Friday, 11 April 2014

WAZIRI MEMBE APOKEA TUZO YA RAIS KIKWETE MAREKANI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amepokea Tuzo ya Rais Jakaya Kikwete ya Utumishi Bora wa Umma Barani Afrika, iliyotolewa na Jarida maarufu la kimataifa la African Leadership Magazine jijini Washington, Marekani.

Waziri Membe alikabidhiwa tuzo hiyo juzi na Balozi wa Nigeria nchini Marekani, Profesa Ade Adefuye ambaye naye aliitoa kwa niaba ya Rais Goodluck Jonathan ambaye, kama alivyo Rais Kikwete, hakuweza kuhudhuria sherehe hiyo iliyofanyika kwenye Hoteli ya St. Regis, Washington.
Jarida la African Leadership ambalo huchapishwa London, Uingereza na Washington, lilimchagua Rais Kikwete kushinda tuzo hiyo kwa mwaka 2013, baada ya wasomaji na wadau wake wengine kumchagua kwa kura ya maoni kuwa ni kiongozi aliyetoa mchango mkubwa zaidi kwa maendeleo ya wananchi wake katika Bara la Afrika.
Mbali na Rais Kikwete, Waafrika wengine ambao wamepewa heshima kwenye sherehe hiyo ni Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Nigeria, Dk Kingsley Moghalu na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mahujaji Wakristo wa Nigeria, John Kennedy Opara ambaye pia ni mshauri wa Rais Jonathan kuhusu uhusiano wa kidini.
Akizungumza kabla ya kukabidhi tuzo hiyo, Balozi Adefuye alieleza anavyomfahamu Rais Kikwete akisisitiza kuwa kiongozi huyo wa Tanzania ni kielelezo cha rika jipya la viongozi wa Afrika, ambao dira na mitazamo yao ni maendeleo ya Bara la Afrika na wananchi wake.
Naye Membe alisema uzoefu wa Tanzania unaonyesha kuwa ushirikiano na uhusiano wa karibu kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ni msingi mkuu wa maendeleo ya nchi yoyote, ikiwamo Tanzania.
Alisema ushirikiano kati ya sekta hizo mbili umeleta manufaa na faida kubwa katika maendeleo ya Tanzania katika sekta za huduma za jamii na katika huduma za kiuchumi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!