Ujenzi wa daraja Kigamboni. |
Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limesema ujenzi wa daraja la Kigamboni, upo katika hali nzuri, ingawa kuna changamoto ya wananchi kumi ambao hawajahama, kupisha ujenzi huo.
Meneja Kiongozi Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa shirika hilo, Eunice Chiume alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.
"Ujenzi wa daraja unaendelea vizuri sana, ila changamoto ni wale wanaotakiwa kulipwa fidia kugoma kuondoka, kwa upande wa Kigamboni wapo watu wanane na upande mwingine wapo wawili," alisema.
Aliomba Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi kuingilia kati suala hilo ili ujenzi uendelee kama ulivyopangwa na hatimaye daraja likabidhiwe ifikapo 2015.
Katika hatua nyingine, NSSF imejenga nyumba 279 za bei nafuu katika eneo la Kijichi wilaya ya Temeke, ambazo zitauzwa kwa wanachama wake kwa fedha taslimu au mkopo.
Alisema nyumba hizo ambazo awali zilikuwa zikiuzwa kwa mkopo kupitia Benki ya CBA kwa sasa mkopo huo utatolewa na shirika hilo kwa riba ya asilimia 11.4 kwa mwaka kwa miaka 15.
Alisema nyumba hizo zipo za aina tofauti kuanzia za vyumba viwili hadi vinne na bei zake huanzia kati ya Sh 64,875,310 hadi Sh 112,500,000 bila VAT kulingana na aina.
Alisema wanachama ambao wangependa kuwa wanunuzi wa nyumba hizo wafike katika ofisi za NSSF kwa ajili ya maelezo zaidi na huduma.
No comments:
Post a Comment