Monday, 23 May 2016

FAHAMU KUHUSU UGONJWA WA KISUKARI


Kisukari ni ugonjwa unaotokea pale ambapo sukari ya glukozi kwenye damu inapozidi kiwango cha kawaida. Hujulikana kama diabetes mellitus kwa kiingerezaUgonjwa huu haumbukizwi na huathiri ufanyaji kazi wa seli na tishu mbalimbali za mwili hasa moyo,figo,macho na mishipa ya damu.


Namna Kisukari Kinavyotokea
Kila seli ya mwili wa binadamu inahitaji nishati ili iweze kufanya kazi, chanzo kikuu cha nishati hii ni sukari aina ya glukozi. Glukozi ni aina ya sukari inayotokana na kumeng’enywa kwa vyakula vya wanga. Glukozi husambazwa na damu ili kuzifikia seli mbalimbali za mwili baada ya kunyonywa kwenye utumbo.
Unapokula chakula,  glukozi huongezeka kwenye damu baada ya kunyonywa kwenye utumbo. Kongosho huzalisha homoni ya insulini ya kutosha ili kuisafirisha glukozi kutoka kwenye damu iingie kwenye seli na hivyo kupunguza kiasi cha glukozi kwenye damu.
Pale inapotokea insulini imepungua au mwili unashindwa kuitumia (Insulin resistance), glukozi hubaki kwenye damu zaidi ya kiwango chake cha kawaida na hivyo ugonjwa wa kisukari kutokea.
Aina za Ugonjwa wa Kisukari.
Kuna aina kuu mbili za kisukari;
Aina hii ya kisukari hutokana na kongosho kushindwa kuzalisha homoni ya insulini ya kutosha mwilini, matokeo yake ni glukozi kuongezeka na ugonjwa wa kisukari kutokea. Aina hii ya kisukari hutokea hasa kwa watu wenye umri mdogo hasa chini ya miaka.
Kisukari aina ya pili hutokea kutokana na mwili kushindwa kuitumia insulini iliyozalishwa hali iitwayo insulin resistance na hivyo kusababisha glukozi kwenye damu kuongezeka na ugonjwa wa kisukari kutokea.
Dalili za Ugonjwa wa Kisukari
Ugonjwa wa kisukari huweza kuleta dalili zifuatazo;
  • Kiu kali ya maji
  • Kukojoa mara kwa mara
  • Hamu ya kula kuongezeka
  • Mwili kuchoka
Kujua Kama Una Kisukari
Tafiti zinaonesha kuna kiasi kikubwa cha watu wenye ugonjwa wa kisukari ambao hawana dalili hivyo ni muhimu kufanya vipimo ili kuweza kujua. Mara nyingi vipimo vifuatavyo hupimwa;
  • Random Blood Glucose.
.Hupima kiasi cha sukari ya glukozi kwenye damu kwa mtu ambaye amekula chini ya masaa 8 yaliyopita. Kiasi cha glukozi kikizidi 11.0mmol/dl zaidi ya mara mbili au mara moja na dalili basi mtu huyo ana kisukari.
  • Fasting Blood Glucose
Kipimo hiki hupima kiasi cha sukari kwenye damu kwa mtu ambae amekula si chini ya masaa 8 yaliyopita. Kiasi cha sukari kikizidi 7.0mmol/dl zaidi ya mara mbili au mara moja na dalili basi kuna ugonjwa wa kisukari.
Matibabu
Matibabu ya ugonjwa wa kisukari hujumuisha mabadiliko katika mtindo wa maisha, lishe na dawa. Njia hizi zote hunuia mgonjwa awe na kiwango cha sukari cha kawaida na kuzuia madhara ya kisukari kwenye mwili wake.
Mabadiliko Katika Mtindo wa Maisha
Kisukari hasa aina ya pili hutokea kwa kiasi kikubwa kikichangiwa na mtindo wa maisha. Hivyo ni muhimu kufanya mabadiliko katika mtindo wa maisha kwani kwa kiasi kikubwa husaidia  kudhibiti kiasi cha sukari katika damu. Mabadiliko haya ni;
  • Ufanyaji wa mazoezi
  • Kuacha/kupunguza unywaji wa pombe
  • Kuacha uvutaji sigara
Mabadiliko Katika Lishe
Ni sehemu muhimu sana katika matibabu ya kisukari. Kwa baadhi ya wagonjwa, mabadiliko katika mtindo wa maisha na lishe ni tiba tosha ya ugonjwa wa kisukari na kwa wengine husaidia kupunguza kiasi cha dawa na kuzuia madhara ya kisukari.
Ni muhimu kufanya mabadiliko kwa mgonjwa mwenye kisukari, kwa ujumla kwa kupunguza kiasi cha wanga kwenye mlo,kutumia nafaka zisizokobolewa na kuongeza matunda na mboga za majani kwenye mlo.
Dawa za Kisukari
Matibabu ya kisukari kwa dawa huanza kama kiasi cha glukozi kwenye damu kimeshindwa kudhibitiwa na mabadiliko katika mtindo wa maisha na lishe peke yake. Pamoja na kutumia dawa ni muhimu kuzingatia mabadiliko katika matindo wa maisha na lishe, la sivyo madhara ya kisukari yatajitokeza mapema. Kuna aina mbili ya matibabu ya dawa, nazo ni;
Sindano za Insulini
Insulini hutumika kutibu kisuakri aina ya kwanza (type 1 diabetes), kutokana na upungu wa insulini mwilini. Insulini hutolewa kwa njia ya sindano, huchomwa chini ya ngozi(subcutaneous) kwenye mapaja, mikono, tumbo au matako.
Athari (complication) moja kuu ya insulini ni glukozi kushuka zaidi ya kawaida (hypoglycemia) ambayo ni hatari wakati mwingine. Athari nyingine ni kunenepa na kuvimba sehemu za kuchoma sindano.
Dawa za kupunguza sukari.
Dawa hizi hutumika kwa watu wenye kisukari aina ya 2 (type 2 diabetes), hufanya kazi ya kupunguza kiwango cha glukozi kwenye damu kwa kupunguza unyonywaji wa glukozi kutoka kwenye utumbo, kuongeza uzalishwaji wa insulini na kuziwezesha seli za mwili kutumia glukozi.
Kuna makundi mbalimbali ya hizi dawa, ambazo zinatumika mara kwa mara hapa nchini ni metformin na Glibenclamide.
Madhara ya Kisukari
Ugonjwa wa kisukari hasa usiotibiwa una hatari kubwa ya kuathiri tishu na viungo mbalimbali vya mwili. Sukari inayozidi kwenye damu huharibu mishipa ya fahamu, damu na kudhoofisha mfumo wa kinga ya mwili, ambayo matokeo yake ni;
  • Mtoto wa jicho (cataract) ambayo husababisha macho kutoona vizuri na hatimaye upofu.
  • Figo kushindwa kufanya kazi (renal failure).
  • Mishipa  ya fahamu kutofanya kazi na misuli kukosa nguvu (peripheral neuropathy).
  • Shinikizo la damu la kushuka (hypotension).
  • Kidonda mguuni (diabetic foot).



