MAZISHI ya Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, hayati Nelson Mandela, yanatarajia kuweka rekodi ya dunia kwa kuhudhuriwa karibu na marais 140 kutoka sehemu mbalimbali duniani. Taarifa iliyochapishwa na Gazeti la DailyMail la Uingereza jana, ilisema viongozi hao wataungana na familia na wananchi wa Afrika Kusini.
Lakini kwa mujibu wa gazeti hilo, Malkia wa Uingereza, Elizabeth II, hatohudhuria mazishi ya Mandela baada ya kushauriwa na jopo la wasaidizi wake. Jopo hilo lilisema kutokana na umri mkubwa alionao Malkia Elizabeth hataweza kuhimili mwendo mrefu wa ndege kutoka Uingereza hadi Afrika Kusini.
Kutokana na hali hiyo, Malkia Elizabeth atahudhuria misa maalumu iliyoandaliwa katika Kanisa la Westminster Abbey mjini London na kusaini kitabu cha kumbukumbu.
Gazeti hilo lilisema tayari Rais wa Marekani, Barack Obama na marais wastaafu wa nchi hiyo, George W. Bush na Bill Clinton na wake zao, Hillary Clinton na Laura Bush wataungana na viongozi wengine watakaoaga mwili wa Mandela katika Uwanja wa Taifa wa Afrika Kusini wa First National Bank (FNB).
Taarifa ya Ikulu ya Marekani ilisema marais hao wote watatumia ndege moja ya Airforce One.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais mstaafu, Bush atahudhuria mazishi ya Mandela baada ya kukubali mwaliko aliopewa na Rais Obama.
Viongozi wengine ambao wamethibitisha kuhudhuria mazishi hayo ni Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, Kiongozi wa Kidini wa Jimbo la Tibet, Dalai Lama, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis I na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon ambaye jana alitarajia kuondoka nchini Ufaransa kuelekea Afrika Kusini.
Misa
Askofu mstaafu, Desmond Tutu, anatarajiwa kuongoza misa ya mazishi.
Habari zinasema zaidi ya watu 80,000 wanatarajiwa kuuaga mwili wa Nelson Mandela katika Uwanja wa FNB uliopo mjini Soweto, Johannesburg.
Akizungumza na waandishi wa habari, Msemaji wa familia ya Mandela, Temba Matanzima, alisema Serikali imeandaa utaratibu ambao utaelekezwa kwa maelfu ya wananchi watakaohudhuria uwanjani hapo kutoa heshima za mwisho.
Jana asubuhi, maelfu ya wananchi wa Afrika Kusini walikusanyika katika makanisa, misikiti, masinagogi na maeneo mbalimbali kwa ajili ya kumuombea Mandela ambaye alifanikiwa kuleta mapatano katika Taifa hilo bila kujali rangi, makabila wala tofauti za kidini.
Shughuli za kumuombea Mandela zimedumu kwa siku kadhaa tangu Desemba 6, mwaka huu, baada ya Rais Jacob Zuma kutangaza kifo cha shujaa huyo.
Wananchi wa Afrika Kusini wataanza kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Mandela kesho na kesho kutwa yaani Desemba 11 mwili wa kiongozi huyo utapelekwa Ikulu ya Pretoria.
Desemba 14, mwili huo utasafirishwa kwa ndege ya kijeshi hadi mji wa Mthatha, ambako utabebwa kwa gari maalumu kuelekea katika Kijiji cha Qunu na siku inayofuata atazikwa.
Rais Zuma alisema: “Shughuli ya kuagwa Mandela itafanyika kwa uwazi na tutazingatia vigezo vyote vya urithi wake. Tunatakiwa kumuombea kwa kila namna, kuimba nyimbo zote, kwa sauti yoyote, tucheze na kufanya lolote litakalokuwa na maana ya kuenzi kazi ya Mandela na mapinduzi aliyoleta.”
Juzi, Rais Zuma alihudhuria misa ya maombezi katika Kanisa la Methodist ambalo hutumiwa na wazungu walio wengi jijini Johannesburg, wakati Rais mstaafu, Thabo Mbeki, aliungana na wananchi wengine katika masinagogi kumuombea Mandela.
Watu wengi wanadaiwa kujumuika katika Kanisa Katoliki lililopo mjini Soweto, ambapo walipokea wageni wengi kutoka London huku Askofu Caunterbury, Justin Welby Kiongozi wa Kanisa la Anglikana ambalo lina wafuasi takriban milioni 80 duniani.
Kabla ya kuzikwa, wafuasi wa Chama cha ANC watakuwa na kongamano la kuaga mwili wa Mandela, Desemba 14 litakalofanyika katika ngome ya kijeshi ya Waterkloof Air Force Base mjini Pretoria.
Qunu
Katika Kijiji cha Qunu alikozaliwa Mandela, wananchi walikusanyika katika kanisa ambalo lilijengwa na mama yake Mandela miaka mingi iliyopita kumuombea.
Askofu wa Kanisa hilo, Sabelo Ngqeleni, alisema: “Leo tunasherehekea kumbukumbu ya mtu muhimu katika Taifa letu.
“Lazima tulikumbuke kanisa hili ambalo muasisi wake ni mama wa Madiba, Noqaphi Nosekeni. Lilianza kutoa huduma mwaka 1960.
“Wakati sisi tukiendelea hapa, kule Mthataha watu zaidi 6,000 wamekusanyika ambako ni katika makazi ya Madiba.
“Vijana kwa wazee wamekusanyika kwenye viwanja vya Ngangelizwe ambako kumewekwa mahema, wakiwa wamevalia fulana zenye picha ya Madiba.
Mama mzazi wa Madiba alifariki dunia mwaka 1968.
Mandela alifariki dunia Alhamisi iliyopita akiwa na umri wa miaka 95 huko Houghton, Johannesburg.
No comments:
Post a Comment