Wednesday, 30 April 2014

MTUHUMIWA WA MAUAJI YA BILLIONEA ERASTO MSUYA AACHIWA HURU!

OFISI ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini imemfutia kesi ya mauaji ya kukusudia mfanyabiashara Joseph Damas ‘Chusa’ anayetuhumiwa kumuua mfanyabiashara mwenzake wa madini ya tanzanite, Erasto Msuya (43).

Hati ya kumwachia huru mtuhumiwa huyo ilisainiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Elieza Feleshi na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuiwasilisha kwa Hakimu Munga Sabuni anayesikiliza kesi hiyo.
“Mheshimiwa hakimu upelelezi wa kesi hii umekamilika na ikikupendeza upande wa mashitaka tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea washitakiwa maelezo ya mashahidi kabla ya kulipeleka jalada la mashitaka Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa.
“Aprili 16 tulipokea hati ya kuachiwa huru kwa mshitakiwa namba saba Joseph Damas,” alisema Wakili wa Serikali, Julius Semali.
Mbali na Chusa, washtakiwa wengine katika kesi hiyo namba 6/2013 ni Sharif Athuman (31), Shaibu Jumanne ‘Mredii’ (38), Mussa Mangu (30), Jalila Said (28), Sadiki Jabir ‘Msudani’ (32), Karim Kihundwa (33) na Alli Majeshi.
Baada ya kupokewa kwa taarifa hiyo, Hakimu Munga aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 6, mwaka huu na kuamuru washitakiwa saba, waliosalia katika kesi hiyo kurejea rumande.
Marehemu bilionea Msuya aliuawa Agosti mwaka jana kwa kupigwa risasi hadi kufa saa 6 mchana kando ya barabara kuu ya Arusha-Moshi, eneo la Mijohoroni, Wilaya ya Hai, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
TZ-DAIMA

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!