Monday 20 February 2017

JINSI YA KUKABILIANA NA UGONJWA WA KUHARA KWA WATOTO


Katika magonjwa ambayo huwasumbua watoto mara kwa mara ni ugonjwa wa kuhara, lakini habari njema ni kuwa ugonjwa huu humalizika ndani ya siku chache mtoto anapohudumiwa vyema.



Lakini pamoja na hayo ni vyema kujua jinsi ya kumsaidia mtoto anayekabiliana na ugonjwa huu na jinsi ya kuwakinga wale wasio na ugonjwa.

 Ni nini kinachosababisha ugonjwa wa kuhara?
Kuhara ni ugonjwa ambao husababishwa kwa kiasi kikubwa na aina ya virusi, lakini pia yaweza kua bacteria au vimelea vinginevyo vya magonjwa. Mtoto(mgonjwa) hupata choo mara nyingi ambacho ni majimaji.

Aina ya vijimelea vinavyosababisha kuhara kwa watoto hutegemea eneo la kijiografia kulingana na viwango vya usafi wa mazingira, hali ya kiuchumi na usafi wa mwili. Kwa mfano nchi zinazoendelea ambapo hali ya usafi wa mazingira ni duni na maeneo ambayo kinyesi cha binadamu hutumika kama mbolea, hukabiliana na milipuko ya magonjwa ya kuhara mara kwa mara kwa sababu taka hizi zitokanazo na binadamu ni rahisi kuingia katika vyakula na maji ya kunywa.

Kwa ujumla, vimelea vinavyosababisha kuhara ni rahisi kuambukiza kutoka mtu mmoja hadi mwingine au mtu kupata  ugonjwa kwa kujigusa na mazingira yaliyo na vimelea vya ugonjwa huu. Maambukizi yanayosababisha ugonjwa wa kuhara yanaweza kusambazwa kupitia: Mikono michafu iliyoshika sehemu zenye vimelea vya ugonjwa, maji machafu au chakula kilichoingia vimelea vya ugonjwa, wanyama wa kufugwa nyumbani, kujigusa katika mazingira yaliyochafuliwa na kinyesi cha binadamu na wadudu warukao na watambaao kama inzi na mende.

Virusi ni sababu kuu ya ugonjwa wa kuhara kwa watoto (hujulikana wakati mwingine kama “mafua ya tumbo” ambayo yaweza pia kusababisha kutapika). Kuna aina tofauti tofauti ya virusi vinavyosabisha kuhara kwa watoto, ambavyo husambazwa majumbani, shuleni na hata watoto wanapocheza na watoto wenzao. Ingawa dalili za ugonjwa huu huwepo kwa siku chache lakini waweza kuwaathiri sana watoto wachanga ambao hawawezi kunywa maji mara kwa mara na wananapata upungufu wa maji mwilini ( kwa kitaaalamu -dehydration).

Kundi la virusi lijulikanalo kama “Rotavirus” ndilo linahusika  zaidi na magonjwa ya kuhara kwa watoto. Virusi hawa husababisha mtoto kuhara choo cha maji maji mara kwa mara ingawa sio watoto wote huonyesha dalili.

Kundi jingine la virusi hujulikana kama “coxsackievirus” ambalo husababisha kuhara kwa watoto, lakini sio sana ukilinganisha na kundi lililotangulia.

Pia kuhara kwa watoto kwaweza kusababishwa na uambukizi wa bacteria tofauti ambao kitaalamu wanajulikana kama” Escherichia coli”, “ Salmonella enteritis”, “Shigella”, “Giardia” na “Cryptosporidium”.

Uambukizi wa magonjwa ya kuhara ni kawaida kuwakumba watoto walio wengi, lakini pia kuhara kunaweza kuwa dalili ya magonjwa mengine yasiyo ya uambukizi, mfano kuhara kunaweza kuashiria mzio (allergy), tumbo la mtoto linaposhindwa kumeng’enya maziwa (kwa kitaalamu-lactose intolerance) hususani anapobadilishiwa maziwa, kutoka maziwa ya mama na kutumia maziwa ya ng’ombe. Pia kuna
                        magonjwa mengine ambayo huathiri                                   tumbo (kwa kitaalamu-Inflammatory bowel disease)

Dalili za ugonjwa wa kuhara kwa watoto
Dalili za ugonjwa huu huanza na tumbo kunyonga na hufuatiwa na kuhara ambako hudumu  kwa siku chache. Uambukizi wa virusi au bakteria wasababishao kuhara yaweza kupelekea pia mtoto kupata homa, kukosa hamu ya kula, kichefuchefu, kutapika, kupungua uzito, na upungufu wa maji mwilini.

