Tuesday 16 February 2016

MALI ZA MAOFISA WA TAKUKURU ZAANZA KUCHUKUZWA


Serikali imesema kesho itaanza upembuzi yakinifu wa tamko la mali za wafanyakazi wote wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kwamba watakaobainika kudanganya, watafukuzwa kazi na kuchukuliwa hatua za kisheria.
 
pia imesema Takukuru ina watendaji ‘majipu’ wengi, hivyo serikali itayatumbua, na haitaona shida kuwafukuza wote na kuajiri wafanyakazi wapya.
 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angela Kairuki, aliyasema hayo jana wakati akifungua mkutano wa kazi wa viongozi wa Takukuru.
 
Alisema serikali itafanya ukaguzi Takukuru katika idara zote zikiwamo Fedha, Uchunguzi na Ununuzi. 
 
Alisema wafanyakazi wa Takukuru wanapaswa kujitathmini upya umiliki wa mali zao, kabla kazi ya kuhakiki mali zao kuanza.
 
“Baada ya siku mbili serikali itaanza upembuzi yakinifu wa tamko la mali za wafanyakazi wote wa Takukuru. Watumishi wa Takukuru wana mali nyingi, hivyo serikali itafanya ukaguzi,” alisema Kairuki.
 
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlawola, alisema katika utekelezaji wa majukumu ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini kwa mwaka 2014/15 walipokea malalamiko 4,675 na kufanya uchunguzi na kukamilisha majalada 667.
 
Aliongeza kuwa Takukuru imepeleka majadala hayo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) majalada 278, na ilirejeshewa majalada 172 yakiwa na vibali vya kufungua mashtaka.
 
Alisema Takukuru pia imefungua kesi mpya 314 kote nchini na kushinda kesi 132 mahakamani na watuhumiwa walihukumiwa vifungo mbalimbali ikiwamo kulipa faini na kufanikiwa kuokoa Sh. bilioni saba zilizokuwa ziingie kwenye mifuko ya wabadhirifu wachache.
 
Mlowola alisema katika siku 100 za Rais Magufuli madarakani, Takukuru imeweza kupokea malalamiko 411 kutoka kwa wananchi, na kufungua mafaili 146 ya uchunguzi pamoja na kupokea mafaili 103 kwa DPP.
 
Alisema Takukuru ilirejeshewa majalada 65 yakiwa na kibali cha kufungua mashauri mahakamani kutoka kwa DPP, na kufungua kesi mpya 72.
 
Pia, alisema Takukuru imeshinda kesi 40 na kushindwa 52 pamoja na kuokoa Sh. bilioni 8.5 zilizokuwa ziingie kwenye mikono ya wabadhirifu.
 
Alisema Rais Magufuli wakati akifungua Bunge, aliahidi kuunda mahakama maalum ya walarushwa na mafisadi ili kuwashughulikia kwa uharaka zaidi na weledi, hivyo mchakato wa kulishughulikia agizo hilo umeshaanza na wako katika hatua nzuri ya kukamilisha azma hiyo ya Rais Magufuli.
 
Alisema kuundwa kwa mahakama hiyo, kutaimarisha mapambano dhidi ya rushwa na kutaongeza uharaka na kusikilizwa kwa mashauri ya rushwa na uhujumu uchumi wanayoyafungua kwenye mahakama mbalimbali nchini.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!