(Nimonia), ni aina ya maambukizi yanayoathiri mapafu.
Inakadiriwa kwamba watoto karibu milioni 1.6 walio chini ya miaka 5 maisha yao hupotea kila mwaka kutokana na ugonjwa huu.
Kuna aina kadhaa ya vimelea ambavyo vinaweza kusababisha maambukizi katika mapafu. Vimelea hivi hujumuisha bakteria, virusi, parasaiti na fangasi.
Vimelea hivi hushambulia mwili wa binadamu kulingana na umri na kinga ya mwili wake. Kwa mfano, bakteria wanaosababisha homa ya mapafu kwa watoto wachanga ni tofauti na wale wanaosababisha ugonjwa huo kwa watoto wakubwa.
Baadhi ya vimelea wa bakteria wanaoshambulia watoto ni pamoja na Streptococcus Pneumonia, ambao ni aina ya bakteria wanaoongoza kusababisha homa ya mapafu kwa watoto. Wapo pia Haemophilus Influenzae aina ya kundi B (Hib), ambao ni aina ya pili ya bakteria walio maarufu zaidi kwa kusababisha ugonjwa wa homa ya mapafu kwa watoto.
Staphylococcus Aureus ni aina nyingine ya bakteria ambao hushambulia zaidi watoto wachanga. Kwa upande wa virusi, aina ya Respiratory Syncytial virus ndiyo wanaoongoza kwa kusababisha homa ya mapafu kwa watoto.
Aidha, vimelea wa Pneumocystis Jiroveci ambao kwa sasa huwekwa kwenye kundi la parasaiti ni maarufu zaidi miongoni mwa parasaiti wanaosababisha homa ya mapafu kwa watoto wenye upungufu wa kinga mwilini hususan watoto wenye virusi vya Ukimwi. Aina nyingine za bakteria ambao hushambulia zaidi watoto wakubwa ni pamoja na Mycoplasma Pneumonia na Chlamydia Pneumonia.
Kuna namna nyingi za kuenea kwa ugonjwa huo. Kwa kawaida, virusi na bakteria hupatikana katika sehemu ya juu ya mfumo wa njia ya upumuaji yaani Upper Respiratory Tract. Inapotokea kinga ya mwili ya mtoto imeshuka kwa sababu yoyote ile, vimelea hivi huweza kusambaa na kufika mpaka sehemu ya chini ya mfumo wa njia ya upumuaji yaani Lower Respiratory Tract na hatimaye kushambulia mapafu.
Hali kadhalika, vimelea hawa wanaweza kuenea kwa njia ya damu kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kabla ya kuzaliwa yaani kipindi cha mimba.
Dalili za ugonjwa wa homa ya mapafu
hutegemea umri wa mtoto. Kwa watoto wadogo, dalili za awali zinaweza kuwa homa kali pamoja na mtoto kuhangaika na kunyong’onyea. Watoto wanaozaliwa wakiwa na maambukizo ya bakteria aina ya Streptococcus kundi B wanaweza kuwa na homa na kupumua kwa shida.
Wakati mwingine mtoto anaweza kuwa na dalili ambazo si maalumu kama vile kuhangaika na kushindwa kunyonya au kula vizuri bila kuwa na dalili yoyote ya kushindwa kupumua. Hali hii inaweza kutokea kwa mtoto wa umri wowote ule.
Dalili za kawaida za homa ya mapafu ambazo huwapata karibu watoto wote wanaoathirika na ugonjwa huu ni pamoja na kuwa na homa, kuhisi baridi na kikohozi. Kupumua kwa haraka kuliko kawaida na kutoa sauti isiyo ya kawaida wakati wa kupumua.
Dalili nyingine ni mbavu za mtoto kuingia ndani wakati wa kupumua na pia maumivu ya tumbo.
kutokuwa na hamu ya kucheza na kupoteza hamu ya kula na kushindwa kunyonya. Pia mtoto hubadilika rangi na kuwa na rangi bluu katika midomo na kucha. Hata hivyo, si lazima dalili zote hizi ziwepo kwa kila mtoto.