KUISHI VIZURI NA UGONJWA WA KISUKARI

Kuishi Vizuri Na Ugonjwa wa Kisukari

Kuishi vyema na ugonjwa wa kisukari kunaweza kuonekana ni changamoto kubwa hasa ukizingatia ugonjwa huu hauna tiba mpaka sasa. Ingawa hauna tiba, ugonjwa wa kisukari unaweza kudhinitiwa. Unaweza kuishi vizuri kabisa ukiwa na ugonjwa huu.
Ni muhimu kuwe na uwiano mzuri kati ya kiasi cha chakula unachokula, mazoezi na dawa za sukari ii kudhibiti kiasi cha sukari kwenye damu. Hii itakusaidia kupunguza matatizo yanayotokana na kisukari.
Kuwa na ugonjwa wa kisukari itakulazimu ubadili mambo kadhaa juu ya mtindo wako wa maisha.


Kuna aina mbili za ugonjwa wa kisukari:
  • Kisukari aina ya kwanza (type I diabetes
  • Kisukari aina ya pili (type 2 diabetes). 
Aina ya kwanza hujitokeza hasa katika umri mdogo zaidi ukilinganisha na aina ya pili.
Sio kosa lako kupata ugonjwa wa kisukari, lakini ni jumuku lako kujitunza.
Namna Kisukari Kinavyojitokeza

Unapokula chakula cha wanga kama ugali, wali au mihogo mwili humeng’enya na kuuvunja wanga kuwa aina ya sukari iitwayo glukozi (glucose). Glukozi huupa mwili nguvu ya kufanya kazi, ili mwili uweze kuitumia glukozi huitaji kichochezi kiitwacho insulini (insulin). Insulini hutengenezwa na ogani iitwayo kongosho (pancreas).
Unapokuwa na kisukari aina ya pili, mwili wako hushindwa kutengeneza insulini ya kutosha au hushindwa kuitumia vizuri. Kisukari aina ya kwanza mwili hushindwa kutengeneza insulini ya kutosha.
Kwa sababu seli za mwili zinashindwa kutumia glukozi iliyo kwenye damu kwa ajili ya kutengeneza nishati, glukozi hukusanyika kwenye damu na kusababisha ugonjwa wa kisukari.
Kuishi Vyema Na Kisukari


