MALIKIA Elizabeth wa Uingereza amemtunuku mjumbe wa Jumuiya ya Ahamadiyya, Dk. Iftikhar Ahmad Ayaz, tuzo ya heshima ya KBE kutokana na mchango wake mkubwa wa kuhamasisha amani na kusaidia jamii.



Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, kufuatia kutunukiwa tuzo hiyo, Dk. Iftikhar Ahmad Ayaz, amepanda daraja kutoka OBE na kuwa KBE (Hababi) katika jumuiya hiyo.
“Kama mtu wa heshima, Dk. Iftikhar Ayaz, anaitwa kwa heshima Hababi (Sir). Hivyo, kuanzia sasa atakuwa Hababi Iftikhar Ahmad Ayaz, KBE, OBE,” ilisema taarifa hiyo.
Iftikhar Ayaz alikuja Tanzania wakati huo Tanganyika akitokea Qadian, India mwaka 1946 na aliishi na baba yake Tanga na kupata elimu ya sekondari mkoani humo kabla ya kujiunga na masomo ya ualimu Nairobi, Kenya na kuwa mtumishi wa serikali mwaka 1958.
Alifanya kazi kwenye Idara ya Elimu kama Naibu Mkaguzi wa shule za ‘English Medium’ na baadaye alifanya kazi kama Ofisa Elimu wa wilaya, jijini Dar es Salaam. mwaka 1963 na kasha kuhamishiwa mkoa wa Ziwa Magharibi (Bukoba) kama Mkaguzi wa Shule wa Mkoa.
Baadaye aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Jopo la Walimu wa Kiingereza. Alitumikia pia kama Mhadhiri Mwandamizi na Ofisa Mwandamizi wa Mtaala Chuo Kikuu Dar es Salaam.
Mwaka 1981, alijiunga na Chuo cha Maendeleo Jumuishi Vijijini kwa Afrika, kilichokuwa kimeanzishwa Arusha. Mwaka 1969 kwa maelekezo ya Hadrat Khalifatul Masih III, alikana uraia wa Uingereza na kuwa raia wa Tanzania.
Alipelekwa na Serikali ya Tanzania kusoma elimu ya juu Uingereza na baada ya kuhitimu masomo yake alitunukiwa Shahada ya Uzamili.
Baadaye alijiunga na Taasisi ya Jumuiya ya Madola na aliporudi Tanzania alianzisha Chama cha Jumuiya ya Madola Tanzania kilichokuza mshikamano na kufundisha shuleni juu ya jumuiya ya nchi huru zilizokuwa chini ya utawala wa Kiingereza.
Ayaz alikuwa mwanachama hai wa Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya Dar es Salam, Tanga, Morogoro na Bukoba na mwaka 1964 aliratibu Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya Mkoa wa Ziwa Magharibi na kuanzisha kituo cha Waahamadiyya Bukoba.
Alianzisha pia kituo cha Waahmadiyya Arusha na kutumikia Waahmadiyya Afrika Mashariki kwa njia nyingi, akijulikana serikalini kwa huduma zake kama Kamishna wa Mafunzo ya Skauti (wavulana), Katibu Mkuu wa Chama cha Jumuiya ya Madola Tanzania na mashirika mengine.