WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania ina mpango wa kujenga njia ya umeme kutoka Mbeya hadi Zambia kupitia Tunduma ili kupunguza tatizo la umeme linaloikabili nchi hiyo.
“Serikali ya Tanzania inajenga njia ya umeme ya msongo wa KV 400 kutoka Iringa – Dodoma – Singida – Shinyanga ambayo ni sehemu ya mradi mkubwa wa umeme unaolenga kuunganisha Zambia, Tanzania na Kenya,” amesema.
Amesema upembuzi yakinifu kwa ajili KV400 kutoka Iringa hadi Mbeya umekwishakamilika tangu mwaka 2012, na hivi sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili kuunganisha kipande cha kutoka Mbeya na gridi ya Taifa ya Zambia.
Waziri Mkuu ambaye anahudhuria mkutano huo kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli, ametoa ufafanuzi huo leo mchana (Jumanne, Mei 24, 2016) wakati akichangia hoja kwenye mjadala wa wakuu wa nchi na Serikali uliohusu Nishati na Mabadiliko ya TabiaNchi kwenye ukumbi wa mikutano cha kimataifa wa Mulungushi.
Amesema ili kukabiliana na changamoto ya nishati barani Afrika, nchi za bara hili zinahitaji kuwa na fedha ama mitaji, teknolojia ya kisasa na wataalamu wenye ujuzi wa kutosha jambo ambalo amesema ni gumu kulikamilisha kila nchi peke yake.
Amesema ili kukaribisha wawekezaji kwenye sekta ya umeme, Tanzania inafanyia marekebisho sheria zake ili kuruhusu uwekezaji kwenye sekta hiyo.
No comments:
Post a Comment