Baadhi ya watoto huonesha kupumua kwa haraka kama dalili pekee ya homa ya mapafu. Iwapo vimelea vimeshambulia sehemu za chini ya mapafu karibu ya tumbo, sehemu ijulikanayo kama kiwambo au diaphragm, mtoto anaweza asioneshe hali yeyote ya kushindwa kupumua ingawa anaweza kuwa na homa na kuhisi maumivu makali ya tumbo, vichomi na pia kutapika. Watoto wachanga wanaweza kushindwa kunyonya, na pia kupoteza fahamu na kupata degedege.
Katika hali ya kawaida kinga ya mtoto mwenye afya njema humlinda asishambuliwe na vimelea vinavyosababisha magonjwa mbalimbali. Hali huwa ni tofauti pale kinga ya mtoto inapokuwa ndogo au dhaifu, kwa vile mfumo mzima wa ulinzi huathirika na hivyo basi kuwa rahisi kwa mtoto kupata homa ya mapafu.
Mfumo wa kinga ya mtoto unaweza kuwa dhaifu kwa ukosefu wa lishe bora hasa kwa watoto wachanga ambao hawanyonyeshwi maziwa ya mama ipasavyo. Aidha uwepo wa magonjwa mengine, kwa mfano maambukizi ya virusi vya Ukimwi VVU, saratani na ugonjwa wa surua hupelekea kinga ya mwili kuwa dhaifu.
Lakini vile vile kuna mazingira yanayoweza kusababisha mtoto kuwa katika hatari ya kupata homa ya mapafu, mfano moshi wa sigara au moshi ndani ya nyumba unaosababishwa na kupikia kuni au mkaa. Pia msongamano ndani ya nyumba kutokana na watu kuwa wengi sehemu moja nayo huweza kusababisha watoto kupata homa ya mapafu.
Uchunguzi, vipimo na matibabu ya Pnemonia
Kwa kawaida daktari humchunguza mtoto mgonjwa kwa kusikiliza dalili za ugonjwa kutoka kwa mzazi au mlezi wa mtoto na pia huchunguza viashiria vya ugonjwa huu na kisha kumpima mtoto kwa kutumia kifaa kinachosaidia kusikia sauti mbalimbali katika mfumo wa hewa wa mgonjwa kinachoitwa stethoscope.
Ili kuwa na uhakika kwamba mgonjwa ana homa ya pneumonia, vipimo vifuatavyo vinaweza kufanywa kulingana na mazingira na upatikanaji wake. Vipimo hivyo ni pamoja na X-ray ya kifua, au CT-scan ya kifua, pamoja na damu ili kuchunguza madhara yaliyoletwa na homa hii ya mapafu. Faida ya kipimo cha CT-scan ni uwezo wake wa kutofautisha aina tofauti za homa ya mapafu na aina ijulikanayo kama Atypical pneumonia ambayo si rahisi kuonekana kwa kutumia X-ray ya kawaida ya kifua. X-ray ya kifua na CT-scan ya kifua kwa pamoja vina uwezo wa kuonesha tatizo hata pale ambapo daktari ameshindwa kusikia sauti maalumu kwa kutumia kifaa chake cha stethoscope.
Maamuzi ya matibabu kwa watoto wenye homa ya mapafu hutegemea aina ya vimelea, umri na hali ya mtoto. Mara nyingi dawa za antibiotics ndizo hutumika katika kutibu homa ya mapafu inayosababishwa na maambukizi ya bakteria. Kwa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi, dawa za antibiotics hazina uwezo wowote wa kutibu.
Kumbuka antibiotics hazina uwezo wowote wa kutibu homa inayosababishwa na virusi hivyo hupona kwa kutumia tu dawa za kushusha homa, lishe, mazingira yenye hewa safi. na kumpa mtoto maji mengi. Ieleweke kuwa ni tabibu anayeweza kufahamu kama mtoto wako anahitaji antibiotics au dawa za aina nyingine, kwahiyo ni muhimu kwa mzazi ama mlezi kumpeleka mtoto hospitalini haraka pindi mtoto anapoonesha dalili za ugonjwa huu badala ya kuamua kumpa dawa bila kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.
No comments:
Post a Comment