HIFADHI
ZA TAIFA TANZANIA
Mhifadhi Mwandamizi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Genes
Shayo (60) anashikiliwa na Kikosi Kazi Maalum cha kupambana na ujangili nchini
kufuatia taarifa za kuhusishwa kwake na upatikanaji wa jino la tembo wilayani
Arumeru mkoani Arusha.
Shirika la Hifadhi za Taifa kupitia taratibu za utendaji
kazi lilipokea taarifa za kintelijensia tarehe 14.05.2016 zikimhusisha mwananchi
mmoja mkazi wa Ngarenanyuki, Arumeru Emmanuel Nassari (46) ambaye ni Mchungaji
wa Kanisa TAG kumiliki jino la tembo na kuwa alihitaji kupata mtu wa kufanya
naye biashara. Baaada ya kupata taarifa hizi shirika liliwasiliana na Kikosi Kazi
Maalum cha Kitaifa kinachohusika na masuala ya ujangili ili kushirikiana kwa
ajili ya ufuatiliaji.
Kikosi Kazi hiki mara baada ya kupata taarifa hizi
kiliendelea na taratibu zake za kiuchunguzi na baada ya ufuatiliaji walifanikiwa
kumkamata Emmanuel Nassari tarehe 15.05.2016 akiwa na jino moja la tembo ambapo
katika mahojiano yaliyofanyika alimhusisha Mhifadhi Mwandamizi wa TANAPA Genes
Shayo kuwa anazo taarifa za yeye kuwa na jino hilo na hivyo kukamatwa tarehe
16.05.2016 kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Shirika la Hifadhi za Taifa linaendelea kutoa wito kwa raia
wema wa nchi hii kuendelea kutoa taarifa za kufichua vitendo vya ujangili na
kwamba halitasita kuchukua hatua stahiki kwa yeyote anayehusika na vitendo hivi
ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wake watakaobainika kisheria kuhusika na vitendo
hivi.
Imetolewa na Idara ya Mawasiliano
Hifadhi za Taifa Tanzania
S.L.P 3134
ARUSHA
Simu: +255 027 254 4082
Baruapepe: dg@tanzaniapaks.go.tz
Wavuti: www.tanzaniaparks.go.tz
23.05.2016
No comments:
Post a Comment