Wednesday, 7 March 2018

Hatari kukaa saa nane bila kushughulisha mwili

MOJAWAPO ya kanuni muhimu za afya za kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni kufanya mazoezi. Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kwa watu wazima wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 64, ni muhimu kufanya mazoezi ya mwili kwa muda usiopungua dakika 150 ndani ya wiki moja.


Mazoezi ya kiwango chochote husaidia damu kuzunguka kwa urahisi mwilini na ubongo kupata kiasi cha kutosha cha hewa ya Oksijeni ambayo huchangamsha akili.
Mazoezi pia husaidia mwili kuwa na usawaziko sawia wa vichocheo vya mwili. Mtu yeyote ambaye hafanyi mazoezi kwa sababu yoyote ile ni lazima ajiandae kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza mapema katika maisha yake.
Takwimu za WHO zinaonesha kuwa takribani asilimia 60 hadi 85 ya watu duniani, hawafanyi mazoezi ya kutosha. Mwaka 2010, WHO iliripoti kwamba asilimia 81 ya vijana wenye umri kuanzia miaka 11 hadi 17 duniani kote, walikuwa hawafanyi mazoezi ya kutosha.
Hali hii kwa sasa inachangia ongezeko la magonjwa sugu yanayosababisha vifo vingi duniani. Miongoni mwa magonjwa hayo ni msongo wa mawazo, kisukari, shinikizo la damu, kiharusi, magonjwa ya moyo, matatizo ya figo na aina mbalimbali za saratani kama vile saratani ya tezi dume, matiti na utumbo mpana.
Kwa bahati mbaya sana watu wengi hasa wafanyakazi wa maofisini wanakosa muda wa kufanya mazoezi kwa sababu ya kuwa na majukumu mengi ya kikazi.
Watu wengi wanatumia zaidi ya saa nane kila siku wakiwa wamekaa na bila kushughulisha miili yao kiasi cha kutosha. Mtu anatoka nyumbani asubuhi na kukaa katika chombo cha usafiri kwa takribani saa moja, akifika ofisini anakaa kwenye kiti kwa saa saba na akirudi nyumbani anakaa kwa zaidi ya saa tatu akiwa anaangalia televisheni.
Utafiti ulioongozwa na Profesa Ulf Ekelund wa Chuo Kikuu cha Cambridge na kuchapishwa Julai 27, 2016 katika jarida la kisayansi la The Lancet, unaonesha kuwa kukaa kwa saa nane kila siku bila kushughulisha mwili kunaongeza hatari ya mtu kufa mapema kwa kiwango kinachofikia hadi asilimia 60.
Wataalamu kupitia utafiti huo wanafafanua kwamba mfanyakazi wa ofisini anaweza kujitafutia fursa ya kufanya mazoezi mepesi kila siku na kupunguza hatari ya magonjwa yanayosababishwa na maisha ya kutokuushughulisha mwili.
Mazoezi mepesi kila siku yanaweza kuonesha tofauti kubwa katika afya ya mwili. Inashauriwa kwa wafanyakazi wanaokaa ofisini, wanaweza kupunguza muda wa kukaa kwa kusimama wanapofanya mikutano ya asubuhi.
Lakini pia kusimama wakati wa kupokea simu au kumpigia mtu simu uwapo ofisini, inaweza kuwa fursa nyingine ya mazoezi. Kama una shida na mfanyakazi mwenzako, nenda ukamuone ofisini badala ya kumpigia simu au kumtumia barua pepe na kubaki ukiwa umekaa.
Wakati wa kutoa nakala au kuchapa ripoti kwa mashine ni fursa nyingine nzuri ya kufanya mazoezi ya kunyoosha na kukunja miguu huku ukisubiria kazi hiyo ikamilike. Printa na mashine za fotokopi zikiwa katika chumba kingine, pia hutoa fursa ya kufanya mazoezi unapokwenda kupata huduma hiyo nje ya ofisi yako. Kupanda ngazi ni fursa nyingine ya kufanyisha misuli ya miguu mazoezi.
Pia kunasaidia moyo kufanya kazi zake vizuri. Lakini pia kama kuna vyoo vya kuchuchumaa na vyoo vya kukaa, pendelea matumizi ya vyoo vya kuchuchumaa kwa ajili ya kujipatia fursa ya mazoezi ya misuli ya mapaja.
Wakati wa chakula cha mchana mfanyakazi anaweza kufanya mazoezi ya kutembea kwa dakika kadhaa hasa kama atachagua kula katika mgahawa ambao upo mbali kidogo na sehemu ya kazi.
Ukiwa umekaa ofisini unaweza kufanya mazoezi ya kuimarisha misuli ya shingo, mabega na pango la nyonga mara kwa mara bila kuathiri utendaji wa kazi zako au kazi za muajiri.
Mazoezi ya kunyoosha mikono na kukunja pamoja na kukunjua viganja kama unaita mtu mara nyingi, kuinua mabega na kuzungusha shingo mara kwa mara yanaweza kufanywa wakati wowote ukiwa umekaa.
Zoezi jingine linaloweza kufanyika ofisini ni lile la kusimama na kukaa kwenye kiti angalau mara kumi. Zoezi hili linaweza kufanyika kila baada ya saa mbili za kukaa.
Mazoezi ya kubana na kuachia misuli ya njia ya haja kubwa mara kwa mara maarufu kama mazoezi ya ‘Kegel’ yanaimarisha misuli ya njia ya haja kubwa, via vya uzazi, kibofu cha mkojo na misuli ya nyonga, na yanaweza kufanywa wakati wowote unapokuwa unaendelea na kazi ofisini.
Baada ya kazi hakikisha unafanya mazoezi mepesi kwa ajili ya afya ya moyo na mapafu kabla ya kuoga na kuanza kutazama televisheni wakati wa mapumziko ya jioni au usiku.
Mfanyakazi akizingatia mfumo huu wa maisha kila siku, atapata fursa ya kuimarisha afya yake hata kama hana muda wa kutosha wa kwenda kufanya mazoezi na michezo viwanjani au kwenye maeneo maalumu.


Makala haya yameandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanaopambana na Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza Tazania (TJNCDF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TANCDA).

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!