Sunday, 10 January 2016

Simulizi ya mama wa mtoto mlemavu imewaliza watu Geita

ULEMAVU wa midomo wazi maarufu kwa jina la Midomo ya sungura ‘’Hare lips’’ni moja ya ulemavu unadaiwa kuhusishwa na imani potofu za kishirikina.


Idadi kubwa ya watu wenye ulemavu wa mdomo hutengwa na jamii kwa imani kuwa ulemavu huo unatokana na kurogwa, mkosi na mara nyingine unahusishwa na kurithi laana jambo linalosababisha kushuka kwa hadhi ya wenye ulemavu huo. Siwema Ndelema, mama wa watoto sita, mkazi wa kijiji cha kata ya Kamena wilayani Geita, ni miongoni mwa wazazi wanaoshuhudia ukatili na mateso yanayowapata watoto wanaozaliwa wakiwa na Mdomo wa sungura.
Ndelema amewafanya watu waliokuwa wakimsikiliza watokwe na machozi pale alipoelezea kwa uchungu adha na taabu alizopata mwanawe aliyezaliwa akiwa na ulemavu wa mdomo. Akizungumza katika hafla ya kuwatakia safari njema walengwa zaidi ya 40 waliopelekwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa ajili ya upasuaji wa kurekebisha mdomo, Ndelema anasema baada ya kujifungu mtoto aliyepasuka mdomo jamii ilimtenga.
Simulizi ya Ndelema iliwahuzunisha viongozi waliohudhuria hafla hiyo ikiwa ni pamoja Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Omary Mangochie na wadau mbalimbali akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa mgodi wa dhahabu wa Geita wa GGM, Terry Mulpeter, ambaye kampuni yake imegharimia sehemu ya matibabu. Ndelema anasema hivi sasa ni miaka minne tangu alipoanza kuishi maisha ya kunyanyaswa, kubezwa na kutengwa na hata kususwa na jamii wakiwemo wanandugu baada ya kuzaa mtoto mlemavu wa mdomo.
“Wapo walionihukumu kwa madai kuwa mtoto huyo ni matokeo ya adhabu zangu. Pia wapo waliodai kuwa nimezaa mtoto mlemavu kama matokeo ya malipizi ya kisasi kwani hali hiyo inatokana na kurogwa au hasira za mizimu kwa mtu mwenye matendo maovu….nilibezwa badala ya kupewa faraja,” anasema Ndelema. Stela Senga ambaye ni mmoja wa waliofaidika na ufadhili wa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando kufanyiwa upasuaji na Timu ya Madaktari Bingwa watano kutoka nchini Australia, anasema aliomba ufadhili huo ili kumhudumia mjukuu wake aliyezaliwa na ulemavu wa mdomo.
Senga anasema mtoto huyo alinyooshewa vidole na kutafuta chanzo hadi ilipobainika kuwa katika ukoo wa mumewe shemeji yake ndiye aliyewahi kuzaliwa na ulemavu huo hivyo mtoto huyo inawezekana amerithi. Hata hivyo Marima Otieno Muuguzi wa Mgodi wa dhahabu wa Geita GGM anayewahudumia walengwa hao ili wakapatiwe matibabu katika Hospitali ya Bugando anasema kuwa ulemavu wa mdomo hauna uhusiano wowote na uchawi wala laana.
Anasema ulemavu huo unatokana na ukosefu wa madini joto na vitamini muhimu zinazohitajika katika ujenzi wa mwili wa mtoto wakati wa makuzi ya mimba. Amewataka wananchi kuachana na imani potofu kwa kuwa ugonjwa huo unatibika na baada ya upasuaji mtoto anakuwa katika hali ya kawaida. Uzoefu wa changamoto hii ndiyo uliousukuma mgodi wa dhahabu kupitia kitengo chake cha maendeleo ya jamii baada ya utafiti wake kuainisha utaratibu wa kuwatambua na kisha kuwapa ufadhili walengwa wanaoishi ndani na nje ya mkoa wa Geita kuwapatia matibabu ya ulemavu huo.
Ufadhili huo unajumuisha watoto na watu wazima kwa kuwa mtu yeyote mwenye ulemavu huo anapona endapo watapatiwa matibabu ya upasuaji. Watu wazima wenye ulemavu huo ambao hawakutaka majina yao yatajwe gazetini wanasema hawakubahatika kupata matibabu walipokuwa watoto jambo ambalo limesababisha wakose wachumba. Watu hao wenye umri kati ya miaka 35 hadi 45 wanadai hawakuwahi kubahatika kuoa wala kuolewa kutokana na kutengwa na jamii kutokana na hali yao ya ulemavu.
Meneja Uhusiano ya Jamii wa Mgodi huo Manase Ndoloma anasema mpango wa kuwafadhili watu wenye ulemavu wa midomo umeanza mwaka 2002 ambapo watu 1,200 walinufaika. Wastani wa gharama ya kila mlengwa unafikia zaidi ya Sh 650,000 kwa kumgharimia matibabu na huduma nyingine kwa mlengwa ikiwa ni pamoja na usafiri kutoka wanakoishi pamoja na kuwahudumia waisaidizi wanaowasindikiza.
Karibu Sh bilioni moja imetumika kufadhili mpango katika kipindi cha miaka 13 ambapo walengwa 1,200 kutoka ndani na nje ya mkoa wa Geita wamehudumiwa na kurejea katika hali zao za kawaida. Wagonjwa wanaofanyiwa tiba ya upasuaji wanarudi katika hali ya kawaida na kuanza maisha mapya yenye furaha na familia zao. “Lengo la Mgodi ni kuhakikisha mpango huo wa huhudumia walemavu wa midomo unakuwa endelevu, ’’anasema Ndoloma, Meneja wa Maendeleo ya Jamii wa mgodi huo.
