Tuesday 22 November 2016

AFIKISHWA MAHAKAMANI KUJIBU MASHTAKA 448


MFANYAKAZI wa kampuni ya GBP Tanzania Ltd iliyopo Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Onesimo Yohana (40), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma kujibu mashtaka 448 yakiwamo 220 ya kughushi nyaraka." 


Mengine ni 110 ya wizi wa Sh. milioni 634, mengine idadi kama hiyo ya kuwasilisha nyaraka za kughushi na mashtaka manane ni ya kutakatisha fedha kinyume cha sheria.


Mshtakiwa huyo alifikishwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Sylivester Kainda.
Hata hivyo, mshtakiwa alikana mashtaka yote na kupelekwa mahabusu katika Gereza la Bangwe kwa kukosa wadhamini.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Mkoa wa Kigoma, Javalin Rugaihuruza, ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kwamba una mashahidi watatu.
Upande wa mshtakiwa unatetewa na Wakili wa Kujitegemea, Daniel Rumenyela.
Hakimu Kainda aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 24, mwaka huu itakapoendelea kusikilizwa.
Awali, akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali, Javalin Rugaihuruza, alidai kuwa katika tarehe tofauti Januari, 2015 hadi Machi 6, mwaka huu, eneo la Mwanga katika kituo cha mafuta cha GBP Manispaa ya Kigoma/Ujiji, mshtakiwa alifanya makosa 448.
Wakili Rugaihuruza alifafanua kuwa kati ya makosa hayo, 220 ni ya kughushi nyaraka, makosa 110 ya wizi wa Sh. milioni 634, makosa 110 ya kuwasilisha nyaraka za kughushi na makosa manane ya kutakatisha fedha kinyume cha sheria.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!