Mambo muhimu ya kuzingatia ni;
  • Kuchagua aina na kiasi cha chakula cha kula kila siku
  • Kufanya mazoezi na viungo
  • Kutumia dawa za kupunguza sukari kama umeanzishiwa na daktari wako
  • Kupima kiasi cha sukari mara kwa mara
  • Kuhudhuria Kkini ki ya kisukari
  • Kujifunza zaidi juu ya kisukari
  • Kuutunza mwili wako vizuri
Kuchagua aina na kiasi cha chakula cha kula kila siku

Kipindi cha nyuma, mlo kwa watu wenye kisukari ilikuwa ni tatizo. Katika mlo wako zingatia yafuatayo; 
  • Pata aina tofauti za vyakula ikijumuisha mbona za majani, nafaka zisizokobolewa, maziwa na bidhaa za maziwa na mafuta.
  • Usile chakula kingi sana na usiache kula chakula
  • Usile chakula cha aina moja peke yake
  • Pata mlo kila baada ya muda unaofanana
  • Panga aina ya vyakula na kiasi cha mlo wako
Kupangilia Kiasi Cha Mlo Wako

  • Katika sahani yako ya chakula chora mstari mmoja katikati kugawanya katika sehemu mbili, kisha gawanya sehemu moja katikati tena kupata sehemu tatu kama mchoro hapo chini unavyoonesha. 
    Mlo Wa Chakula
    Mpangilio Wa mlo
  • Weka sehemu kubwa ya sahani mboga za majani kama spinachi, karoti, majani ya kunde, kabichi, nyanya, uyoga, matango n.k.
  • Sehemu nyingine ndogo weka vyakula vya nafaka na wanga kama oats, ugali wa dona, mchele usiokobolewa, maharagwe, kunde, njegere, mahindi, viazi ulaya, viazi vitamu na ndizi za kupikwa.
  • Sehemu ndogo iliyobaki weka vyakula vya protini kama kuku, samaki, mayai, vyakula vya baharini kama kaa, ngisi, pweza, nyama ya ng’ombe au mbuzi isiyo na mafuta. 
  • Usisahau matunda katika mlo wako.
  • Tumia mafuta ya mimea kama alizeti, pamba au zeituni katika mapishi yako.
  • Kunywa maji  si chini ya glasi 10 kwa siku.
Kufanya Mazoezi
Kufanya mazoezi ni sehemu muhimu ya kudhibiti ugonjwa wa kisukari. Mazoezi husaidia kupunguza kiasi cha glukozi kilichipo kwenye damu. Tenga angalau dakika 30 za mazoezi kila siku.
Unaweza kufanya mazoezi yafuatayo:
  • kutembea, kukimbia
  • kuendesha baiskeli au kuogelea
Kupungua Uzito


Kupunguza uzito wa mwili husaidia kudhibiti glukozi, kupunguza presha na lehemu kwenye mwili. Sahani ya mlo hapo juu pamoja na ufanyaji wa mazoezi vitakusaidia kupunguza uzito wa mwili.
Kutumia Dawa za Kisukari


Zipo dawa za aina mbalimbali kwa ajili ya ugonjwa wa kisukari. Dawa hizi ni:
  • Sindano za Insulini
  • Vidonge vya kupunguza glukozi kwenye damu
Kumbuka dawa zitafanya kazi vizuri zaidi kama ukifanya mbadiliko kwenye lishe na mazoezi.
Kupima Sukari


Ni muhimu kupima kiwango cha glukozi kwenye damu ili kujua kama sukari imedhibitiwa au la. Wakati mzuri wa kupima ni kabla ya mlo au masaa mawili baada ya mlo.
Utashauriana na daktari wako mara ngapi utakuwa unapima na viwango vya glukozi vinavyotakiwa.
Kuutunza Mwili Wako


Ugonjwa wa kisukari huathiri mfumo wa kinga mwilini, hivyo kusababisha uponaji wa vidonda kuchelewa. Pia mfumo wa fahamu unaweza kuathiriwa kusababisha usipate maumivu unapoumia.
Mwili huwa na hatari ya kupata vidonda visivyopona hasa kwenye miguu. Hivyo ni muhimu kutunza na kukagua sehemu zako za mwili ikiwemo miguu na vidole mara kwa mara.
Pia kuwa makini na maambukizi ya fangasi kwenye vidole. Hakikisha miguu yako inakuwa laini kwa kupaka mafuta, ikaushe vizuri kila baada ya kuoga.
Ikiwa unapata vidonda au maambukizi, onana na daktari mapema kwa ajili ya matibabu.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!