Friday, 8 April 2016

KEMIKALI BILA TAHADHARI, NI HATARI KWA AFYA NA MAZINGIRA


Kijana huyu alikuwa miongoni mwa vijana 12 waliounguzwa na kemikali, baada ya kubeba magunia yanayodhaniwa kuwa na vitu vyenye kemikali huko Handeni mkoani Tanga




BIDHAA nyingi zinazotumika kwa mahitaji ya kila siku zinatengenezwa viwandani kwa kutumia kemikali.
Kemikali hizo zipo katika vyakula, dawa, vinywaji, na hata kwenye nguo. Kemikali zina faida kwa mwanadamu lakini pia zina madhara makubwa kwa afya na mazingira kama hazitatumika inavyostahili. Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele, alisema hayo mjini Morogoro wakati anafungua mafunzo ya wakuu wa usalama barabarani wa mikoa ya Tanzania Bara. Profesa Manyele anasema madhara ya kemikali yanaweza kujitokeza wakati wa uzalishaji , usafirishaji, uhifadhi na matumizi.
“Katika hali ya kawaida madhara ya kemikali kwa afya na mazingira wakati mwingine hayawezi kudhihirika moja kwa moja. Ukweli unabaki pale pale kuwa athari kwa afya na mazingira zipo ingawa zinaweza kuchukua muda mrefu kuonekana,“ anasema. Profesa Manyele anatoa mfano kuwa, ongezeko la magonjwa kama saratani wakati mwingine ni madhara yatokanayo na kemikali zilizotumika kwenye kilimo miaka ya nyuma.
Anasema, kwa mujibu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), inakadiriwa kuwa watu milioni 270 kati ya wafanyakazi bilioni 2.8 kote duniani wamekumbwa na ajali za kemikali maeneo ya kazi na wengine milioni 160 wanasumbuliwa na magonjwa yanayotokana na madhara ya matumizi ya kemikali kila mwaka. Kwa mujibu wa Profesa Manyele, kutokana na utafiti wa ILO, imeripotiwa kuwa watu milioni 125 duniani kote wako katika hatari ya kudhurika na kemikali aina ya asbesto.
Anasema, watu 90,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na madhara ya madini hayo. Profesa Manyele anasema , Tanzania si kisiwa na hivyo kemikali zilizoleta madhara makubwa katika nchi nyingine ni hizo hizo zinazotumika nchini. “Kwa mfano, tunavyo viwanda vinavyofanya urejeshaji wa betri za magari yaliyotumika kwa kuzalisha kemikali aina ya lead,” anasema Profesa Manyele.
Kadhalika anasema kuna utumiaji mkubwa wa kemikali aina ya Ammonium Nitrate kama mbolea ili kuongeza uzalishaji mashambani na kutengeneza milipuko ya kulipulia miamba wakati wa uchimbaji madini. Anaitaja kemikali aina ya Sodium Cyanide ambayo ni sumu kali lakini inatumika kwenye uchenguaji wa dhahabu sambamba na kemikali nyingine zenye madhara zinazotumika katika migodi, viwanda vya rangi na magodoro.
Mbali na madhara ya kemikali kumpata mwanadamu au mazingira baada ya kupita muda mrefu, lakini pia Profesa Manyele anasema, kuna ajali za kemikali nchini. Baadhi ya hizo zimesababisha magari ya mafuta kupata ajali, kuwaka moto na kuua watu waliokuwa wanajihusisha na uchotaji wa matufa wakati wa ajali. Anasema, kuna ajali viwandani zilizohusisha kemikali na kusababisha madhara kwa afya na mazingira.
Kwa mujibu wa Profesa Manyele, utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani Namba 3 ya mwaka 2003 umesaidia kutambua mapema aina ya kemikali zinazoingia nchini, mahali zinapokwenda na matumizi yake. Anasema, sheria hiyo imepunguza matukio ya ajali zinazotokana na kemikali wakati wa matumizi, usafirishaji au uhifadhi usio salama.
Profesa Manyele anasema, mafunzo kwa wakuu wa usalama barabarani wa mikoa ya Tanzania Bara kuhusu namna ya kuitekeleza sheria hiyo yatasaidia udhibiti wa kemikeli hizo. Anasema, lengo la mafunzo hayo ni pamoja na kujenga uelewa ili kuhakikisha kuna usafirishaji salama wa kemikali, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Kemikali za Viwandani na Majumbani ya mwaka 2003, sura ya 182 na kanuni zake za mwaka 2015.
Profesa Manyele anasema, kabla ya kutungwa na kuanza utekelezaji wa sheria hiyo, kemikali zilikuwa zinaingia nchini kiholela na kutumika bila kuwa na ufuatiliaji. Anawataka wakuu wa usalama barabarani kusimamia matakwa ya sheria na kanuni zake katika maeneo yao kuhakikisha kuwa madereva wote wanaosafirisha kemikali wamepitia mafunzo ya usafirishaji salama wa kemikali na kupewa cheti na Mkemia Mkuu wa Serikali.
Amekitaka kikosi cha usalama barabarani nchini kufanya ukaguzi wa madereva wa magari ya mizigo wanaosafirisha kemikali ili kubaini iwapo wana vyeti vya mafunzo maalumu ya usafirishaji salama wa kemikali kutoka Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali. “Sasa ni wakati wa kikosi cha usalama barabarani kukagua pia vyeti maalumu zinazotolewa kwa madereva wa magari ya usafirishaji wa mizigo ya kemikali vinavyotolewa na madereva wasiokuwa navyo wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria ” anasema Profesa Manyele.
Anasema, wakuu wa usalama barabarani wa mikoa ya Tanzania Bara wana wajibu wa kuainisha maeneo ambayo ni hatarishi kwa ajali, kuegeshwa magari makubwa na mizani ili magari ya mizigo yenye kamikali yawe salama . “Maeneo ya uegeshaji wa magari ya mizigo kama Mikumi, Mikese, mizani pamoja na katika foleni ndefu ambazo zinachanganyika na magari ya abiria, tahadhari zichukuliwe mapema,” anasema Profesa Manyele.
Mwakilishi wa Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani nchini, Awadhi Haji, anasema mafunzo hayo yatawajengea weledi katika ukaguzi, kuchukua tahadhari na hatua za kudhibiti madhara yanayoweza kusababishwa na kemikali. Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha, Marison Mwakyoma, ameiomba ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kushirikiana na wadau wa elimu ili kuandaa mtaala maalumu wa somo hilo katika vyuo vya madereva ili lifundishwe sanjari na masomo mengine.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!