WAUNGWANA wote nchini bila shaka wamefurahi kusikia kwamba meno ya Sheria ya Uhalifu wa Mitandao iliyopitishwa na Bunge mwaka huu yataanza kung’ata rasmi Septemba mosi, takribani siku 20 tu zijazo kuanzia leo.
Hii ni taarifa njema kwani pamoja na elimu ambayo imekuwa ikitolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) juu ya matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii na simu za mkononi, Tanzania bado inaongoza kwa kuwa na watu wengi wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii katika eneo hili la Afrika.
Kutokana na hali hiyo, taarifa za mitandao mingi imekuwa haiaminiki hadi nchi za nje kutokana na kujaa uzushi, uongo, uchochezi, lugha zenye ukakasi na picha za matusi.
Taarifa hii imekuja ikiwa ni masaa kadhaa kupita tangu watu wazushe kwamba Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal, alikuwa ana mpango wa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu msimamo wake ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakimaanisha kuhamia upinzani, jambo ambalo limekanushwa vikali na ofisi ya Makamu wa Rais.
Taarifa hizo za uzushi, zilisababisha watu wengi kuhangaika kutafuta ukweli na bila shaka zilimuumiza zaidi Makamu wa Rais.
Tunampa pole sana. Sheria hiyo ambayo tayari imeshasainiwa na Rais Jakaya Kikwete, inatoa adhabu kwa wahalifu wa mtandao pamoja na wasambazaji wa picha za uchi na ngono, wasambazaji wa taarifa za uongo, za kibaguzi na matusi na watu wengine wanaofanya udanganyifu unaohusu kompyuta.
Adhabu ni kwenda jela hadi miaka 10 au kulipa faini isiyopungua Sh milioni 50. Kwa upande wa kusambaza picha za ngono, matusi na uasherati, mhalifu atalipa faini isiyopungua Sh milioni 30 au kwenda jela miaka 10 au vyote. Lakini mtu atakayesambaza picha za uchi atalipa faini isiyopungua Sh milioni 20 au kwenda jela miaka saba au kutumikia adhabu zote kwa pamoja.
Kadhalika, mtu atakayetoa taarifa, takwimu au maelezo kwa njia ya picha, maandishi, alama au aina nyingine yoyote ikiwa ni ya uongo, akipatikana na hatia atalipa faini isiyopungua Sh milioni tatu au kutumikia kifungo jela kisichopungua miezi sita au vyote.
Tunakaribisha kwa mikono miwili kuanza kutumika kwa sheria hii kwa sababu inaonekana matumizi ya elimu pekee hayawezi kuwafanya watu kuacha tabia ya kutumia mitandao vibaya. Imani yetu ni kwamba kuna wanaofanya hivyo kwa makusudi na siyo kwamba hawajui kuwa wanalolifanya ni kosa.
Pamoja na hayo, tunashauri wakati sheria ikianza kung’ata, elimu iendelee kutolewa kwani bila shaka wataendelea kuwepo Watanzania wachache wanaoweza kutojua matumizi sahihi na yenye manufaa ya mitandao kama blogu, ukurasa wa facebook, whatsapp na kadhalika.
Tumefurahi kusikia TCRA ikisema kwamba inao uwezo wa kuwatambua na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wote wanaotumia vibaya mitandao hata kama watabadilisha kadi zao za simu mara 300 na kubadili majina.
Lakini kubwa tunalosisitiza ni usimamizi imara na madhubuti wa sheria hii ili kuzaa matunda yaliyokusudiwa na nchi yetu kuondokana na taarifa za uongo na uzushi na pia kuiepusha jamii yetu, hususan vijana wadogo na kutazama picha zenye ukakasi.
Kuwa na sheria ambayo haitasimamiwa vyema na kuzaa matunda yaliyokusudiwa, haitakuwa na maana yoyote na badala yake itakuwa ni hasara ya muda na rasilimali fedha zilizotumika hadi kupatikana kwa sheria hiyo.
No comments:
Post a Comment