Tuesday, 19 April 2016

WABUNGE WOTE KUCHUKULIWA ALAMA ZA VIDOLE

BUNGE linaanza rasmi usajili wa wabunge na watumishi wa Bunge hilo pamoja na wageni mbalimbali, wanaoingia bungeni kwa kutumia mfumo wa kisasa wa kuchukua alama za vidole.


Sambamba na mfumo huo, Bunge pia limetoa taarifa rasmi ya kudhibiti urushaji wa matangazo ya Bunge ambayo sasa vyombo vya habari vya kielektroniki havitaruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi wa mbunge na kamera kwa lengo la kurekodi yanayoendelea.
Na badala yake, jukumu la kurusha matangazo ya vikao vya Bunge litafanywa na Bunge lenyewe kupitia Feed Maalum ili kurahisisha kila kituo cha redio na televisheni kupata matangazo hayo kwa sehemu walipo bila kufunga mitambo yao bungeni.
Hayo yalibainishwa jana na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah wakati akitoa taarifa kwa Naibu Spika wa Bunge hilo, Dk Tulia Ackson alipofanya ukaguzi wa ukarabati uliofanywa ndani ya Ukumbi wa Bunge linaloanza vikao vyake vya Bajeti katika Mkutano wa Tatu wa Bunge la 11 mjini hapa.
Dk Kashilillah alisema kuanzia jana wabunge wataanza usajili kwa njia ya kuchukuliwa alama za vidole badala ya utaratibu wa zamani wa kujisajili kwa kutumia makaratasi. Alisema usajili huo utachukua alama za vidole vyote 10 na lengo la kutumia mfumo huo ni kuboresha kanzi data ya Bunge na kwamba usaili huo utapunguza pia matumizi ya makaratasi ambayo yana gharama.
“Tumeanza usajili huo leo (jana) kwa wabunge waliofika, ila tutaendelea kusajili nadhani ndani ya wiki tutakuwa tumekamilisha kazi hiyo, na tumejipanga kuifanikisha kwa haraka,” alisema Dk Kashilillah.
Akizungumzia usajili huo, Dk Kashilillah alisema utasaidia kufahamu idadi ya wabunge waliohudhuria vikao vya bunge na hivyo itakuwa rahisi kwenye kazi ya upigaji kura wakati wa kupitisha hoja mbalimbali.
Alisema Bunge limeboreshwa na kuwa la kisasa zaidi ambapo kila meza ya mbunge ndani ya ukumbi huo, itakuwa na ‘tablet’ itakayomuwezesha kufuatilia majadiliano ya bunge hata ya siku zilizopita na pia wabunge wataweza kuona ratiba ya shughuli mbalimbali za Bunge.
Akizungumzia elimu kwa wabunge hao juu ya matumizi ya mfumo huo, Dk Kashilillah alisema wameandaa utaratibu wa kuwaelimisha wabunge hao juu ya matumizi ya mfumo huo, ili iwe rahisi kwao kuutumia.
Naye Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Bunge, Didas Wambura alisema wamejipanga vizuri kuhakikisha matangazo ya bunge yanapatikana kwenye vituo vya televisheni kama ilivyopangwa.
Wambura alisema kuanzia sasa Bunge litarusha matangazo ya Bunge lenyewe kupitia feed maalumu ili kurahisisha kila kituo cha televisheni na redio kupata matangazo hayo kwa sehemu walipo, bila kufunga mitambo yao bungeni.
“Tutarusha matangazo ya Bunge wenyewe tutatumia Feed Maalumu itakayorushwa na satelaiti ya INTELSAT 17,” alisema Wambura.
Kutokana na hatua hiyo, vituo vya televisheni na redio nchini havitaruhusiwa kuingiza kamera zao ndani ya Ukumbi wa Bunge kurekodi vikao hivyo na badala yake wanapaswa kutumia Masafa ya Matangazo ya Bunge.
Katika mabadiliko hayo, pia idadi ya viti vipya 94 vimefungwa ndani ya Ukumbi wa Bunge hilo na hivyo kufanya idadi ya vitu vyote vya ukumbi kuwa 404.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bunge, Owen Mwandumbya alisema watakaa na wadau wote wa habari ili kuona ni namna gani wataweza kupata matangazo hayo.
“Haturuhusu wapicha picha za televisheni na redio kuingia na kamera ndani ya Ukumbi wa Bunge kurekodi, kazi hiyo itafanywa na Bunge, ila waandishi wa habari wa magazeti na wapigapicha za mnato wataendelea kuingia,” alisisitiza Mwandumbya

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!