Wednesday, 30 April 2014

TAJIRI WA ZAMANI ATANGAZA KUUZA FIGO YAKE MOJA ILI KUJIKWAMUA KIUCHUMI"


MKAZI wa Iringa Mjini, Ramadhan Mrisho (Makosa), ametangaza kuuza figo yake moja kwa kile anachodai anatafuta fedha za kumsaidia kuendesha maisha yake.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni mjini Iringa, Mrisho, alisema amefikia uamuzi wa kutangaza kuuza figo yake akiwa na akili timamu. 


 “Nisidhaniwe nimekuwa na akili tofauti,” alisema Mrisho na kuongeza; “Nina akili timamu, nimeamua kuchukua uamuzi huu kama nilivyosema kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.”
Hata hivyo Mrisho hakuwa tayari kutaja bei ya figo yake iwapo atapatikana mteja. Alisema anajua wapo watu wenye matatizo ya figo na wamekuwa wakisafiri mbali na nchi kutafuta tiba.
“Kama kuna mtu ana matatizo ya figo au ameitafuta ameikosa aje kwangu tukubaliane bei,” alisema Mrisho.
Katika harakati zake za kutafuta fedha za kusaidia familia yake, Julai, 2012 Mrisho alitishia kujinyonga, tukio alilopanga lifanyike Uwanja wa Samora kwa sharti kuwa mashuhuda kutalipa kiingilio ambacho kingekusanywa kwa ajili ya familia yake.
Wakati huo huo, Mrisho alinukuliwa akisema kuliko familia yake kuendelea kutaabika ni bora ajitoe mhanga ili fedha zitakazopatikana kama kiingilio zitumike kusaidia watoto yake.
Hata hivyo, alisema mpango wake haukufanikiwa kwani akiwa kwenye maandalizi walitokea watu mbalimbali wakiwemo Polisi waliompa ushauri nasaha, hivyo alisitisha mpango huo.
“Sasa nimekuja na mpango mpya, mpango huu si mwingine zaidi ya huu wa kuuza figo yangu moja, naamini nikifanikiwa nitapata fedha,” alisema.
Mrisho ambaye ni maarufu mkoani Iringa kutokana biashara zake zake nyingi alizokuwa akifanya mwanzoni mwa miaka ya tisini baada ya kuacha kazi yake ya ubaharia.
Wakati akifika mjini Iringa, Mrisho alikuwa hanywi pombe, bali alikuwa mnyenyekevu ambapo alijikita kuisaidia jamii ya watu wa Iringa kutunza mazingira kwa kupanda miti kila mtaa.
Aliongoza kupanda miti ya aina mbalimbali ikiwemo ya matunda inayoonekana mjini Iringa.
Mrisho ndiye alikuwa mtu wa kwanza mjini Iringa kuingiza mabasi madogo ya kusafirisha abiria aina ya Coaster yaliyokuwa yakifanya kazi katika maeneo mbalimbali ya mjini Iringa.
Pamoja na biashara ya usafirishaji, Mrisho alijikita katika biashara ya hoteli. Na kwa muda mrefu aliendesha hoteli ya CATS iliyopo jirani na Maktaba ya Mkoa wa Iringa.
Kwa kadri biashara ilivyozidi kumchanganyia katika hoteli hiyo, alimua kuibadili jina na kuiita MAKOSA CATS Hotel.
Katika hoteli hiyo bendi nyingi zimepiga muziki na kwa mara ya mwisho, mwanamuziki Macay Fanta alikuwa akifanya shoo zake mpaka pale Mrisho aliposhindwa kuiendesha mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Mtandao wa biashara za Mrisho haukuishia hapo, alikuwa pia akimiliki hospitali maarufu sana iliyopo jirani kabisa na Soko Kuu la Mjini Iringa, ambayo ilikuwa ikiitwa MAKOSA.
Alisema biashara zote hizo haziko tena mikononi mwake na ugumu wa maisha unazidi kumwandama. Alisema anatafuta njia za kujikwamua na njia halali anayoiona mbele yake hivi sasa ni kuuza figo yake moja


CRD: MAJIRA

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!