisha mfumo wa kuwakumbatia wafanyabiashara, nao kwa upande wao wamejenga tabia ya kisingizio kuwa wanashindwa kulipa kodi vizuri kutokana na maombi mengi ya michango inayokusanywa na wanasiasa kutoka kwenye faida zao.
Wapo wanaodiriki kuonyesha michanganuo ya mwaka mzima wakidaiwa michango mbalimbali ya kukijenga chama tawala kwa masharti kuwa bila kufanya hivyo biashara zao zitakufa.
Tabia hiyo ni mbaya na msingi wake umewafanya wafanyabiashara wakubwa ama wengine waendelee kukwepa kulipa kodi na wengine wanaamua kuhamisha biashara zao na kuzipeleka nchi jirani ili wakwepe adha ya kuombwa michango mara kwa mara.
Katika makundi niliyoyataja na uasili wake, wapo Waafrika jasiri, Wahindi, Wazungu, Wasomali, Waarabu na wengine ambao kwa kutambua kuwa wametimiza masharti yote ya kulipa kodi, hawakiogopi chama chochote cha siasa.
Na katika makundi hayo wapo wafanyabiashara woga ambao ili waonekana kuwa wao ni wafuasi wa chama chao kwa tabia yao ya kuogopa na kukimbia vitisho huvaa skafu, mavazi ya rangi waitakayo na kutundika vipeperushi vya chama kinachowatisha ndani ya magari yao.
Hawafanyi hivyo kwa nia njema, wanafanya hivyo ili kuficha makucha yao na kwa sababu hizo baadaye huhesabiwa kuwa ndio vinara wakubwa wa kukwepa kodi na wanapobanwa na watoza ushuru wanasingizia kuwa biashara hizo si zao ni za vigogo.
Ndiyo maana nasema hivi heri kuwa masikini jasiri kuliko kuwa tajiri mwoga, madhara ya kuwa mfanyabiashara mwoga ni makubwa zaidi kuliko kuwa mtu wa kawaida anayeweza kujitetea mwenyewe na kupigania maslahi yake kuliko kujipendekeza.
Mtindo wa kuwasogeza karibu zaidi matajiri na kuwaingiza kwenye siasa hata kama wao hawapendi na hawaijui, umeathiri kwa kiasi kikubwa nchi ijiendeshe kwa kutegemea walipa kodi wadogo.
Walipa kodi wadogo ni wale wanaomudu kununua sigara na kunywa pombe, hali inayoifanya serikali nayo itegemee zaidi makusanyo ya kodi kutoka kwenye pombe na sigara.
Kwa kuamini kuwa kundi kubwa linalolipa kodi kila siku ni lile la wananchi wengi wa kawaida (masikini) watumiaji hao ndio wanaotegemewa zaidi kuwa mhimili wa nchi ikilinganishwa na idadi ndogo ya wafanyabiashara wakubwa na matajiri ambao hao ni mabingwa wa kukwepa kulipa kodi.
Kwa maana hiyo, kuharibika kwa mfumo mzuri wa utozaji wa kodi kumefanywa na wanasiasa na hasa kutoka ndani ya chama tawala, ama wanatumwa au wanajituma kukusanya fedha kutoka kwa matajiri kwa kisingizio cha kukijenga chama chao, kuendesha harambee wanayodai kuwa ina baraka zote za Baba wa Taifa, hayati Julius Kambarage Nyerere wakiuza picha zake.
Kwa kufanya hivyo lazima wachangie michango mikubwa ya mbio za mwenge, wachangie sherehe za muungano, wachangie kuzaliwa kwa chama tawala, wachangie kuweka makambi ya vijana na jumuiya nyingine, kila siku ni michango tu.
Hiyo haitoshi, majina ya wafanyabiashara wakubwa na matajiri ndiyo yanayowekwa mbele kwenye mapokezi ya viongozi wa serikali na chama tawala, ndio wanaopewa nafasi ya kushikana nao mikono.
Haieleweki utamaduni huo wa kibaguzi asili yake ni nini kwa kuwa umati mkubwa unaojitokeza kuwapokea viongozi hao ni wa aina ya watu wa kawaida ambao hawapaswi kujipanga mbele ya vigogo hao ili wasalimiane nao.
Tunaona jinsi wafanyabiashara na matajiri wanavyopigana vikumbo kupiga picha na viongozi wa juu serikalini, hawa wanang’ang’ania kupiga picha na rais, makamu wake, waziri mkuu, mawaziri na watendaji wengine, wakiwemo makatibu wakuu na makamishna.
Wakifanikiwa hivyo, picha hizo zenye sura za viongozi wa juu serikalini huzikuza sana na kuzibandika kwenye biashara zao ili wale wanaokwenda kukusanya kodi wapumbazike, waone na wakubali kuwa biashara hizo na vigogo nao wamo.
Ni nadra sana kumkuta mtu masikini akiwa ameweka picha za aina hiyo kwenye biashara ndogondogo wanazozifanya, si rahisi mkulima au mfanyakazi akapewa huruma ya kulipa ushuru wa mazao na kodi kutoka kwenye vipato vyao.
Kwa maana hiyo, siasa za kuomba takrima na kisingizio cha harambee zimeweza kukuza tabaka la kiuchumi kati ya matajiri na wananchi masikini, kwamba hao hawana sauti yoyote kwa kuwa hawana kitu, hawatambuliki.
Yupo rais mmoja mstaafu aliyewahi kusema “mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe” nami naongeza kuwa mtaji mzuri wa tajiri ni kukwepa kulipa kodi halali na katika maandiko matakatifu yanasema “heri ngamia akaweza kupita kwenye tundu la sindano kuliko tajiri”.
Kwa maana hiyo chama tawala na serikali yake inayoamini kuwa haiwezi kujiendesha bila wafanyabiashara tajiri, hakiwezi kudumu milele kwa kuwa wapo masikini jasiri ambao ndio wanaoweza kuifikisha nchi yao katika himaya ya milele.
Hayo yanaweza kutokea na ukweli uliopo umesababisha matajiri wengi wawe na woga kushirikiana na Watanzania wenzao katika harakati za ukombozi wakiogopa kupoteza mali zao bila kujua kuwa hayo hayawezi kutokea kama wao ni waadilifu kuliko watawala mafisadi.
Kwa kuwa kikombe cha ujasiri kinatumiwa na masikini na kikombe cha woga kapewa tajiri, kila upande unapaswa kujipima nikiamini kuwa kiongozi mzuri hana sababu ya kulamba miguu ya tajiri, huko ni kujifedhehesha.
Mshikamano wa wananchi wenye ujasiri kwenye nchi yao na hasa wale wanaopenda kupigania maslahi yao, ndio wanaoonekana zaidi wakiwalaki na kuwapokea viongozi wao, lakini wafanyabiashara matajiri hawadiriki kufanya hivyo, ni woga.
Kwa kuwa hawaamini siku ya kufilisika, pia wamesahau tarehe waliyokuwa wakiupiga vita umasikini, hao si wakombozi bali ni vibaraka wa wanasiasa na viongozi wanaoliliwa kwa ufisadi, kwa maana hiyo heri kuwa masikini jasiri kuliko kuwa tajiri mwoga, inatisha.
VIA-TZ-DAIMA

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!