Friday, 8 April 2016

UFUNGAJI WA VIFAA VYA ULINZI BANDARI DAR KUKAMILIKA MWEZI HUU

Kazi ya ufungaji wa vifaa vya ulinzi zikiwamo kamera za kisasa (CCTV)  kudhibiti vitendo vya wizi katika Bandari ya Dar es Salaam, inatarajiwa kukamilika  mwishoni mwa mwezi huu.
 
Kamera hizo zinafungwa kila kona ya bandari hiyo, ikiwamo katika mageti kunakopita magari ya kutolea mizigo na sehemu nyingine muhimu.
 
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari ambao walitembelea bandari hiyo mwishoni mwa wiki kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa bandarini hapo, Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi wa Mamlaka ya  Usimamizi wa Bandari (TPA), Lazaro Twange, alisema mpaka  sasa kamera 240 zimeshafungwa na wanatarajiwa kufunga 450 mpaka kumalizika kwa mradi huo.
 
Alisema mradi huo utagharimu dola za Marekani milioni 6.5 sawa na Sh. bilioni 14.24 na kwamba  vifaa vingine vya ulinzi vinavyofungwa katika bandari hiyo vina uwezo wa kubaini vitu vya mionzi vinavyopitishwa bandarini.
 
Twange alisema kamera hizo zitakuwa zinafanya kazi saa 24 na zitakuwa zikinasa  matukio yote na mengine kurekodiwa.
 
“Mradi huu ni mkubwa sana na kamera hizi zina uwezo mkubwa wa kunasa kila tukio, ni nyingi na si rahisi kuona kila sehemu wakati mmoja, hivyo matukio yote yatakuwa yanarekodiwa na kwa vifaa hivyo vya ulinzi tulivyofunga yeyote atakayejaribu kuiba lazima abainike,” alisema.
 
 “Tunayo sehemu maalum ya kuhifadhi matukio yanayorekodiwa kila siku na tutakuwa tunayapitia kila  mara. Hivi sasa wanakamilisha ufungaji wa vifaa hivyo katika geti namba tano na uwapo wa kamera katika bandari kila mtu anafahamu isipokuwa hakuna anayefahamu inachukua sehemu gani, tukio gani na wakati gani,” alisema.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!