Wednesday, 8 July 2015

SIMULIZI ZA HASHIM ZUNGU ALIVYOBEBA "UNGA" KWA SIKU 55 TUMBONI

Ama kwa hakika kila binadamu hufanya makosa, lakini baadaye hujuta. Kama waswahili wasemavyo; majuto ni mjukuu, ndivyo ilivyokuwa kwa Hashim Hashim, maarufu kwa jina la Hashim Zungu.

Ni kijana mwenye umri wa miaka 35, aliyewahi kuwa ‘ngulu’ katika usafirishaji wa dawa za kulevya na baadaye mwenyewe kujikuta akitumbukia kwenye lindi la watumiaji dawa hizo.
Nilikutana na Zungu maeneo ya Mwananyamala A jijini Dar es Salaam kwenye mitaa anayopendelea kujumuika na wenzake.
Kwa ukarimu, ananikaribisha katika eneo tulivu alilolichagua tuketi ili tuzungumze.
Hashim au Zungu anaanza simulizi ya maisha yake akibainisha kwamba alizaliwa mwaka 1980, jijini Dar es Salaam, akiwa ni mtoto wa pili kati ya watatu wa Mzee Hashim Praful na Farid Bekker.
Baba yake ambaye kwa sasa ni marehemu ni Mtanzania mwenye asili ya India na mama yake (marehemu pia) ni raia wa Afrika Kusini, mwenye asili ya Uholanzi.
Zungu, alisoma katika Shule ya Msingi Upanga iliyoko Dar es Salaam na baadaye Shule ya Sekondari ya Al-Haramain, lakini hakumaliza kidato cha nne baada ya wazazi wake kufariki,
Anasema kuwa alijikuta akiingia kwenye biashara ya kusafirisha dawa za kulevya baada ya wazazi wake kufariki.
Anaeleza kuwa baada ya kufariki mama yake aliyekuwa tegemeo, hawakuwa na msaada mwingine kimaisha.
“Mama alipofariki, ndipo nilipoona dunia ikoje, maisha yalikuwa magumu sana. Tulikuwa tukilala nje, hata sehemu ya kuishi ilikuwa tabu,” anasema.
Zungu anasema hakuna yeyote aliyemshawishi au kumshauri aingie kwenye biashara ya dawa za kulevya, ila katika kutafuta maisha alikutana na mzee mmoja (jina limehifadhiwa), ambaye baadaye ndiye aliyekuwa akimtuma nchi mbalimbali kusafirisha dawa hizo.
Tajiri huyo wa kwanza ndiye aliyefanya naye kazi nyingi na kumtuma sehemu mbalimbali akisafirisha ‘unga.’
Hata hivyo, anaeleza kuwa wapo watu wengine zaidi waliowahi kumshawishi afanye biashara hiyo haramu kutokana na kuwa na asili ya Kizungu na Kihindi.
“Watu waliponiona nazurura, sina cha kufanya wakaniambia; dogo rangi yako inalipa, njoo ufanye kazi na kwa sababu unajua lugha, una uwezo wa kusafiri, nami nikashawishika kutokana na ugumu wa maisha,” anasema.
Safari ya kwanza Pakistan
Hashim Zungu anasema safari yake ya kwanza ilikuwa kusafirisha ‘unga’ Pakistan, kazi ambayo anasema alikuwa na woga uliokithiri.
“Kusafiri kwenyewe kulikuwa ni kwa kujipanga hasa, tulikuwa tunasafiri kwa utaratibu maalumu na kwa mipango,” anasema.
Anasema ili kuanza kazi hiyo ni lazima tajiri akutengenezee hati ya kusafiria na viza, wakati huo ilikuwa ni muhimu kuondokea jijini Nairobi, Kenya kwenye Uwanja wa Jomo Kenyatta. Hilo lilifanyika kwa sababu Tanzania na Uganda hazikuwa na ubalozi wa Pakistan.
“Unasafiri kwa basi mpaka Nairobi, ukifika pale unapanda ndege ya Emirates, unafika Dubai saa sita usiku, unalala Dubai. Asubuhi yake, saa 2 asubuhi unapanda ndege kuelekea Karachi. Kwa pale ni saa mbili unakuwa umefika,” anasema.
Anafafanua kwamba ukiwa Karachi unapanda ndege za ndani kwa safari ya saa mbili nyingine kuelekea katika mji wa Lahore, ambao unatajwa kuwa na Watanzania wengi wanaosafirisha dawa za kulevya.
Zungu anasimulia kwamba, ukiwa Lahore, utatakiwa kwenda katika mji wa Peshawar, ili kufika huko ni lazima uvuke mpaka wa Afghanistan na Pakistan na unatumia saa sita kufika.
Ukifika hapo Peshawar, unafungiwa unga au kumeza kisha unapanda ndege za ndani kurudi Karachi, ambako unatakiwa kulala hotelini.
