Monday, 23 May 2016

WANAFUNZI DAR WAWAPIGA JEKI WENZAO WA MAZINGIRA MAGUMU


Wanafunzi wa Shule ya Msingi Fountain Gate Academy ya Tabata jijini Dar es Salaam, wakijiandaa kwa maandamano kwenye siku ya kutoa shuleni hapo (Charity Day).





WANAFUNZI wa Shule ya Msingi Fountain Gate Academy ya Tabata jijini Dar es Salaam, wametoa msaada wa vyakula vya aina mbalimbali kwa watoto wenzao wa vituo vya kulelea walio katika mazingira magumu.
Walitoa msaada huo wenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni tano katika sherehe maalum ya kila mwaka iliyofanyika shuleni hapo ambapo hununua mahitaji mbalimbali kwa watoto wenzao.
Mgeni rasmi kwenye sherehe hiyo ambayo ilihudhuriwa pia na wazazi wa wanafunzi hao, alikuwa Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Anglikana, Donald Mtetemela.
Akizungumza kwenye sherehe hiyo, Mkurugenzi wa shule hiyo, Japhet Makau, alisema wazo la kuwa na siku kama hiyo lilitokana na dhamira ya shule hiyo katika kutimiza nguzo tatu za ufahamu, busara na vipaji.
Alisema Fountain Gate inaamini katika kumuandaa mtoto, si kumpa taaluma pekee kwani wanatoa nafasi ya kutambua na kukuza vipaji vya watoto katika maeneo mbalimbali ya michezo na muziki ili kuwajengea kujiamini.
“Katika kuwajenga watoto kuwa na hekima na busara, kwanza tunaamini katika kumlea kwa kujenga kuwa na hofu ya Mungu...kama inavyoaminika kumcha Mungu ni chanzo cha hekima,” alisema Makau.
Alisema tukio hilo la kutoa msaada linalenga kuwafundisha watoto kuhusu upendo, kuwathamini na kuwajali wenzao wanaoishi kwenye mazingira magumu ambao hawajapata bahati ya kuishi na wazazi kama wao.
Alisema familia ya Fountain Gate wanaichukulia siku hiyo ya kutoa kumshukuru Mungu kwa neema aliyowajalia kwani wanaamini kuwa wako hivyo walivyo kwa neema za Mungu na si kwa uwezo wao.
“Tunaona tunawajibika kutoa kidogo tulichonacho kwa ajili ya wenzetu, familia hii ya Fountain Gate kwa umoja wao wamechangia vyakula, nguo, vifaa vya usafi, fedha taslim ambavyo vyote wamekabidhi ili iwe chachu kwa shule na taasisi nyingine katika kujenga utamaduni wa kuwasaidia wengine,” alisema.
Mgeni rasmi, Askofu mstaafu Mtetemelwa, aliasa jamii kujenga utamaduni kama ulioonyeshwa na jamii ya Fountain wa kuwasaidia wengine wasio na uwezo.
“Watu waone ni wajibu wao kutoa hata kidogo walichonazo kusaidia wengine, kutoa ni moyo na si utajiri na naishukuru jamii hii ya Fountain maana imeonyesha mfano wa kuigwa katika jamii,” alisema.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!