Wafugaji wa jamii ya Kimasai wanaoishi ndani ya Mamlaka a Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wamepinga ujenzi wa hoteli mpya katika kingo za bonde la Ngorongoro kwa sababu licha ya kuathiri mazingira pia itaziba mapito ya wanyamapori na malisho ya mifugo.
Msimamo huo ulitangazwa jana na viongozi wa mila wa jamii hiyo (Malaigwanan) wakati wa mkutano wao na waandishi wa habari uliofanyika Ngorongoro ambapo waliahidi kutumia jeshi la kimila (Morani) kuzuia ujenzi huo iwapo watapuuzwa.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mwenyekiti wa Malaigwanan wa Kata ya Ngorongoro, Francis Ole Siapa alisema eneo linalotarajiwa kujengwa hoteli mpya ni sehemu maalumu kwa ajili ya wanyama aina ya pofu na nyani kuzalia pamoja na ndege aina ya mbuni.
Alisema kuna hatari ya Bonde la Ngorongoro kupoteza hadhi ya urithi wa dunia iwapo mipango na mikakati ya NCAA ya kuboresha utalii kwa kuongeza ujenzi wa hoteli hifadhini, hautadhibitiwa.
Kiongozi mwingine wa Mila, Lazaro Ole Saitoti yeye alikwenda mbali kwa kusema kitendo cha NCAA kuruhusu ujenzi kwenye eneo hilo ni sawa na kuwafukuza wenyeji bila kuwaambia toka.
Meneja uhusiano wa NCAA, Adam Akyo alikiri kuwapo vibali vya ujenzi wa hoteli katika maeneo ya hifadhi tangu mwaka 2006, lakini miradi hiyo haiwezi kutekelezwa bila utafiti wa athari za kimazingira.
Alisema jamii ya wafugaji wa Kimaasai hushirikishwa kwenye mipango na utekelezaji wa miradi yote ndani ya NCAA kwa sababu ni wadau na kuwataka kuondoa hofu kwani ujenzi hautafanyika iwapo utafiti utabaini uwapo wa athari .
No comments:
Post a Comment