Anasema kwa kawaida unga hautoki Tanzania, bali nchi nyingine na kufikishwa nchini kupitia mipaka mbalimbali, ikiwamo baharini.
“Ukifika hotelini Karachi, unatakiwa kuutoa ule unga na kuuosha ili upumzike kabla ya kuumeza tena, wakati huo unaangalia muda wa ndege kuondoka. Zikibaki saa mbili unachukua teksi kuelekea uwanja wa ndege ili kwenda Dubai, ”anasema.
Zungu anasema kuwa alikuwa akimwomba Mungu katika kila hatua alipokuwa akivuka mipaka na kusali sana wakati akikaguliwa.
Anaeleza kuwa wakati wa kurudi, alifika Dubai saa sita usiku kwa ndege ya Shirika la Emirates iliyokuwa ikielekea Afrika Kusini na baada ya hapo hutakiwa kuondoka na Malawi Airways kueleka Blantyre.
“Ukifika Blantyre unashuka na pale kuna watu wanakupokea, unaushusha na unawapa mzigo wao, unapanda gari kuelekea Lilongwe, Malawi, mwendo wa saa nane, ukimaliza unachukua gari unarudi Makambako,” anasema.
Jinsi alivyomeza dawa za kulevya
Zungu anaeleza jinsi kazi ya kumeza dawa za kulevya ilivyo na taabu akisema kuwa kwanza ni lazima mmezaji awe na ujuzi na afuate sheria na kanuni za kumeza.
Kwa mfano, hutakiwi kula vyakula laini, bali vigumu, kama wali, ugali, nyama iliyokaushwa. Lakini, pia mmezaji lazima awe amekula ameshiba.
“Unameza kama unavyomeza kitu chochote kile kama dawa au chakula, lakini unatakiwa uwe umekula umeshiba, ukimeza ukiwa hujala kitu, ule unga unashikana katika utumbo mkubwa na baadaye unaweza kugoma kutoka kwa njia ya haja kubwa na siyo ajabu mtu huyo akafanyiwa upasuaji au kupoteza maisha,” anasema.
Zungu anasema kwamba ni vyema chakula atakachokula kiwe kimejaa tumboni ili ule unga uelee usishikane na utumbo kwani ukishikana unauchana utumbo na dawa zinaweza kupasukia tumboni.
Anaongeza kuwa umezaji wake ni wa kupimiwa ili hesabu ya idadi ya kete isiharibike. Lakini, pia wakati wa kumeza, unameza kama unavyokunywa dawa, huku ukitumia maji kidogo. Unatakiwa kujizuia ili usitapike kwani ukitapika unachubuka koo.
“Mimi nilikuwa nameza kidogo kidogo, niliweza kuanza saa sita usiku kwa kumeza kete 40 hadi 50 kisha napumzika. Asubuhi ikifika nameza nyingine, lakini asubuhi ni lazima uombe Mungu. ukienda chooni uangalie iwapo tumbo lako linafanya kazi na lina uwezo wa kutoa pipi?” anasema.
Anasema kuwa ni muhimu kujua iwapo tumbo lako linafanya kazi kwa kutoa baadhi ya ‘pipi’ kwa njia ya haja kubwa na baada ya kujiridhisha kuzimeza tena.
“Kama unaondoka Jumatatu, unaanza kumeza kidogo kidogo kuanzia Jumamosi, siku ya Jumapili saa saba umeshamaliza, kisha unajiandaa kwa safari,” anasema.
Anaikumbuka safari yake ya kwanza kuwa ilimpa taabu zaidi kwa sababu alilazimika kunusa ‘unga’ kwa mara ya kwanza.
Kwa kawaida, kunusa unga kiasi kidogo, kunasaidia usijisikie kwenda haja kubwa, hivyo kuzuia kete za unga zisitoke.
“Siku ile siwezi kusahau, nilitakiwa kusafiri kwenda Pakistan kwa hiyo nikameza mzigo, lakini ili kuzuia nisiutoe, ikanibidi kama kawaida ninuse unga enzi zile ‘brown’,” anasema Zungu na kuongeza:
“Basi jicho langu likagoma kufunguka, kila nikijaribu kulifungua linagoma…nilisinzia wakati huo nilitakiwa kuelekea uwanja wa ndege.”
Anasema ilikuwa vigumu kwake kwa sababu alitamani kufumbua jicho, lakini alishindwa na kilichomtia shaka zaidi ni kwamba kufika uwanja wa ndege akiwa anasinzia kwani ni rahisi kutiliwa shaka na kukamatwa na wanausalama.
Katika safari hiyo ya kwanza, Zungu anasema alifamikiwa kupata Sh3 milioni ambazo hata hivyo hazikuwa nyingi kutokana na mzigo alioubeba na ugumu wa safari hiyo.
“Hazikuwa nyingi, lakini wakati ule ilikuwa ukibeba ‘vidude’ 120, sawa na kilo 1.2 nilistahili kulipwa Sh5 milioni na wakati mwingine ukimeza pipi 120, 100 ni za tajiri na 20 zako, hivyo pipi 20 ni sawa na Sh5 milioni, ” anasema na kuongeza: “Sikuweza kufanya biashara vizuri kwa sababu sikuwa na uzoefu.”
Changamoto nyingine ya safari zake ni kuwa baadhi ya matajiri wanaowatuma kazi hizo, wana tabia ya kuwapa fedha kidogo kidogo kama Sh500, 000 au milioni kwa sababu wanadhani kuwa wakiwapa fedha nyingi watazitumia vibaya.
Zungu anasimulia kwamba hakupata utajiri wa kutisha kwa kipindi hicho, lakini alipata fedha za kutosha kutimiza mahitaji yake ya kawaida hata kununua gari.
“Namshukuru Mungu nilipata fedha kiasi, nakumbuka mwaka fulani nilitaka kununua nyumba pale karibu na Mango Garden, Kinondoni, ilikuwa ikiuzwa Sh5 milioni na mimi nilikuwa na Sh4 milioni, hivyo sikununua, badala yake nilinunua gari aina ya Corolla,” anasema.
Hata hivyo, Zungu aliuza magari yake, baada ya kuanza kutumia dawa za kulevya.
Hawezi kusahau
Katika harakati za kuuza dawa za kulevya, Zungu amewahi kukutana na matukio mengi anayosema hataweza kuyasahau.
Anakumbuka Novemba 9, 2004 akiwa nchini Iran, ambako alikaa na kete 135 tumboni kwa siku 55. Alichokuwa akifanya ni kuzitoa kwa njia ya haja kubwa, kuziosha kisha kuzimeza tena.
“Ndugu yangu, siwezi kusahau, ujue unga ukiutoa hautakati unakuwa na kinyesi, hata ukibeua unasikia harufu ya kinyesi. Nilibeba pipi 135, ilikuwa ni kazi kubwa.
“Siku ya 56 nilipanda ndege kule Iran, nikatua Dubai, nikaingia Blantyre (Malawi) siku ya 57. Nikautua mzigo, nikaja Dar, siwezi kusahau,” Zungu anasimulia.
Kingine asichoweza kusahau ni tukio la mwaka huo, 2004, akitokea Iran, kupitia Malawi.
Anasema kuwa alipita Johanersburg, Afrika Kusini akiwa na mzigo wa dawa za kulevya tumboni na walikamatwa watu kumi akiwemo yeye. Walikamatwa walipokuwa wakishuka kutoka kwenye ndege.
“Nilijua ule ndiyo mwisho wangu. Kwanza, kwa sababu kipindi kile Afrika Kusini walikuwa wameshaongeza kifungo kutoka miaka 10 hadi miaka 25. Nilijua sasa hii ndiyo napotea… nitaishia hukohuko kwa sababu wakati ule nilikuwa na miaka 24, ukijumlisha miaka 20, ningetoka na miaka 44. Nina maisha tena hapo?” anasema.
Hata hivyo, baada ya kushuka aligundua kuwa waliokuwa wakihojiwa ni raia wa India, ambao walikuwa na tabia ya kuingia nchini humo kinyume cha sheria na kufanya uhalifu.
“Mimi sikuwa na shida kwa sababu nina pasipoti ya Kiafrika, nikawaambia nimekuja Afrika Kusini kukusanya kodi kwenye maduka ya mama yangu, waliridhika zaidi walipoona nina hati ya Tanzania,” anasema.
Hata hivyo, Zungu anasema alipoachiwa na kupanda kwenye ndege hali yake ilibadilika na kuwa mbaya kwani alijisikia vibaya na jasho lilimtoka kwa wingi.
“Nilipofika kwenye kiti cha ndege, hali ilibadilika nilijisikia vibaya, jasho linanitoka, nilikaa nimenyoosha miguu nalijisikia kutapika si kutapika, kuhara si kuhara,” anasimulia.
Anasema hali yake ilikuwa mbaya zaidi kwa sababu alikuwa amechomoa nusu ya kete kutoka kwenye haja kubwa, ambayo husaidia kuzuia haja kutoka.
“Niliichomoa ile kete kutoka haja kubwa kwa sababu nilidhani watanipekua, kwa hiyo nikaanza kusikia haja inatoka. Kama haja ikitoka basi ujue na unga unatoka, unapata hasara kwa sababu kipindi kile kete moja ni Dola 50…ukitoa kete 10 unapoteza fedha nyingi, we acha tu, ilikuwa hatari,” anasema na kuongeza:
“Basi ndugu yangu nilipata shida, najaribu kuizuia haja, nakaa kila mkao, mara nikunje nne, mara nibane miguu, mara nikae hivi mara vile.”
