
Watoto watano wa familia moja wamefariki dunia na mama yao mzazi kujeruhiwa vibaya, baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuteketea kwa moto wakati wamelala usiku.
Tukio hilo lilitokea Julai 6, mwaka huu, saa 3:00 usiku katika kitongoji cha Muleba kijiji cha Muleba kata ya Rwabwere Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera.
Inadaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni kibatari kilichokuwa kimewashwa kudondoka chini na moto kushika nyumba hiyo ambayo ilikuwa imejengwa kwa makuti ya migomba na kuteketea kwa moto.
Watoto waliokufa papo hapo kutokana na kuungua vibaya kwa moto ni Zaituni Mohamed (mwaka mmoja na miezi 3); Atwaibu Mohamed (4); Sajira Mohamed (3) na Shine Mohamed (7). Khadija Mohamed (5) alifariki dunia baada ya kufikishwa Hospitali Teule ya wilaya hiyo ya Nyakahanga kwa matibabu.
Mama mzazi wa watoto hao, Sania Mohamed (27), amejeruhiwa na kulazwa hospitalini hapo akiendelea kupata matibabu.
Akizungumza na NIPASHE katika wodi ya hospitali hiyo alikolazwa kwa matibabu, Sania alisema ameungua mwilini wakati akiwaokoa watoto wake.
Hata hivyo, alisema hakufanikiwa kuwaokoa watoto hao kutokana na moto kumzidi.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, Edson Salvatory, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwashauri wananchi kutumia taa zinazotumia mwanga wa jua (solar) au tochi za gharama nafuu ili kuepuka madhara yatokanayo na vibatari.
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Andrew Cesari, pia alithibitisha kupokelewa kwa majeruhi wawili, mama na mwanawe na mmoja kufa kabla ya kuanza kupatiwa matibabu kutokana na kuungua vibaya sehemu kubwa ya mwili wake.
Dk. Cesari alisema mama wa watoto hao wanaendelea kupatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.
Akizungumza kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Olomi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Hata hivyo, Kamanda Olomi hakuwa tayari kuzungumzia tukio hilo kwa undani kwa madai kwmaba alikuwa kwenye kikao.
NIPASHE













No comments:
Post a Comment