Katika kile kinachoonekana kukithiri kwa hali ngumu ya maisha, baadhi ya Watanzania wameanza biashara ya kuuza figo zao kwa gharama kubwa kwa watu wenye mahitaji ya kiungo hicho muhimu mwilini.
Uuzaji huo umetokana na ongezeko la maradhi ya figo miongoni mwa Watanzania kwani takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zinaeleza kuwa kuna wagonjwa 470,000 nchini ambao figo zao zimeshindwa kufanya kazi kabisa na wanahitaji upandikizaji. Katika uchunguzi wake, mwandishi wa gazeti hili alifanya kazi ya kutafuta kama wafanyavyo watu wengine wenye mahitaji hayo na alifanikiwa kukutana na watu kadhaa ambao walikuwa tayari kumwuzia lakini kwa gharama kubwa.
Kijana mmoja alikuwa tayari kumwuzia figo mwandishi wetu. Katika kufikia makubaliano mazungumzo ya kijana huyo, Abiyudi Mtaki na mwandishi wetu yalikuwa hivi:
Mwandishi: “Habari yako kaka, nimepata namba yako kutoka kwa (jina linahifadhiwa) amesema upo tayari kuuza figo yako, mimi nina shida kwa sababu mama yangu anahitaji na hali yake si nzuri.”
Muuzaji: “Nitumie meseji nipo kwenye gari.”
Alipotumiwa meseji alijibu hivi: “Dada yangu mimi naelekea Uganda, kuna mtu kanitumia tiketi jana, wakala nilimwambia kuwa nauza, ila yeye hakuniambia iwapo kuna mtu wa Dar es Salaam anayehitaji.”
Mwandishi: “Jamani kaka tusaidie kwa sababu tuna shida, kwani huyo wa Uganda anakupa shilingi ngapi?”
Muuzaji: “Napata milioni 80 aisee!”
Mwandishi: “Basi sitaweza kupata hizo fedha, ngoja niangalie namna nyingine.”
Muuzaji: “Kwani we ulikuwa na ngapi?”
Mwandishi: “Tuna shilingi milioni 20 tu.”
Kiwango hicho hakikukubaliwa na muuzaji huyo.
CRD: MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment