Sunday 15 April 2018

Makonda: Wanawake matapeli kukiona

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (pichani) amesema wanawake ambao watawasingizia wanaume kuhusu watoto, watashtakiwa na wanaume husika.


Hata hivyo, amesema pia wanaume watakaoitwa baada ya kutajwa na wenza wao kuwa wamewatelekeza watoto wao na kukaidi mwito huo, watatangazwa kwenye vyombo vya habari yakiwemo magazeti. Akizungumzia suala hilo ofisini kwake jana, Makomnda alisema kuwa ofisi yake ndiyo itakayogharamia upimaji wa Vipimo vya Vinasaba (DNA) kwa wanaume waliotajwa ili kupata uhakika wa uhalali wa baba wa mtoto ili haki iweze kutendeka kwa pande zote Katika hatua nyingine, wabunge na viongozi wa dini ni kati ya makundi ya wanaume waliotajwa kuhusika na kuwatelekeza watoto kwa wanawake waliozaa nao kwenye usikilizwaji wa malalamiko unaendelea chini ya usimamizi wa ofisi hiyo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Kazi hiyo itakamilika Ijumaa wiki hii. Kwa mujibu wa Makonda hadi sasa, wabunge waliotajwa ni 47 huku viongozi wa dini ni 14. Aidha katika orodha hiyo anadaiwa kutajwa pia mmoja wa wanasiasa ambao walijitokeza kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Hadi jana wanawake 900 walikuwa wamehojiwa huku zaidi ya wanawake 7,000 wakitajwa kujitokeza. Akizungumzia mwito kwa wale watakaotajwa, Makonda alisema baada ya kutajwa ofisi yake itatoa barua ya mwito kwa wahusika na kwamba kwa wale watakaokaidi na hivyo kushindwa kufika, hatua itakayofuatia itakuwa ni majina yao kutangazwa kwenye vyombo vya habari.
Kuhusu kutajwa kwa viongozi wa kisiasa na kidini katika tukio hilo, Makonda alisema inasikitisha kuona kuwa hata viongozi wa kisiasa na dini wamekwepa majukumu ya kuwahudumia watoto wao na kuwa ni wazi kuwa kuna haja kubwa ya jamii kuendelea kuelimishwa kuhusiana na umuhimu wa kutunza watoto. Alisema, watoto wana haki ya kulindwa, kuhudumiwa na kupewa mahitaji yote muhimu na kwamba wapo wanaume ambao wameshaanza kutoa matunzo kwa wanawake ambao walikuwa wamewatelekeza na kusisitiza kuwa hatua hiyo inatia moyolakini aliwataka wanawake kutodanganyika na hatua hiyo kwa kuwa wanaweza kuwakwepa tena.
“Najua hapa tunapigania haki ya mtoto zaidi na wala si kuoneana wala kudharirishana sasa kama kuna wanawake ambao wanaona kuwa wanaume waliokuwa wakiwakwepa kuwasaidia kwa sasa wameshaanza kuwasaidia wajue kuwa hiyo inaweza kuwa ni msaada wa muda, ila wakiwaleta hapa inakuwa ni makubaliano kabisa ya kusaidiwa kila mwezi,” alisema.
Aliwataka wanawake kutoogopa kujitokeza kuwasilisha malalamiko yao kwa kuwa hakuna kibaya kitakachowakuta huku akibainisha kuwa ofisi yake itagharamia vipimo vya DNA kwa wanaume ambao watawakataa watoto waliotajwa kuwa ni wa kwao. Makonda alisema pia kuwa jana wanaume 10 nao walijitokeza kulalamikia kunyang’anywa watoto. Mmoja wa wanasheria wanaowasikiliza wanawake hao, Amanieli Kidali alisema licha ya kuwapo kwa idadi kubwa ya wanawake wanaolalamikia matunzo lakini wapo ambao wanataka kuongezewa kiwango cha matunzo husika wakati tayari Mahakama ilishaweka kiwango cha wao kulipwa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!