Kama ni uambukizo uliosababishwa na virusi, mara nyingi watoto huanza kupata homa na kutaapika, na hufuatiwa na kuhara.

Kinga
Huwa ni vigumu sana kuwakinga watoto wasipate maambukizi yanayosababisha ugonjwa wa kuhara, zifuatazo ni baadhi ya mbinu zitazosaidia kumkinga mwanao kupata maradhi ya tumbo:
o   Hakikisha watoto wananawa mikono vyema kwa maji safi na sabuni mara kwa mara, hususani baada ya kutoka chooni au kabla ya kula. Kunawa mikono ni njia iliyo thabiti katika kuwakinga watoto na maambukizi yanayosababisha kuhara na ambayo huambukizwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. Mikono michafu hubeba vimelea vya magonjwa na watoto hupenda kung’ata na kunyonya vidole, kula kwa kutumia mikono au kuingiza kiganja mdomoni.
o   Hakikisha vyoo na bafu nyumbani kwako viko katika hali ya usafi ili kuzuia ueneaji wa vimelea vya magonjwa.
o   Osha matunda na mbogamboga kwa kutumia maji safi kabla ya kula, kwa sababu maji na chakula huweza kubeba vimelea vinavyoweza kusababisha magonjwa ya kuhara.
o   Hakikisha jikoni kwako ni pasafi, safisha vizuri kwa kutumia maji safi na sabuni meza iliyotumika kukatia nyama mbichi, na safisha vizuri vyombo vilivyowekewa nyama mbichi hususani zile zitokanazo na ndege.
o   Hakikisha nyama ambayo haijapikwa inawekwa kwenye jokofu pindi inapofikishwa nyumbani, au kama huna jokofu hakikisha inachemshwa pindi unapofika nyumbani kutoka buchani au sokoni. Na kila baada ya mlo, vyakula vinavyobaki vihifadhiwe vizuri katika jokofu.
o   Kamwe usinywe maji ya vijito, mito, chemchem, bombani au ziwani ambayo hayakuchemshwa. Pia chukua tahadhari unaponunua chakula cha mtaani kwa sababu vyakula hivi kwa asilimia kubwa huandaliwa katika mazingira machafu ambayo huwa hayakaguliwi na bwana afya.
o   Usioshe vyombo vinavyotumiwa na wanyama katika sinki moja na vyombo ambavyo hutumiwa na familia.
o   Hakikisha wanyama wafugwao nyumbani wanatengewa sehemu tofauti ya kula mbali na sehemu ya kula ya familia.
Ni wakati gani unahitajika kumpeleka mtoto hospitali?    
Mpeleke mtoto mchanga hospitali haraka kama amepata ugonjwa wa kuhara, na kwa watoto wakubwa walio na dalili zifuatazo:
o   Kuhara kusikoisha baada ya siku chache.
o   Mtoto amepata homa.
o   Kutapika mara kwa mara na mtoto hataki kunywa maji.
o   Maumivu ya tumbo.
o   Mtoto anaharisha damu na choo chenye makamasi.
Pia mpeleke mtoto hospitali haraka kama ana upungufu wa maji mwilini. Dalili za upungufu wa maji mwilini  ni hizi zifuatazo:
o   Kuchoka na kizunguzungu kwa watoto wakubwa.
o   Kukauka mdomo au ulimi kuwa mkavu.
o   Machozi kidogo au bila machozi mtoto anapolia.
o   Ngozi kusinyaa na kuwa kavu.
o   Kukosa kupata mkojo katika muda wa saa 10 kwa watoto wakubwa au mkojo kidogo na wa njano kwa watoto wadogo
o   Pampa au nepi  kavu katika muda wa saa sita na zaidi kwa watoto wachanga au mkojo kidogo wa njano.
o   Utosi wa mtoto unabonyea.
o   Macho yamebonyea kuingia kichwani.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!