Lakini, tukio jingine asiloliweza kulisahau ni la mwaka 2007, alipokuwa akitokea Pakistan huku tumboni akiwa na mzigo wa kilo 1.2 na kwenye begi akiwa na kilo moja. “Siku hiyo Mungu mkubwa, nilikuja kimya kimya bila bughudha… nilikuwa nimebahatika, sikuulizwa wala kumhonga askari yeyote, wala sikusimamishwa na mtu yeyote pale Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, ”anasema.
Lakini, kumbe kuna watu walikuwa wanamfuatilia hatua kwa hatua hadi nyumbani kwake Temeke, Wailes. Wakati huo alikuwa ameficha baadhi ya unga kwenye tumbo na kwenye viatu. Unga mwingine alikuwa ameficha nyuma ya kioo cha meza aliyobeba. “Ilipofika saa 4:45usiku, watu watatu walikuja, nikakimbia, nikaruka ukuta wa nyumba, nikaruka kama mitaa minne, nyumba nane, nikatokea geti la nyuma, nikavuka barabara, nikatokea kituo cha mafuta, nikaingia nyumbani kwa watu, nikavuka hadi Uwanja wa Taifa nikakimbia,” anasema.
Alipofika barabarani alichukua teksi na kuamuru impeleke Tandale, lakini kwa wasiwasi alipofika huko hakutaka kulala na alitafuta usafiri ambao ulimpeleka Newala, Mtwara kwa bibi yake na kujificha huko kwa siku kadhaa.
Alivyoanza kutumia dawa
Mara zote unaposafirisha dawa za kulevya unajiweka katika mazingira ya kuzama katika uraibu.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwake (Zungu ). Mienendo yake ya kubeba dawa hizo kwa kuzimeza ilimfanya apate uraibu.
Kwa mfano, inapotokea akazitoa ‘pipi’ hizo kwa njia ya kuzitapika, huwa zinauchubua utumbo na unaweza kuuona ukiwa na damu damu kwa njia hiyo, ‘unga’ unaingia kwenye damu taratibu.
“Unga ni kama ujauzito, unaficha, lakini baadaye unajulikana. Utadanganya, lakini watu watajua,” anasema.
Zungu anasema unga ulishamwingia kwenye damu na alijikuta akianza kuvuta ambapo kwa siku aliweza kutumia Sh50,000 hadi 70,000 kununua unga.
“Ukiwa na Sh300,000 inaisha kwa siku tatu. Nilijidunga, nilivuta nilichanganya kwenye sigara hata na bangi. Yaani, nilikuwa ‘teja’ haswaa,” anasema.
Anasema ilifikia kipindi hata wale matajiri wake waliokuwa wakimtuma kusafirisha walianza kumkwepa kwa sababu walimwona ameshaharibikiwa kwa hiyo hakuwa tena akifanya safari za masafa ya Brazil, Pakistan, India wala Dubai.
“Ukishakuwa teja tu, familia inakutenga, watu wanakutenga, unaiba na unadanganya, watu wanakuuliza unavuta, unasema sivuti, uongo mwingi uliisha, lakini baadaye watu walijua,” anasema.
Zungu anasema pamoja na kujitahidi kujificha ili watu wasijue kuwa ameshatumbukia kwenye lindi la utumiaji wa dawa hizo, alibobea kiasi cha kuwa mwizi, kudanganya na kutapeli.
Hata mke wake wa ndoa naye alimkimbia baada ya kumwona amedhoofu mwili kwa kutumia dawa za kulevya.
“Mwisho, nikaona sasa hapa nitakufa kwa sababu unga ulikuwa unaingia kwenye damu, ukiamka asubuhi ukilala unga umeisha, unataka tena. Nikaona nitakufa, nikatuliza akili, nikamwomba Mungu,” anasema.
Anaongeza kuwa licha ya watu wengi kumtenga, lakini mwanamke mmoja, aliyemtaja kwa jina la Mwanaidi alimwona na kuamua kumsaidia kwa kumpeleka kwenye tiba ya kupungunza uraibu ya Methadone.
“Nilianza tiba Aprili 6, 2013, hapo Mwananyamala, na ninakunywa dawa kiasi cha miligram 250. Nimepunguziwa dawa na ninapimwa kila siku. Mungu akijalia mwanzoni mwa mwaka ujao, 2016, nitamaliza dawa na kuacha kabisa,” anasema.
Hashim anaeleza kujutia kila hatua aliyopitia ya kuuza na kutumia dawa za kulevya, lakini hatoacha kumshukuru Mungu kwa kumwondoa kwenye janga hilo na pia kumshukuru mke wake wa sasa, Mwanaidi kwa kumtoa kwenye uraibu wa dawa za kulevya.
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!