Mganga Mkuu wa mgodi wa Geita, Kiva Mvungi, anasema kuwa wakati mradi huo unaanzishwa kulikuwa na changamoto nyingi kutokana na mwitikio mdogo wa wananchi ambao walidhani kuwa ulemavu hauwezi kutibiwa kwa sababu unasababishwa na kurogwa. Elimu ilianza kutolewa kwa kikundi cha kwanza kilichosafirishwa hadi Dar es Salaam katika hospitali ya CRTB kutibiwa na kufanyiwa upasuaji na madaktari Bingwa kutoka nchini Australia.
Watu waliofanyiwa upasuaji walitoa picha kamili kuhusu tiba ya mdomo wa sungura na kufungua mlango wa jamiii kuamini kuwa ulemavu huo unaisha kwa njia ya matibabu. “Baada ya kuona waliofanyiwa upasuaji na kupona ndipo wanaamini kuwa ina wezekana na kusambaza ujumbe kwa wengine wenye ulemavu huo,” anasema.
Daktari Mvungi anaongeza kuwa wanaelimisha jamii kuwa, chanzo cha ulemavu huo sio kurogwa, kurithi au adhabu inayotokana na kulipiza kisasi bali ni matatizo yanayoweza kupata jibu kupitia ufafanuzi wa kisayansi na kibaiolojia kuhusu tatizo linalompata mtoto wakati akiwa katika hatua za kukua katika tumbo la mama kabla ya kuzaliwa.
Ofisa katika Idara ya Maendeleo ya Jamii na Mawasiliano Susana Mwita, anasema kuwa ililazimika kuzungumza na walengwa na familia zao kuwashawishi wakubali kupatiwa tiba na kuwahakikishia kuwa watarudi salama. Anasema familia nyingi zinapenda tiba ila zinahofu kuwa huenda walengwa watapata matatizo au kufa wakati wa upasuaji hivyo kuwakataza au kuwashawishi walengwa wasikubali tiba.
Elimu imesaIdia walengwa na familia zao kuridhia walengwa kuchukuliwa kwenda kutibiwa katika Hospitali ya CCBRT iliyopo Dar es Salaam kabla ya tiba hiyo kuhamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando ili kuizogeza karibu na walengwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita, Terry Mulpeter anasema ni furaha na faraja kwake kuona sehemu ya faida ya mapato yanayoingizwa na mgodi huo kutokana na uwekezaji katika sekta ya uchimbaji dhahabu inanufaisha pia jamii ya watu wanaoishi katika eneo linalozunguka mgodi huo kwa kuwapatia huduma za kijamii matibabu ya upasuaji kurekebisha ulemavu wa mdomo.
‘’Ni sera yetu ya Anglogold Ashanti kuona sehemu yoyote duniani inakofanyia shughuli zake za uchimbaji …jamii inayoishi jirani na kuzunguka migodi yake inanufaika na ujio huo wakati uzalishaji ukiendelea,” anasema Mulpeter. Lakini pia kuwekeza katika sekta za kijamii ambazo baada hata ya shughuli za mgodi kukoma jamii itaendelea kunufaika na uwepo wa mgodi huo hata baada ya kukoma na ndicho kinachofanyika’’anadai Terry Mulpeter.
Huku akishuhudia mtoto ambaye miaka miwili iliyopita alikuwa ametengwa na jamii lakini sasa familia yake ilikuwa imeungana tena na jamii baada ya kufanyiwa upasuaji na kupona na kuwa katika hali ya kawaida na kuwashtua watu wengi katika kijiji anachoishi cha Andelema kupitia mama yake mzazi alimwambia Mulpeter kuwa mchango wenu umerejesha ndoa yetu kwa yenye furaha na jamaa zetu.
‘’Nawatakieni safari njema mara baada ya kukutana na hao madaktari Bingwa kutoka nchini Australia watakaowafanyia upasuaji wenu na muweze kurejea salama baada ya matibabu ya upasuaji alisema Terry Mulpeter.’’ Mulpeter amewaomba wakazi wanaozunguka mgodi huo kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo ili kuimarishwa usalama na kuchochea maendeleo ya wananchi wa eneo hilo. “Ningependa kuona Geita na wakazi wake wanakuwa miongoni mwa wanufaika wa uwepo wa midodi ya dhahabu katika eneo hili… sio kunufaisha mtu mmoja mmoja bali kupitia huduma za pamoja na vikundi ili kuleta maendeleo ya kweli,” anasema Mulpeter.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Manzie Omari Mangochie ameushukuru uongozi wa mgodi wa Geita kwa kusaidia watu wenye ulemavu kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Bugando. Amewataka wawekezaji wengine kuiga mfano wa GGM katika kusaidia huduma za kijamii. ‘’Haina maana GGM itachukua wajibu na jukumu la serikali katika kutimiza wajibu wake kwa jamii zikiwemo huduma za kijamii… lakini pia sehemu ya kujenga mahusiano mazuri na jamii inayozunguka Mgodi,” anasema Mangochie.
Amewataka wananchi kupuuza baadhi ya watu wanaodai kuwa Mgodi wa Geita haujafanya lolote katika kuchangia na kuboresha huduma za kijamii ikiwemo sekta za elimu, afya na maji na kusaidia vikundi vya ujasiriamali kwa kuwa uongozi wa mgodi huo unajitahidi kutimiza lengo la kusaidia wananchi wanaozunguka mgodi huo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!