Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara kutoka Jamhuri ya Czech, Zdenek Adamec akiweka sahihi kwenye kitabu cha wageni Ofisini kwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (Hayupo pichani).
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani akizungumza katika kikao chake na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Czech, Zdenek Adamec (Hayupo pichani) kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (mwenye tai nyekundu), akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara kutoka Jamhuri ya Czech, Zdenek Adamec (Kushoto kwake), Meneja Mradi wa Czech nchini, Dkt. Mturi Arnold (mwenye suti ya kahawia) wakiwa kwenye picha ya pamoja na watendaji wa wizara.
……………………………………………………………………………………
Na Devota Myombe
Imeelezwa kuwa Serikali ya Jamhuri ya Czech inaendelea na juhudi za kuimarisha uhusiano na Serikali ya Tanzania hususan kupitia uwekezaji.
Hayo yalielezwa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara kutoka Jamhuri hiyo ya Czech, Zdenek Adamec ambaye aliongozana na Ujumbe kutoka Czech ambao ulitembelea Wizara ya Nishati na Madini na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani.
Adameck alisema Jamhuri ya Czech imedhamiria kurudisha uhusiano baina yao na Serikali ya Tanzania ambao aliuelezea kwamba kwa muda mrefu ulikuwa umedorora.
Aliongeza kwamba wamevutiwa na maendeleo ya uchumi wa Tanzania hivyo wako tayari kuwekeza, “Tumevutiwa kuwekeza Tanzania na tuko tayari kuwekeza na nadhani huu ndo muda mwafaka.”
Naye Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Sera ya Uchumi wa Mambo ya Nje kutoka Czech, Mhandisi Petr Kulovany alisema wameamua kujenga upya uhusiano wao na Tanzania ambao kwa muda mrefu ulikuwa umedorora na kueleza dhamira ya Serikali yao ya kuwekeza katika Sekta ya Nishati na Elimu.
“Tunataka tuendeleze ushirikiano wetu na Tanzania na ushirikiano huu utajengwa kupitia uwekezaji maeneo mbalimbali kama vile uwekezaji kwenye nishati ya jua, gesi, ujenzi wa bomba la gesi, Mafunzo ya Teknolojia na Sayansi ya Habari pamoja na Mafunzo ya Uhandisi,” alisema Mhandisi Kulovany.
Kwa upande wake Dkt. Kalemani alisema fursa za uwekezaji nchini hususani kwenye Sekta ya Nishati na Madini zipo nyingi na kuongeza kwamba Tanzania bado inahitaji wawekezaji wengi kwa kuwa sehemu za kuwakeza bado ni nyingi.
Alisema Tanzania imekusudia kuwa na viwanda vingi na hivyo umeme mwingi unahitajika kwa ajili ya uendeshaji wa viwanda hivyo.
“Viwanda haviwezi kufanya kazi kama hakuna umeme; kwahiyo tumelenga kuzalisha umeme wa kutosha kutokana na vyanzo mbalimbali tulivyonavyo hapa nchini.”
Alitaja baadhi ya vyanzo hivyo kuwa ni, upepo, gesi asilia, jua, maji na makaa ya mawe na kueleza kuwa mpaka sasa mradi wa nishati ya upepo haujakamilika ambao unafanywa huko mkoani Singida na Makambako mkoani Njombe.
Dkt. Kalemani vilevile alimshukuru Naibu Waziri huyo kwa uamuzi wa kuendeleza uhusiano na Tanzania na kumsihi wafikirie kuwekeza katika sekta nyingine mbali na hizo walizokusudia.
“Ningependa kuwasihi muwekeze na sehemu nyingine pia kama kwenye madini na kilimo kwa kuwa tunazo maliasili nyingi na vilevile kwakuwa tumekusudia kuendeleza viwanda, ni muhimu kilimo pia kikaboreshwa,” alisema Dkt. Kalemani.
No comments:
Post a Comment