Watu wasiojulikana wamevunja makaburi, likiwamo la marehemu Sheikh Yahya Hussein lililopo jirani na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Mtoto wa Sheikh Yahya, Hassan Yahya Hussein alisema ameambiwa kwamba kaburi la baba yake na mengine yamevunjwa na askari wa jiji wanaoendesha bomoabomoa katika eneo hilo.
Alisema mbali na kaburi la Shekh Yahya, pia watu hao walivunja kaburi la Sheikh Kassim Bin Juma lililipo jirani na kaburi la baba yake.
“Kwa kweli hadi sasa sielewi kwa nini askari hao wamefanya kitendo hicho,” alisema Hussein.
Alisema Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Bin Shaaban Simba ametuma ujumbe kwenda kwa meya na viongozi wa Manispaa ya Ilala.
Akizungumzia suala hilo kwa simu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki alisema yeye na viongozi wa Manispaa ya Ilala na wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) walitembelea eneo hilo.
Alisema walichobaini ni kwamba makaburi hayo hayakuvunjwa na tingatinga la jiji, bali uchunguzi umeonyesha kwamba yamevunjwa na watu.
Alisema Serikali imeiagiza Manispaa ya Ilala, Bakwata na familia kuandaa ujenzi wa makaburi hayo ili yaweze kuwa kama mwanzo.
Alisema makaburi hayo yamevunjwa na watu ambao wanachukizwa na bomoa bomoa inayoendelea jiji zima la Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe alisema amepata taarifa za tukio hilo kutoka kwa waandishi wa habari.
“Tuwe makini na tukio hilo kwa sababu wanaovunjiwa vibanda hawafurahishwi, hivyo wanaweza kutumia mwanya huo kufanya hujuma zozote ili ionekane askari wa jiji wamefanya kitendo hicho,” alisema.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment