Saturday, 18 July 2015

SERINA LETARA: KUTOKA KUTEMBEZA MITUMBA OFISINI MPAKA KUANZA KIMILIKI KIWANDA"


MAFANIKIO yanatafsiri nyingi, wengine wakisema ni juhudi, wengine mawazo chanya na utayari wa kutokata tamaa katika kufikia malengo katikati ya changamoto.


Ndivyo anavyoweza kuelezewa Selina Letara, ambaye alianza kushona nguo akiwa na cherehani, akaingia katika biashara ya kutembeza nguo za mitumba katika ofisi mbalimbali jijini Dar es Salaam, leo ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni mbili na anatarajia kujenga kiwanda.
Mwanamke huyu pamoja na elimu yake kuwa ya kidato cha nne, lakini mafanikio aliyofikia na historia ya alikoanzia, vimemfanya asihofu kuzungumzia ndoto yake ya kuja kujenga kiwanda kwa ajili ya taulo za wanawake, ambacho tayari maandalizi yake yameanza kwa kununua eneo mkoani Shinyanga.
Alikotoka Mafanikio ya Selina ya leo ni matokeo ya juhudi kubwa zilizotengeneza sehemu muhimu ya historia ya maisha yake, ambayo leo imekuwa na mvuto wa aina yake kwa akinamama wengi, kwa kutoa hamasa wajishughulishe na kuongeza kipato chao.
Akizungumza na gazeti hili, Selina anasema baada tu ya kuolewa mwaka 1987 na Godfrey Letara, alijifunza ushonaji kwa kutumia cherehani na baadaye akachukua mafunzo ya muda mfupi ya kompyuta.
Pamoja na mafunzo hayo, anasema aliamua kuachana na kazi zinazotokana na mafunzo yake na kujikita katika biashara ya kununua na kuuza nguo za mitumba. Katika Jiji la Dar es Salaam, Selina anasema alikuwa akinunua nguo za mitumba kutoka Soko la Ilala na kutembeza nguo hizo maofisini na pia alijihusisha na biashara zingine ndogo.
Jitihada za kutafuta kazi atakayodumu nayo na kuikuza ziliendelea, ambapo mwaka 2000, Selina aliamua kurudi kwenye biashara yake ya ushonaji. Aliamua kufungua kiwanda cha kushona nguo, akiwa na mtaji wa vyerehani viwili tu katika maeneo ya Banana Ukonga na baadaye mumewe alienda nchini Kenya na kumnunulia mashine ya kudarizi.
Anasema alianza kazi ya kudarizi akiwa wa kwanza nchini kufanya kazi hiyo na kuanza kuomba kazi za zabuni za kushona sare katika kampuni na mashirika mbalimbali, lakini akakabiliwa na changamoto ya kukosa zabuni, kwa sababu hakuwa na kampuni.
*Kufungua kampuni
“Niliamua kufungua kampuni yangu na kuipa jina la Sinyati Enterprises. Maana ya Sinyati kwa Kimasai, ni kitu kilichobarikiwa na baada ya kuianzisha, nikaanza kupata zabuni mbalimbali kutoka kampuni na sehemu mbalimbali nchini,” anasema Selina. Zabuni zilianza kuongezeka na nyingine zilikuwa na vigezo ambavyo havipatikani nchini, ambapo Selina anasema alilazimika kupeleka kazi nyingine za mashati na nguo nyingine za sare nchini China.
Mapumziko,mawazo mapya
Mwaka 2009 baada ya mafanikio mazuri, Selina anasema aliamua kwenda nchini Singapore kwa mapumziko akiwa na mume wake na alipofika huko, alitumia taulo za wanawake ambazo hazikumpa athari yoyote tofauti na baadhi ya taulo nyingi za hapa nchini.
“Kwa kweli nilikuwa nikitumia taulo za hapa nchini, nawashwa na kuchubuka hadi nakosa raha, lakini nilipotumia hizo nchini Singapore, sikupata tatizo lolote nikaamua kununua nyingi kwa ajili ya kutumia na kurejea nchini,” anasema.
Anasema akiwa nchini alianza kutafakari na kuona kuna fursa ya kusaidia akinamama wengine wenye matatizo kama yake, akafikia uamuzi wa kwenda kwenye kiwanda kinachotengeneza taulo hizo za kike, kuomba kuwa wakala kuzisambaza hapa nchini. Mazungumzo na uongozi wa kiwanda hicho, anasema hayakuwa rahisi kwa kuwa walihisi angeweza kughushi utengenezaji wa bidhaa hizo, lakini baadaye walikubali awe msambazaji wao.
Biashara mpya
Mwaka huo huo wa 2009, makubaliano hayo yalianza kutekelezwa ambapo taulo hizo ziliingia nchini zikiwa na maelekezo ya lugha za Kichina na Kikorea na yeye alibandika karatasi yenye lugha ya Kiingereza na kuzipeleka kupimwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Baada ya kuthibitishwa na TBS na kupata alama ya ISO ya ubora wa kimataifa, Selina anasema aliunda kampuni ya ‘General Supplies’ na kuanza kuzisambaza nchini.
Anasema taulo hizo za kike zina ubora wa hali ya juu kwa kuwa zimetengenezwa kwa pamba kwa asilimia 100, huku zikiwa na jani maalumu la mchaichai ambalo halina kemikali wala madhara yoyote, lenye ubaridi kwa ajili ya kumlinda mwanamke, kuzuia joto, kuondoa harufu na muwasho.
Pia wanasambaza taulo za aina nyingine ziitwazo Cherish, ambazo hazina jani hilo, hivyo hazina ubaridi lakini ubora wake unafanana kwani ziko kwa ajili ya wasiopenda ubaridi huo. Mbali na taulo hizo, aliamua kusambaza bidhaa zingine zinazotengenezwa kwa tunda la mzeituni (oliver oil) ikiwemo shampoo, losheni na sabuni za maji ya kuogea zenye ubora.
*Matarajio, kiwanda
Akizungumzia matarajio yake ya baadaye, Selina anasema katika ushonaji, wanakarabati ofisi ili iwe kubwa zaidi ambapo kwa sasa ana vyerehani 70, ambapo akiwa na zabuni kubwa mafundi wote wanakuwepo, lakini akiwa na zabuni za kawaida anatumia mafundi 10 waliopo kila siku.
Katika usambazaji wa taulo za kike, ana mawakala 10 nchini na wafanyakazi 15 huku akiwa na mpango wa kujenga kiwanda mkoani Shinyanga, ili atengeneze taulo hizo zenye ubora na tayari amenunua ekari nane za ardhi.
Lengo la kujenga kiwanda hicho, Selina anasema licha ya kutengeneza taulo zenye ubora kwa kutumia pamba kwa urahisi mkoani Shinyanga, anatarajia kukinga akinamama na magonjwa mbalimbali yanayotokana na matumizi ya taulo zisizo na ubora na kutoa ajira kwa wananchi wa mkoa huo.
Katika maandalizi hayo, anasema anajipanga kuandikia Serikali mpango wa biashara wa ujenzi wa kiwanda hicho kwa nia ya kumwezesha kupata mkopo usio na riba kubwa. Changamoto Selina anasema amekuwa akikabiliana na changamoto mbalimbali katika kuendesha biashara zake, ikiwa ni pamoja na watu kuelezea bidhaa zake za taulo vibaya bila kujua ubora wake.
Changamoto zingine anasema ni katika kupata mikopo benki, kwa kuwa kumekuwa na riba kubwa jambo linalochangia washindwe kuendesha biashara zao kama wanavyotarajia. “Suala lingine ni taarifa ya Serikali kuanza kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye taulo za kike wakati ni kifaa tiba kwa ajili ya magonjwa, hivyo kuongeza gharama kwa akinamama,” anasema.
Anatoa rai kwa Watanzania wanaponuanua bidhaa kuzisoma na kuzielewa, ili waachane na uvumi unaotolewa na washindani wa biashara na ikiwa wataona utata katika bidhaa yoyote, watumie mawasiliano yaliyopo kwenye bidhaa hizo, ili kupata uhakika wa wanachosikia kuliko kuendelea kueneza uvumi katika mitandao.
Anatoa ushauri kwa akinamama nchini kutoogopa kuanza biashara kwani kwa fedha kidogo na mradi mdogo kama wa bustani, wanaweza kupata mafanikio na anasisitiza kuwa jambo la msingi ni kuwa na bidii katika kuongeza kipato.
*Kujiendeleza kielimu, familia
Katika kujiendeleza kielimu, anasema Septemba mwaka huu anatarajia kuanza masomo ya utawala katika biashara, kwani sasa anafanya biashara kubwa, hivyo analazimika aende na wakati kwa kuelewa utawala wa biashara na masuala mengine. Kwa kuwa yeye ni mama, anasema anaweza kumudu biashara zake na familia kwa kupanga muda wake vizuri, kuhakikisha anamhudumia mume na watoto wake.
Akizungumzia ratiba yake, anasema kila siku asubuhi lazima aende Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kariakoo ndiyo aanze shughuli zake. Akitoka kazini saa 10, anakwenda kufanya mazoezi na akirudi nyumbani kazi yake ni kuhakikisha mumewe anakula vizuri chakula cha jioni.
Anasema anafanya majukumu yote ya mumewe mwenyewe na hata siku moja hamuachii msichana wa kazi kila kitu, tofauti na baadhi ya wanawake ambao wakiwa na biashara kubwa, huwa jeuri kwa wanaume zao pamoja na kumsahau Mungu.
Selina alizaliwa mwaka 1965 mkoani Arusha na kupata elimu katika Shule ya Msingi ya Musa na baadaye akajiunga na Shule ya Sekondari Naboishu, alikosoma kidato cha kwanza mpaka cha nne. Baada ya kumaliza kidato cha nne, anasema alichukua Astashahada ya Biashara katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kwa mwaka mmoja na baadae kusoma masomo ya kompyuta mwaka 1987.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!