Tuesday 16 February 2016

MWANANYAMALA WATUMIA MAJI YA CHUPA CHUMBA CHA UPASUAJI



 
Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala inalazimika kununua maji ya chupa kwa ajili ya kusafisha vifaa vya upasuaji baada ya mashine mbili za kuchujia maji kuharibika.


Hayo yalisema jana na katibu wa afya wa hospitali hiyo, Willborada Athanas wakati akipokea mashine moja ya kuchujia maji iliyotolewa na kampuni ya Tanzania Water Equipment Supply Company( Twesco).
Alisema kwa kipindi cha miezi mitatu sasa, hospitali hiyo inalazimika kununua maji kwa ajili ya kusafishia vifaa vya upasuaji licha ya mashine moja kuuzwa Sh5.6 milioni. “Kila baada ya wiki mbili tunalazimika kununua lita 60 za majisafi ambazo ni sawa na Sh52,000 kwa ajili ya kusafishia vifaa,” alisema Athanas.
Alisema mashine ya kwanza iliharibika miezi sita iliyopita na mtaalamu alipopelekwa kwa ajili ya kutengeneza aligundua kuwa imeharibika na haifai kutengenezwa huku mashine ya pili ikiharibika miezi mitatu iliyopita na hivyo kusababisha changamoto kubwa katika kitengo cha upasuaji.
“Mashine ya pili imeharibika miezi mitatu iliyopita. Tukaandika barua wizarani na kwa wadau kuomba mashine ya kuchujia maji kwa sababu vifaa vya upasuaji vinatakiwa kusafishwa na majisafi na salama na siyo ya chumvi ili viendelee kuwa bora,” alisema.
Alisema licha ya hospitali hiyo kupandishwa hadhi na kuwa ya rufaa, bado mfumo wa majitaka haukidhi mahitaji.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Twesco, Victor Manyanga alisema mashine waliyokabidhi ina uwezo wa kusafisha lita 300 za maji kwa siku. “Tunatarajia kutoa mashine kama hii katika hospitali tatu za jiji hili ambazo ni Palestina, Amana na Temeke kwa kipindi cha miezi sita kuanzia sasa” alisema Manyanga.

MWANANCHI

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!